Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa vifo vya watu watatu vilivyotokea katika msitu wa Hifadhi ya Korogwe Fuel, uliopo wilayani Handeni mkoani Tanga, familia imesema maziko yatafanyika Jumamosi, Septemba 28, 2024.
Jonais Shao (46), Mkaguzi wa Ndani katika Halmashauri Wilaya ya Korogwe, mkazi wa Bagamoyo wilayani humo, mwanaye Dedan Shao (8), mwanafunzi wa darasa la tatu, na mtumishi wake wa ndani Salha (18) walifariki dunia kwa kuchomwa moto, tukio lililotokea Septemba 23, saa tatu usiku.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi akizungumza na waandishi wa habari jana alisema Polisi lilipokea taarifa kuwa ndani ya msitu huo kuna gari aina ya Toyota IST lenye namba za usajili T 305 EAL linaungua moto na pembeni yake kuna watu wawili wakiungua.
Alisema askari waliofika eneo hilo walikuta gari hilo likiungua moto na pembeni yake kukiwa na watu wawili wameungua kwa moto na kufariki dunia ambao walikuwa na jinsia ya kike na ndani ya gari kiti cha nyuma ulionekana mwili mwingine ambao uliungua hadi kupoteza sura.
Msitu wa Korogwe Fuel unamilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Handeni.
Alipotafutwa na Mwananchi leo Jumatano Septemba 25, Kamanda Mchunguzi amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.
Kwa upande wake, Lameck Shao ambaye ni mume wa Jonais amesema miili imeshafanyiwa uchunguzi.
Akizungumza na Mwananchi leo jioni amesema tangu asubuhi Polisi wamekuwa wakienda nyumbani kwake kwa mahojiano.
“Tangu asubuhi Polisi wanakuja kuhoji, wanaondoka na kurudi tena. Tunatarajia kuzika Jumamosi, eneo la Mwika mkoani Kilimanjaro,” amesema Shao.
Kuhusu binti wa kazi Salha, amesema wamepata mawasiliano ya ndugu zake hivyo naye atasafirishwa kwa ajili ya maziko.
Jonais alifikwa na kadhia hiyo muda mfupi baada ya kuwasili Korogwe, akitokea Dar es Salaam ambako pia ana makazi.
Akizungumza na Mwananchi jana Septemba 24, Shao alisema alikuwa akiwasiliana na mkewe hadi Septemba 23, saa tatu usiku kabla ya mawasiliano kukatika.
“Tuliwasiliana vizuri hadi saa tatu kwamba amefika nyumbani baada ya hapo akawa hapatikani, nilijaribu kutafuta namna ya kupata mawasiliano hadi asubuhi ya leo (Septemba 24) nilipomtuma kijana wa shamba aende pale nyumbani.
“Baada ya kufika, yule kijana hakukuta mtu na alipozungumza na majirani walibaini milango iko wazi. Tulianza kufuatilia ndipo mchana tuliposikia taarifa kwamba kuna watu wameungua kwenye gari,” alisema.