AKILI ZA KIJIWENI: Baleke pale Yanga akaze sana

JANA nilimsikia kocha wa Yanga, Miguel Gamondi akizungumza kitu juu ya straika wake anayesotea benchi, Jean Baleke ambaye Yanga ilimsajili katika dirisha kubwa la usajili lililofungwa mwezi uliopita.

Gamondi alisema kuwa mshambuliaji huyo raia wa DR Congo ana kazi kubwa ya kufanya ili apate nafasi ya kucheza mbele ya Clement Mzize na Prince Dube ambao ndio wamekuwa wakipata nafasi kubwa kikosini.

Kauli hiyo aliitoa siku moja kabla ya mchezo wa timu yake dhidi ya KenGold uliochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, juzi Jumatano ambao Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

“Kwenye mfumo wangu ninataka mshambuliaji mmoja. Dube anafunga mabao na anafanya vizuri.  Mzize anafunga mabao na anafanya vizuri. Nikimuweka Baleke maana yake nimtoe Dube au Mzize, kwa nini? Hakuna sababu ya ziada.

“Ninachoweza kusema kuhusu Baleke ni kwamba nina utajiri wa wachezaji wengi wazuri kwenye nafasi yake. Kama binadamu najisikia vibaya kwa sababu ninataka kumpa nafasi Baleke lakini nikimuweka Baleke ninatakiwa nimtoe Mzize au Dube,” alisema Gamondi.

Ukiitafsiri vizuri kauli hiyo ya Gamondi utakubaliana na mimi kuwa bado Baleke hajaonyesha kiwango bora katika viwanja vya mazoezi ambacho kitamshawishi kocha huyo na benchi lake la ufundi kumpa nafasi mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba.

Baleke ana udhaifu fulani ambao unachangia kwa kiasi kikubwa kipaji chake cha kufumania nyavu kuonekana ni cha kawaida mbele ya makocha wa timu anazozichezea.

Mchezaji huyo amekuwa na masihara sana nje na ndani ya uwanja ambayo kuna wakati yamekuwa yakifanya makocha wamuone kama ni mtu ambaye hayupo siriazi na kazi yake hivyo kuamua kutompa kipaumbele mbele ya wachezaji wengine wa nafasi yake.

Lakini soka la sasa linahitaji mshambuliaji ambaye anajishughulisha mara kwa mara na mchezo tofauti na Baleke ambaye yeye mara nyingi hupenda kusimama na kusubiria mipira ije afunge kitu ambacho kitampatia ugumu wa kupata nafasi mbele ya kocha kama Gamondi.

Baleke ana mtihani mgumu pale Yanga na anahitajika kujituma hasa ili aweze kuufaulu.

Related Posts