NAFURAHISHWA na kazi ya kufumania nyavu ambayo inafanywa na washambuliaji wazawa wanaozichezea timu mbalimbali za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pale Fountain Gate vinara wa kufumania nyavu ni Seleman Mwalimu na Edgar William ambao hadi wakati akili za kijiweni inapoandikwa, walikuwa tayari kila mmoja ameshaifungia mabao matatu timu hiyo.
Ukienda Azam kuna Nassor Saadun ambaye katika mechi mbili za nyuma mfululizo aliifungia timu hiyo kwenye ligi akianzia dhidi ya KMC na kisha akafanya hivyo dhidi ya Coastal Union, kabla ya Azam kuvaana na Simba usiku wa jana.
Tena alifunga mabao ya kideoni ambayo yalıkuwa ya uwezo binafsi kuonyesha kuwa hakuyafunga kwa kubahatisha au yalitokana na uzembe wa mabeki wa timu pinzani.
Katika kikosi cha Yanga kuna Clement Mzize ambaye amekuwa tegemeo la kocha Miguel Gamondi na anaelekea kuwa chaguo la kwanza katika nafasi ya mshambuliaji wa kati mbele ya wageni Prince Dube, Kennedy Musonda na Jean Baleke.
Simba kwenye kikosi chao wana Valentino Mashaka ambaye amekuwa na mwanzo mzuri katika Ligi Kuu akiifungia timu hiyo mabao mawili yanayomfanya awe miongoni mwa wachezaji walio nafasi za juu katika chati ya kuwania ufungaji bora.
Hili ni jambo lenye faida sana kwa nchi yetu kwa vile wazawa hao wanaonyesha uwezo wa kufumania nyavu katika kipindi ambacho Taifa lilianza kuwa na uhaba wa washambuliaji wazawa kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa, Taifa Stars.
Kama wachezaji hao watakuwa na muendelezo mzuri wa hicho wanachokifanya maana yake benchi la ufundi la Taifa Stars litakuwa na wigo mpana katika uteuzi wa kikosi cha timu hiyo siku za usoni tofauti na sasa ambapo haina machaguo mengi kwa wachezaji wa nafasi za ushambuliaji.
Jambo jingine la kuvutia ni kwamba wachezaji hao wote wana umri mdogo hivyo wana nafasi ya kutumikia timu yetu ya taifa kwa muda mrefu na hata kusogea mbali zaidi kwa kufuata malisho ya kijani katika ligi kubwa za ndani na nje ya Afrika.