Dar es Salaam. Baada ya kukwama kufikishwa mahakamani Jumatatu hili, leo Alhamisi, Septemba 26, 2024 Meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo jijini Dar es Salaam, Boniface Jacob, anatarajiwa kufikishwa tena mahakamani kwa ajili ya uamuzi wa hatima ya dhamana yake.
Jacob, maarufu Boni Yai, Mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasa anakabiliwa na kesi ya uchapishaji taarifa za uwongo kwenye mitandao.
Alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Alhamisi Septemba 19, 2024 na kusomewa mashitaka mawili, ambayo hata hivyo aliyakana.
Upande wa mashitaka uliieleza Mahakama upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika lakini ukawasilisha maombi mawili, kwanza Mahakama iamuru atoe nywila (password) za simu zake na ya akaunti yake ya mtandao wake wa X (zamani Twitter) ili vifanyiwe uchunguzi na mpelelezi.
Pia, uliomba Mahakama izue dhamana yake kwa madai ni kwa usalama wake, huku wakidai maombi hayo yanatokana na kile mshitakiwa alichomweleza Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO) wa Kinondoni, Davis Msangi kuwa baada ya taarifa hizo alizoziandika anajua atatekwa na kuuawa.
Maombi hayo yalipingwa vikali na jopo la mawakili wa Boni Yai lililoongozwa na Peter Kibatala, wakidai kuwa hoja hizo hazina mashiko na maombi hayo hayakuwasilishwa kwa mujibu matakwa ya kisheria.
Hivyo waliiomba Mahakama iyatupilie mbali na badala yake impe masharti ya dhamana mshtakiwa wakidai dhamana ni haki ya msingi ya Kikatiba, na suala la usalama si moja ya mambo yanayoweza kusababisha mshtakiwa anyimwe dhamana.
Hakimu Mfawidhi Franco Kiswaga anayesikiliza kesi hiyo baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, Septemba 23, 2024 kwa ajili ya uamuzi wa maombi hayo ya Serikali.
Hata hivyo, Jumatatu ya Septemba 23, 2024 Boni Yai ambaye yuko mahabusu katika Gereza la Segerea hakuweza kufikishwa mahakamani hapo pamoja na mahabusu wengine hapo, jambo lililosababisha uamuzi wa hatima ya dhamana yake kuahirishwa mpaka leo, Alhamisi Septemba 26, 2024.
Wakizungumzia kuahirishwa kwa uamuzi huo, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga na kiongozi wa Jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala walisema kuwa Boni Yai hakufikishwa mahakamani kwa sababu za kiusalama, kulingana na hali ilivyokuwa siku hiyo.
Siku hiyo ya Jumatatu ya Septemba 23, 2024 kulikuwa na maandamano yaliyopangwa kufanywa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), pamoja na mambo mengine kupinga matukio ya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa viongozi wake.
Katika kesi hiyo Boni Yai anakabiliwa na mashitaka mawili.
Mashtaka hayo ni kuchapisha taarifa za uwongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti ya X yenye jina la Boniface Jacob @Ex MayorUbungo kwa nia ya kupotosha umma kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandano namba 14 ya mwaka 2015.
Alisomewa mashitaka hayo na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali, Nurati Manja.
Katika shitaka la kwanza Wakili Manja alidai, Septemba 12, 2024 jijini Dar es salaam alichapisha taarifa za uwongo zikimuhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP).
Taarifa hizo zinasomeka kuwa:
“Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji moja kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”
Katika shitaka la pili, Wakili Manja alidai Boni Yai alitenda kosa hilo Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam akidaiwa kuchapisha taarifa za uwongo zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.
Ujumbe huo inasomeka kuwa:
“Mkawasifia Ma-RCO (Wakuu wa Upelelezi Mikoa) wanaozuia uhalifu kwa kutenda uhalifu…bali Ma-RCO waliokuwa wa kuteka, kukamata, kupiga watuhumiwa risasi, kuwafunga tape, kuwafunga mifuko ya nailoni usoni na kisha kutupa miili ya watuhumiwa ndio wanaijua kazi ya upolisi.”