Benki ya Access yakidhi vigezo ununuzi wa BancABC Tanzania

Dar es Salaam. Iliyokuwa Access Bank PLC imekamilisha mchakato na kukidhi vigezo vya kisheria na kikanuni vya ununuzi wa African Banking Corporation Tanzania Limited (BancABC Tanzania) huku ikiahidi hatua hiyo itaongeza ufanisi zaidi.

Ununuzi wa benki hiyo unaifanya sasa taasisi hiyo kuitwa Access Bank Tanzania Limited.

Mkurugenzi Mtendaji wa matawi ya Access Bank barani Africa, Seyi Kumapayi akizungumza Septemba 25, 2024 katika hafla fupi amesema:

“Hatua hii ni hatua muhimu sana katika mkakati wetu wa ukuaji Afrika Mashariki, ikithibitisha dhamira yetu ya kuchangia maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania. Kwa kuunganisha BancABC Tanzania katika kundi la Access Bank, tutaongeza uwezo wetu wa kutoa masuluhisho mbalimbali ya kifedha kukidhi mahitaji ya wateja wetu yanayobadilika kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi.

“Lengo letu ni kuwezesha biashara zaidi kati ya nchi za Africa, huku tukiendelea kuinua jamii kwa kulenga hasa wanawake na vijana, kupitia huduma bora za kibenki na fursa za kifedha,”amesema na kuongeza Kumapayi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Access Bank Tanzania, John Imani amesema hatua hiyo itaongeza ubora wa huduma wanazozitoa kutokana na uzoefu wao.

 “Tunafuraha kubwa kuwa sehemu rasmi ya familia ya Access Bank. Hatua hii inafungua fursa mpya kutokana na ubobevu wa taasisi zote mbili zinazounda benki imara zaidi na yenye ushindani wa hali ya juu utakayokidhi mahitaji ya wateja wetu. Tunaahidi kuendelea kutoa huduma bora huku tukikua pamoja nchini Tanzania.”

Imani ameongeza kuwa: “Ununuzi huu utawanufaisha wateja wa Access Bank Tanzania kwa kuwa na huduma zenye kiwango cha kimataifa, na mfumo wa kipekee wenye ushirikiano wa kimataifa. Zaidi ya hayo, uwepo wa Access Bank unaimarisha biashara barani Africa kwa kujenga daraja la miamala ya kibenki ndani na ya nje ya nchi kwa ufanisi zaidi kwa kuleta suluhisho za kisasa kwa kutumia ushirikiano wake na wadau wake wa kimataifa.”

Related Posts