DPP ashinda shauri la ‘shangingi’ lililobeba wahamiaji haramu

Dar es Salaam. Raia wa Tanzania anayeishi Afrika Kusini, Jackson Ngalya anayedai gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 namba T888 BTY lililokamatwa na wahamiaji haramu mjini Moshi ni mali yake, amekwaa kisiki baada ya Mahakama kutupa maombi yake.

Mahakama imekubali hoja mbili kati ya tatu za pingamizi lililowekwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), kutokana na dosari za kisheria alizobaini katika maombi hayo namba 21838 ya mwaka 2024.

Gari hilo lilikamatwa Juni 4, 2024   Njipanda ya Himo, likiwa na wahamiaji haramu saba, raia wa Ethiopia waliokuwa wakisafiri kuelekea Afrika Kusini, ambao baadaye walitiwa hatiani na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kifungo cha mwaka mmoja jela.

Tangu kukamatwa kwa gari hilo na baadaye Mahakama kukubali litaifishwe kuwa mali ya Serikali baada ya kukubali ombi la DPP, hakuna mtu aliyejitokeza kudai ni mmiliki hadi Julai 31, 2024 alipojitokeza Ngalya.

Gari hilo liliingizwa na kusajiliwa mwaka 2011 kwa jina la mbunge mmoja wa CCM lakini umiliki ukahama Juni 24, 2024 kwenda kwa Ngalya ikiwa ni baada ya kupita siku 20 tangu likamatwe na umefanyika likiwa mikononi mwa vyombo vya dola.

Hili liliibua maswali mengi yasiyo na majibu ya namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilivyoruhusu uhamisho wa gari ambalo ni kielelezo cha kesi.

Katika kiapo cha maombi dhidi ya DPP na raia hao saba wa Ethiopia, Ngalya alidai kuanzia mwaka 2016 hadi sasa, amekuwa akiishi Afrika Kusini na kwamba gari hilo aliliacha nyumbani kwake nchini Tanzania, chini ya uangalizi wa mlinzi.

Kwa mujibu wa kiapo hicho, Juni 2024 alijulishwa kuwa gari lake halijulikani lilipo, hivyo Juni 3, 2024 alikwenda Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam kutoa taarifa.

Alidai kupitia vyombo vya habari aligundua gari lake lilihusika katika usafirishaji wa wahamiaji haramu na linashikiliwa likihusishwa na kesi ya jinai namba 16397 ya 2024 iliyokuwa ikiwakabili wahamiaji hao.

Katika kiapo alieleza alishangazwa baada ya ufuatiliaji alipobaini limehusika katika kesi hiyo ya jinai, akisisitiza gari hilo ni mali yake na hana ufahamu wa aina yoyote na jinai iliyotendwa na washtakiwa.

DPP ambaye ni mjibu maombi wa kwanza katika shauri hilo aliwasilisha pingamizi la awali (PO) akiegemea hoja tatu za dosari za kisheria zinazofanya kiapo cha Ngalya aliyekuwa akitetewa na wakili Mandera Mzirau kiwe batili kisheria.

DPP katika hoja ya kwanza alidai hati za uthibitisho za kiapo cha mleta maombi hazikuwa zimethibitishwa na kamishina wa viapo na hazikuonyesha zilisainiwa wapi, hivyo kukiuka kifungu cha 8 cha Sheria ya Viapo ya mwaka 2019.

Kwa mujibu wa DPP, takwa la kifungu hicho liko wazi na ni la lazima, haliwezi kuondolewa na upande wowote.

Kwa msingi huo, alidai hapakuwa na kiapo sahihi cha kuunga mkono maombi ya mwombaji kwa kukiuka takwa hilo la kisheria.

DPP katika hoja ya pili alidai hati ya kiapo cha Ngalya ina dosari isiyoweza kutibika kwa kuwa na maombi katika aya ya 10, akieleza hilo si sehemu ya vigezo vinne vinavyofanya hati ya kiapo iwe sahihi kisheria.

Kupitia kwa Wakili wa Serikali, Makore Mahere, DPP katika hoja ya tatu alidai katika sehemu ya uthibitishaji kiapo, mwombaji taarifa zote alizotoa ni kwa ufahamu wake, kile anachokiamini na ni kwa uelewa wake.

Wakili Mahere alidai mwombaji alitakiwa kufafanua ni taarifa zipi ni za kweli au ni taarifa zipi sahihi kwa ufahamu wake, akisisitiza alipaswa kuainisha aya ambazo anathibitisha ni ukweli au kama ni taarifa basi aeleze chanzo chake.

Akijibu hoja hizo wakati wa usikilizwaji pingamizi Agosti 30, 2024 Wakili Mandera Mziray aliyemwakilisha Ngalya alikiri kiapo hicho kuwa na dosari.

Hata hivyo, alidai kifungu cha 8 kinapaswa kisomwe kwa pamoja na kifungu cha 9 cha sheria hiyo ya viapo.

Alidai dosari inayotajwa katika kifungu cha 8 inaweza kutibika kupitia kifungu cha 9 na kwamba, kama Mahakama itakubaliana naye, basi wapewe fursa kufanya marekebisho na si kuyatupa maombi.

Alidai kwa kuwa taarifa za kiapo hicho zilitokana na ufahamu wa mwombaji na kile anachokiamini, hakutakiwa kueleza chanzo chake katika sehemu ya uthibitisho ya kiapo.

Katika uamuzi alioutoa Septemba 20, 2024, Hakimu Mkazi Mkuu, Opotuna Kipeta wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi, amesema hoja inayopaswa kujibiwa na Mahakama ni iwapo hoja za pingamizi zikubaliwe au la.

Hakimu Kipeta amesema wakili Mziray amesema dosari iliyoonekana katika kiapo inaweza kutibiwa na kifungu cha 9 lakini sheria inataka kutajwa kwa anayeapa, kiliapwa wapi, na lini mwenye kiapo aliapa.

“Baada ya kupitia kiapo cha mwombaji, ni sahihi kuwa kiapo chake hakina saini ya ofisa anayeshuhudia kiapo, mahali na anuani kiapo kilipoapwa, na tarehe kiapo hicho kiliapwa na mwombaji,” amesema hakimu.

“Hii ina maana kuwa kiapo hakikuchukuliwa, na kama kiapo hakikuchukuliwa ni vizuri kusema hapakuwa na kiapo cha kuunga mkono maombi haya. Nasema hivyo kwa sababu ni taarifa inatolewa kwa njia ya kiapo kwa ofisa anayeruhusiwa.”

Hakimu amesema, “kwa hiyo kukosekana kwa saini, tarehe, mahali na anuani ya wapi kiliapwa kama inavyoonekana kwenye kiapo hiki maana yake hapakuwa na kiapo na kiliwasilishwa mahakamani kikikiuka kifungu hicho cha 8.”

Amesema takwa hilo ni la lazima kwa kiapo chochote, hivyo hoja ya wakili wa muombaji kuwa kifungu cha 9 kinaweza kutibu ukiukwaji unaoonekana haiwezi kusimama, hivyo pingamizi la DPP lina mashiko na linakubaliwa.

Kuhusu hoja ya tatu kuwa kulikuwa na dosari za kisheria katika sehemu ya uthibitisho, hakimu amesema baada ya kupitia kiapo hicho anakubaliana kuwa ni batili kwa vile sheria inataka kueleza ni yapi ni kwa ufahamu wake.

Hakimu amesema sheria imeweka takwa la lazima kueleza chanzo cha taarifa za kiapo na kwamba, kushindwa kuzingatia kifungu hicho inakifanya kiwe batili.

Amesema hoja hizo mbili zinatosha kuyatupa maombi hayo. Muombaji ameamriwa pia kulipa gharama za shauri hilo.

Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro, Fakih Nyakunga Juni, 2024 alizungumzia namna wahamiaji walivyokamatwa wakiwa katika gari hilo ambalo dereva wake alitoroka.

“Jana (Juni 4, 2024), tukiwa kwenye majukumu yetu ya kazi maeneo ya Himo tulikamata raia saba wa Ethiopia waliokuwa wakielekea Afrika Kusini. Tunaendelea na taratibu za uchunguzi na baadaye kuwafikisha Mahakamani,” alieleza.

Wahamiaji hao walifikishwa kortini Juni 14, 2024 na kusomewa mashitaka mawili na mwendesha mashitaka, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Issack Mangunu. Walikiri kutenda makosa hayo ya jinai.

Washitakiwa hao ni Tensa Matwis, Abi Arose, Buruk Helobo, Arigudo Aromo, Sisy Abera, Mirhetu Sulore na Sharifan Betiso.

Usikilizwaji wa awali ulipagwa kufanyika Julai 2, 2024.

Shitaka la kwanza ilidaiwa Juni 4, 2024 Njiapanda wilayani Moshi raia wa Ethiopia washitakiwa waliingia nchini kinyume cha sheria wakitumia gari lenye namba za usajili T888 aina ya Toyota Land Cruiser.

Kosa la pili ilidaiwa siku hiyohiyo katika eneo hilo, walikutwa kinyume cha sheria wakiwa ndani ya ardhi ya Tanzania bila kuwa na hati halali za kusafiria au nyaraka yoyote ya kisheria inayowaruhusu kukaa nchini.

Julai 2, 2024 Hakimu Mkazi, Rehema Olambo aliwahukumu washtakiwa kulipa faini ya Sh500,000 kila mmoja au kwenda jela kutumikia kifungo cha mwaka mmoja. Walishindwa kulipa faini wakapelekwa gerezani.

Related Posts