Mbeya. Hatimaye, Pascolina Mgala alliyekuwa ameshindwa kutibiwa kwa kukosa Sh200,000, sasa atafikishwa katika Hospitali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi.
Hatua hiyo inatokana na uongozi wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kuiona taarifa yake kupitia Gazeti la Mwananchi na hivyo kumsaidia kupata matibabu zaidi.
Pascolina (20) mkazi wa Kijiji cha Nambinzo wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe, anasumbuliwa na uvimbe wa mguu wa kulia kwa miaka tisa bila kujua chanzo chake.
Binti huyo aliyefiwa na baba mzazi, kabla ya kuibuliwa na Gazeti la Mwananchi lililofika nyumbani Kijiji cha Nambinzo, alikuwa akilelewa na bibi yake Rainess Mwampashi (77).
Pascolina alifikia hatua ya kulelewa na kikongwe huyo kutokana na kutelekezwa na baadhi ya ndugu zake kutokana na ugonjwa huo alioupata tangu 2015 alipojikwaa.
Hata hivyo, katika harakati za kupambana na jeraha hilo, operesheni ya awali lilitolewa jiwe ambalo halikueleweka ambapo operesheni ya pili alishindwa kuifanya baada ya kukosa Sh200,000 mwaka 2019.
Baada ya Mwananchi kuibua changamoto ya binti huyo aliyeshindwa kuendelea na masomo akiishia kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Mageuzi, serikali kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbozi iliamua kumsaidia kugharamia matibabu yake.
“Tayari amepelekwa hospitali wilaya na kama atahitajika kwa rufaa ya mkoani ama Muhimbili tayari nimekwisha elekeza cha kufanya, tutashirikiana pamoja ili mtoto apone,” amesema Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esta Mahawe alipozungumza na Mwananchi mwanzo wa wiki hii.
Pascolina ameanza safari leo jioni Septemba 26, 2024 kwa basi la Rungwe Express akisindikizwa na Ofisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mbozi, Mathias Siwale na moja ya ndugu wa ukoo, Sista Msukwa.
Akizungumza kabla ya kuanza safari kuelekea Dar es Salaam katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Pascolina amesema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake kwake, viongozi wilaya na Watanzania wote.
Amesema hakufahamu kama atapata huduma ambayo amehudumiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, lakini ameona matumaini mapya kwa jinsi madaktari walivyompokea na kumhudumia.
“Namshukuru Rais Samia, amekuwa pamoja na mimi, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Gazeti la Mwananchi na Watanzania kwa jinsi wanavyonisaidia, bado nahitaji maombi yao na msaada zaidi,” amesema Pascolina.
Bibi wa binti huyo, Rainess Mwampashi amesema amepata taarifa za mjukuu wake kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwaomba Watanzania kwa ujumla kumuombea ili aweze kupona.
“Mimi naendelea vizuri japokuwa najisikia kuumwa, nimepewa taarifa asubuhi kuwa anapelekwa Muhimbili, niwaombe Watanzania kumwombea ili apone,” amesema Rainess.
Mtoa huduma ngazi ya Jamii, Sikujua Msukwa ambaye alikuwa naye kwa kipindi chote hospitalini hapo, amesema Watanzania wamekuwa bega kwa bega na binti huyo akiwaomba kutochoka kwa michango ya hali na mali.
Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk Godlove Mbwanji amesema walimpokea mgonjwa huyo na kupewa huduma bora na hadi sasa walikuwa wanasubiri majibu ya vipimo.
“Tangu apokelewe alipata huduma muda wote na ilichukuliwa nyama kupelekwa kwenye vipimo hivyo, inamaana ataandikiwa taarifa ya vipimo ‘Medical Report’,” amesema Dk Mbwanji.
Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole amesema yupo Dar es Salaam kumsubiri mgonjwa huyo na tayari ameshaandaa mazingira mazuri ya kupata huduma.
“Ninajua hali yake ilivyo, nasubiri aje na hizo nyaraka za vipimo ili aendelee na huduma, taarifa zake nyingine zipo kwa Mkurugenzi wa Tiba hapa Muhimbili,” amesema mbunge huyo.