Zanzibar yaingiza Sh10 bilioni usajili wa meli 840

Unguja. Kwa kipindi cha miaka minne, Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) imesajili meli za nje 800 na za ndani 40, hivyo kukusanya Sh10.167 bilioni.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 25, 2024 na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Nadir Abdulatif katika mkutano wa 16 wa Baraza la Wawakilishi alipojibu maswali ya wajumbe wa baraza hilo.

Abdulatif alikuwa akijibu swali la msingi la Mwakilishi wa Mtambwe, Dk Mohamed Ali Suleiman aliyeuliza kuhusu idadi ya meli zilizosajiliwa na ZMA, kiwango cha fedha ambacho kimepatikana na namna Serikali inawezesha meli zilizosajiliwa na mamlaka hiyo, kutoa fursa kwa mabaharia wenye asili ya Zanzibar kufanya kazi.

Akijibu swali hilo la msingi, Abdulatif  amesema meli za nje zilizosajiliwa zina uzito wa GT 3,068,376, huku meli za ndani zikiwa na uzito wa GT 58,115. Usajili huo ni kuanzia mwaka 2020 hadi mwaka 2024.

Kuhusu mabaharia wazawa kuajiriwa katika meli za kimataifa zinazosajiliwa kupitia ZMA na changamoto wanazokabiliana nazo, amesema utaratibu wa kuajiri mabaharia katika meli ni suala la biashara ya mmiliki wa meli kuchagua kutoka nchi anayotaka.

“Hata hivyo, mamlaka inaendelea na mazungumzo kuwashawishi wenye meli kuona mabaharia wetu wenye sifa kuajiriwa katika meli hizo,” amesema.

Amesema mabaharia wazawa wamekuwa wakiajiriwa katika meli za nje kupitia Kampuni ya Danaos yenye makao makuu nchini Ugiriki.

Amefafanua kwa sasa kampuni hiyo ina jumla ya mabaharia 841 ambao wako kwenye meli na vijana 1,500 wanasubiri kupangiwa kuingia kwenye meli ambao tayari wameshafanyiwa usaili kwa kuajiriwa kupitia kampuni hiyo.

Akizungumzia njia wanazotumia kukabiliana na changamoto za mabaharia wanaofanya kazi kwenye meli za kimataifa na namna wanavyopata stahiki zao, amesema Serikali inasimamia na kuhakikisha baharia anapatiwa mkataba kabla ya kuanza kazi.

Pia, hutatua migogoro inayojitokeza kati ya mabaharia na wenye meli.

“Pia  tunawapatia mafunzo ya vitendo mabaharia melini kwa kusimamia kanuni ya masilahi ya mabaharia ya 2019 na kanuni za uchunguzi wa afya za mabaharia ya 2019.”

Related Posts