Vijana 12 wabuni roboti inayopiga picha za video

Dodoma. Changamoto ya wapigapicha kusimama muda mrefu wakichukua picha za matukio mbalimbali, imewasukuma vijana 12 wa ngazi tofauti za elimu kutengeneza roboti linaloweza kufanya kazi hiyo.

Ubunifu huo umekuja kutokana na hatua ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuonyesha roboti Eunice wakati ilipokuwa ikiwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni Dodoma, Mei mwaka huu.

Mkurugenzi wa studio inayojihusisha na kurekodi video katika matukio mbalimbali ya KBTIT iliyopo jijini Dodoma na mmoja wa wataalamu walibuni teknolojia hiyo, Brighton Katabazi amesema wazo hilo walilibuni na kuanza utekelezaji mwaka jana.

Katika ubunifu huo, amewashirikisha wataalamu wa vifaa vya umeme, chuma, mbao na aluminium, wakisaidiwa ushauri na Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Eletroniki na Mawasiliano Pepe, Ndaki ya Tehama ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Baraka Maiseli.

Amesema kilichowasukuma kubuni teknolojia hiyo ni baada ya kuona watu wanaofanya kazi hiyo husimama muda mrefu kurikodi video hasa kwenye shughuli za harusi na matukio mengine ya kijamii.

Amesema roboti hiyo inafanya kazi mchana na usiku, kwa kuwa imefungwa taa na hivyo husaidia kuongeza mwanga wakati wa usiku unapohitajika na inatumia rimoti katika wakati wa upigaji wa picha za video.

“Wakati mwingine wapigapicha wamekuwa wakisimama juani wakati unayemrikodi yuko kivulini na hata ukiacha kamera pekee yake muongeaji akihama mbele ya kamera inabidi usogeee kurekebisha kamera.

“Wakati mwingine anaangalia mahali pengine na hivyo anapoteza ubora wa picha,” amesema.

Amesema changamoto hizo ndizo zilizowasukuma kubuni teknolojia hiyo mwaka jana, kwa kutengeneza roboti itakalosimama na kamera na kupiga picha zenye ubora unaotakiwa.

Amesema kupitia roboti hiyo, mtumiaji huisogeza kwa kutumia rimoti mahali anapotaka iende na kupiga picha bila kulazimika kusogea mahali palipo na  kamera.

“Hapa unaweza kutumia rimoti kuisogeza roboti kwa kadri unavyopona katika screen unataka iwe na hivyo unapata picha zilizobora bila mtu kulazimika kwenda kukaa juani ama kusimama muda mrefu,” amesema.

Amesema malengo yao ni kuiboresha roboti hiyo, ili ifanye kazi nyingine yenyewe badala ya kutumia rimoti katika utendaji wake wa kazi (akili mnemba).

Katabazi amesema utengenezaji wa roboti hiyo umefikia asilimia 45 ambapo wametumia Sh3.5 milioni na wanatarajia hadi kukamilika itatumia Sh15 milioni.

Amesema changamoto wanazokutana nazo ni muda mchache wa kukutana kwa ajili ya kutekeleza mradi huo, kwani hulazimika kufanya shughuli nyingine kwa ajili ya kujipatia kipato.

“Tunaomba Serikali itusaidie eneo la kufanyia shughuli hii kwa kuwa bado tunafanyia majumbani, kwa sababu hapa tulipo ni studio ndogo hivyo tukikaa tunawaziba wateja wanaokuja kupata huduma mbalimbali,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri aliyefanya uzinduzi wa awali wa roboti hiyo, amewapongeza kwa ubunifu huo ambao ni wa kwanza kufanyika katika jiji la Dodoma na kuwashauri kuboresha mwonekano wake ili ifanye vizuri sokoni.

“Ufanyaji wa kazi unawezekana ukawa sawa, lakini kwa muonekano huo, utafanya mtu avutike kununua bidhaa yako? Hata kama bidhaa itakuwa nzuri namna gani, kama haivutii ukiangalia inaweza kukupotezea wateja,” amesema.

Amewashauri kuandika mradi wao vizuri wa kutengeneza roboti na kisha kuomba mkopo wa asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Pia amewataka kwenda mbali zaidi kuangalia jinsi wanatakavyowezesha roboti hiyo kufanya kazi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kwenye viwanda na shambani.

Shekimweri amesema Serikali itawasaidia kufikia maono yao waliyopanga.

 “Naona jambo kubwa hapa, ninawaomba mfikirie katika ukubwa huo huo,”amesema Shekimweri.

Kwa upande wake, Profesa Maiseli amesema zipo changamoto zikifanyiwa kazi zitaboresha teknolojia hiyo nchini, ikiwemo miundombinu ya kurahisisha teknolojia hiyo ifanye kazi vizuri.

Amesema bado kuna changamoto ya mtandao wa intaneti kutopatikana ama kasi yake kuwa ndogo, jambo linalokwamisha maroboti hayo kufanya kazi kwa ufanisi.

Amesema changamoto nyingine ni vitendea kazi ambavyo ni kompyuta ama mashine zinafanya kazi kwa kasi zaidi ambazo zinaitwa GPU.

“Bado mashine hizi katika nchi zinazoendelea hazipo, hizi ndizo zinazofanya roboti lifanye kazi kwa ufanisi mkubwa na kusiwe na delay (kuchelewa),” amesema.

Amesema inatakiwa Serikali na wadau wengine kusaidia kuwekeza katika eneo hilo, ili kuboresha utendaji kazi wa maroboti yanayobuniwa.

“Vijana katika eneo hili nimeona wana ari kubwa, wakipewa mentorship nzuri na kwa ukaribu watafanya kitu kizuri zaidi.

Hata sasa naitwa na vijana kwenye laboratory (maabara) kuangalia kazi zao za roboti na unakuta wanakaa hadi saa sita usiku wakifanya kazi hizo,” amesema.

Roboti na tishio la ajira

Wakati Serikali ikiweka mikakati ya ubunifu wa kiteknolojia, ukiwamo utengenezaji roboti, kumekuwa na hofu ya vijana kupoteza ajira.

Hata hivyo, hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC), Dk Nkundwe Mwasaga, amebainisha kuwa roboti ni sehemu muhimu ya maendeleo ya kiteknolojia duniani na zinategemea akili ya binadamu kwa programu na uendeshaji.

Amesema hayo alipozungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na kuwahakikishia kuwa roboti hazitachukua nafasi ya wafanyakazi wa binadamu kikamilifu.

“Hakuna haja ya kuogopa kwa sababu uwezo wa binadamu haujabadilika. Hakuna roboti duniani zilizofikia asilimia 100 ya uwezo wa binadamu, wala haziwezi, kwani zinadhibitiwa na programu za kibinadamu,” amesema Dk Mwasaga.

Katika ziara hiyo ambayo ilijumuisha maonyesho ya roboti (Eunice), Mkurugenzi Mtendaji wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike amesema tishio halisi kwa ajira si roboti, bali ni programu za kompyuta.

“Tunahitaji kufundisha vijana kuelewa ni nani atakayekuwa mfanyakazi wa baadaye,” amesema.

Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) inakadiria kuwa karibu vijana milioni 10 hadi 12 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka barani Afrika, lakini ni vijana milioni 3.1 pekee wanaopata ajira. Pengo hilo linaacha mamilioni ya vijana bila ajira, na litaongezeka kadiri zana za kidigitali zinavyozidi kutumika kazini.

Naibu Makamu Mkuu wa UDOM, Profesa Razack Lokina ameonyesha matumaini juu ya mwelekeo wa Serikali na kupongeza juhudi za vyuo kama UDOM na taasisi kama Nelson Mandela African Institution of Science and Technology kwa kuanzisha programu za sayansi ya roboti.

Profesa Lokina amesisitiza kwa kukumbatia maendeleo ya kiteknolojia na kuwekeza katika ujuzi mpya, vijana watafanikiwa katika uchumi wa kidigitali.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts