Viongozi mbali mbali wa dunia wameendelea kuhutubia mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa mjini NewYork, wengi wakitoa mwito wa amani na kumalizwa kwa migogoro kuanzia Mashariki ya kati hadi barani Afrika.
Rais Cyril Ramaphosa akiwa miongoni mwa viongozi wa Afrika waliohutubia amesisitiza kwamba juhudi zaidi zinahitajika kuvimaliza vita katika nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan.
Rais Cyril Ramaphosa aligusia masuala mengi kwenye hotuba yake jana jioni mbele ya hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa akiwa ni miongoni mwa viongozi wa mwanzo wa Afrika waliohutubia baraza hilo.
Alisisitiza juu ya amani Mashariki ya Kati akiapa kwamba hawezi kukaa kimya na kuacha kuzungumzia kile alichosema ni ubaguzi wa rangi unaoendelea kufanywa dhidi ya jamii nyingine.
Sambamba na hayo kiongozi huyo wa Afrika Kusini aliigusia migogoro mingine inayoendelea duniani ikiwa ni pamoja na barani Afrika akiweka wazi kwamba juhudi zinapaswa kuongezeka kuitatuwa migogoro hiyo.
“Dhamira yetu ni kuendelea kuona kwamba juhudi zinaongezeka kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi Sudan na Yemen mpaka Ukraine na katika pia kanda tete ya Sahel.Tunapaswa kuzingatia pia lengo ya watu wa Sahara magharibi ya kuwa na uhuru wao.”
Ametilia mkazo juu ya suala hilo la kutowakilishwa vyakutosha kwa bara la Afrika na watu wake katika mifumo ya kufanya maamuzi ya kimataifa kupitia Umoja wa Mataifa ,akisema Afrika imetengwa.
Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amewaambia viongozi wengine kwenye mkutano huo wa kilele kwamba baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapaswa kufanyiwa mageuzi ya dharura yatakayohakikisha kinaifanya taasisi hiyo kuwa inayozijumuisha sauti za mataifa yote.
Alikumbusha kwamba wakati nchi yake Afrika Kusini itakapochukuwa uwenyekiti wa kundi la nchi zilizoendelea na zinazoinukia kiuchumi duniani la G20 itatumia fursa hiyo muhimu kupigia upatu malengo ya Waafrika na mataifa yanayoendelea.
Ama viongozi mbali mbali wa dunia jana walitowa mwito wa kufanyika juhudi za kuwekeza zaidi katika nishati mbadala ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi huku mataifa yanayoendelea yakisema yanahitaji msaada wa kifedha kuingia kwenye kipindi hicho cha mpito cha kuachana na nishati inayochafuwa mazingira.
Pembezoni mwa mkutano huo wa hadhara kuu ya Umoja wa Mataifa unafanyika mkutano wa kilele wa kujadili nishati mbadala ambako rais wa Kenya William Ruto alitowa kilio cha Afrika akisema bara hilo linapokea chini ya asilimia 50 ya uwekezaji wote unaofanywa duniani katika miradi ya nishati jadidifu licha ya bara hilo kuwa kitovu cha asilimia 60 ya fursa za nishati ya jua duniani.
Aliwataka viongozi wa dunia kuwekeza zaidi katika nishati jadidifu barani humo kama sehemu ya ahadi iliyotolewa mwaka jana na mataifa ya ulimwengu katika mkutano wa kilele wa COP28 ya kuongeza mara dufu kiwango cha uwekezaji wa nishati isiyochafuwa mazingira kufikia mwaka 2030.
Kwa upande mwingine rais wa Angola Joao Lourenco alitahadharisha kwamba hakuwezi kuwepo ulimwengu wenye usawa na salama na wenye maendeleo ya kudumu ikiwa hakuna hadhi na fursa sawa kwa kila mmoja.