WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani amepokea msaada wa vifaa tiba kwa ajili ya hospitali ya Msoga na madawati 120 kwa ajili ya shule za msingi mbili za Chalinze.
“Kwa mujibu wa takwimu za makusanyo na mapato, NMB- Chalinze ndiyo tawi namba moja Tanzania kwahiyo maana yake NMB wanapozungumza tunapata Bilioni 500 ni pamoja na mchango mkubwa wa Chalinze”. Alisema Kikwete.
Kikwete amezishauri sekta binafsi nyingine nyingi kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi ili kuwa na uchumi endelevu na kurudisha kwa wananchi ambao ndiyo wateja wakuu.
Tukio hilo muhimu la ustawi wa wananchi limefanyika mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, Mkurugenzi wa Halmashauri Ramadhani Possi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze Hassani Mwinyikondo huku benki ya NMB iliyotoa msaada huo ikiongozwa na Mkuu wa Idara ya Mitandao ya Matawi na Mauzo ya NMB Ndugu Renatus Richard.