Straika Fountain Gate katikati ya Maabad, Mgaza

MMOJA wa wachezaji  wanaofanya vizuri Ligi Kuu Bara msimu huu ila hazungumzwi sana ni mshambuliaji wa Fountain Gate FC, Seleman Mwalimu ‘Gomez’, kutokana na kiwango bora anachokionyesha.

Gomez aliyesajiliwa na Fountain msimu huu akitokea KVZ ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), msimu uliopita aliibuka mfungaji bora jambo linalosubiriwa kuona rekodi zake zitakuwaje katika kikosi hicho cha mjini Babati.

Msimu uliopita, Gomez akiwa KVZ alihusika na mabao 27 kwenye michezo 27 kati ya 30 ambapo alifunga 20 na asisti saba, na hadi sasa ameshatupia matatu Fountain Gate.

Nyota huyo amefunga mabao matatu kati ya tisa yaliyofungwa na kikosihicho kwenye michezo mitano, huku baadhi ya nyota waliowika kutoka Zanzibar misimu ya  karibuni wakishindwa kutamba Bara.

Miongoni mwa walitabiriwa makubwa ni Maabad Maulid wa Coastal Union ambaye pia alitoka huku akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), ila ameshindwa kuendana na kasi ya Bara.

Maabad alijiunga na Coastal Julai 11, 2022 akitokea KVZ alikoibuka mfungaji bora mara mbili mfululizo 2020-2021 mabao 17 na 21 ule wa 2021-2022. Licha ya rekodi hiyo tangu ajiunge na Coastal Union hajafikisha hata mabao matano Ligi Kuu kwani 2022-2023 alifunga manne na uliopita matatu.

Msimu huu nyota huyo amefunga bao moja  katika sare ya 1-1 dhidi ya KMC.

Mbali na Maabad, mwingine ni Yassin Mgaza  aliyekuwa mfungaji bora ZPL akiwa na KMKM 2022-2023 ambapo alifunga mabao 17 na kutoa asisti nane kwenye michezo 25.

Kwa maana hiyo, Mgaza alihusika katika mabao 25 akiwa KMKM kwenye michezo 25 kati ya 30 msimu mzima ikiwa ni msimu wake wa kwanza Ligi ya Zanzibar na kuivutia Dodoma Jiji kumsajili.

Mgaza alijiunga na KMKM akitokea Mbuni inayoshiriki Championship kwa sasa alikohusika na mabao 22 kwenye michezo 16 akifunga 16 na asisti sita.

Baada ya kutua Dodoma alijikuta akiangukia pua baada ya kufunga mabao matatu msimu mzima.

Msimu huu Gomez ni miongoni mwa washambuliaji tegemeo Fountain Gate na jambo ameanza vizuri hivyo kilichobaki ni kusubiri kuona kama ataendeleza kiwango bora.

Akizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na mwenendo huo, Gomez alisema Ligi Kuu Zanzibar ni tofauti na Ligi Kuu Bara kwa ushindani na hata mchezaji mmoja mmoja ingawa amejipanga kufanya vizuri kama KVZ.

“Haina maana wachezaji wanaotoka Zanzibar hawawezi kufanya vizuri Bara kwa sababu mifano ipo mingi kwa waliofanikiwa. Ligi ya huku ni ngumu kwani unakutana na mastaa wengi wenye uzoefu mkubwa walikotoka hivyo sio rahisi kihivyo.”

Related Posts