Teknolojia mpya yatumika kujenga maghala Ruvuma

Ruvuma. Imeelezwa kuwa, maghala 28 ya nafaka  yanayojengwa chini ya Wizara ya Kilimo mkoani Ruvuma, yanatumia teknolojia bora na ya kisasa.

Meneja Miradi wa Kampuni Alaf Limited, Julius Nalitolela amesema hayo jana Jumanne Septemba 24, 2024 baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala hayo eneo la Luhimba- Madaba, Songea mkoani Ruvuma.

Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi  nafaka mkoani Ruvuma katika eneo la Luhimba- Madaba, Songea. Kushoto ni Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.

Nalitolela amewahakikishia wakazi wa Ruvuma kuwa, mradi huo ukikamilika utakuwa na  viwango vya kudumu muda mrefu.

Pia, ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa hatua hiyo akisema Alaf inayotekeleza mradi huo imekuwa na teknolojia ya kisasa kabisa katika ujenzi huo.

Wakati wa  uwekaji wa jiwe hilo la msingi, Rais Samia aliongozana na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe na viongozi wengine wa Mkoa wa Ruvuma.

“Teknolojia hii inatumika kwa mara ya kwanza kabisa na sisi kama kampuni inayotekeleza mradi huu chini ya Wizara ya Kilimo tuna uhakika hili ni suluhisho la kudumu kwa sababu tumezingatia ubora wa hali ya juu,” amesema Nalitolela.

Amesema paa za maghala hayo zinajengwa kwa kutumia bidhaa ya saflock ambayo haivujishi kabisa nyakatia za mvua.

“Bidhaa nyingine inayotumika katika mradi huu ni chuma aina ya Light Gauge itakayotumika kujenga ofisi na vyoo.

“Ni nyepesi, rahisi kusafirisha, imetengenezwa kwa mfumo wa kompyuta, hakuna mabaki katika eneo la kazi, sio rafiki kwa mchwa, haipati kutu, ni salama kutokana na muundo wake na ujenzi wake ni wa muda mfupi,” amesisitiza Nalitolela.

Meneja Mradi kutoka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula iliyo chini ya Wizara ya Kilimo, Injinia Iman Nzobonaliba amesema mradi huo ukikamilika utaweza kuhifadhi nafaka takribani tani 28,000.

“Baada ya kukamilika kwa mradi huu ambao una ubora wa hali ya juu suala la uhaba wa maghala ya kuhifadhi nafaka katika Mkoa wa Ruvuma utakuwa historia,”amesema Nzobonaliba.

Ameeleza kuwa, mradi huo ambao umekamilika kwa asilimia 90 unatarajiwa kukamilika kabisa ifikapo Novemba mwaka huu.

Alaf Limited iliyoanzishwa mwaka 1960 ni kampuni inayotengeneza mabati ya kuezekea nyumba  na inaendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini.

Related Posts