Ennovate Ventures yawaita wajasiriamali kuchangamkia ufadhili wa kibiashara

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Ufadhili unatolewa na Taasisi ya Ennovate Ventures inayojihusisha katika kukuza uchumi wa Afrika kwa kuunga mkono biashara zinazoanza na kukua utaongeza usaidizi kwa wafanyabiashara na kuwawezesha kustawi, imeelezwa.

Akizungumza Septemba 25,2024 na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mmoja wa Washirika katika taasisi hiyo, Francis Omorojie, amesema wafanyabiashara wa Afrika wana jukumu kubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya bara hilo lakini bado wengi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.

“Tunalenga kuziba pengo la wafanyabiashara wa Kiafrika wasioonekana kwa kutoa rasilimali zinazoshughulikia changamoto muhimu kama vile ufadhili na uwekezaji. Mpango huu unawalenga wajasiriamali ambao bunifu zao zina uwezo wa kubadilisha mazingira ya biashara ya Afrika lakini wamekosa usaidizi unaohitajika ili kustawi,” amesema Omorojie.

Mkuu wa Masoko katika Ennovate Ventures, Jasmine Abdallah, amesema wanatoa ushauri wa kibiashara kwa wanaoanza kwa lengo la kukuza biashara zao kwa sababu wamegundua wajasiriamali wengi wana changamoto na wengine hawapati taarifa sahihi za fursa mbalimbali.

“Tunaona sasa hivi wawekezaji wengi duniani wanakuja kuwekeza Afrika na macho yao wameelekeza pia Tanzania, lakini tumegundua wajasiriamali wengi wana changamoto na hawapati taarifa sahihi za uwepo wa fursa zilizopo.

“Cha kwanza tunachofanya ni tathmini kuelewa kampuni yako iko katika hatua gani, shida inayokukabili na msaada unaouhitaji kama ni kupeleka bidhaa zako nje au huwezi kupata ‘board members’, tunatoa pia ufadhili kuanzia Dola 10,000 mpaka 20,000,” amesema Jasmine.

Amesema pia watakaokidhi vigezo watapata nafasi ya kushiriki katika mkutano mkubwa wa wawekezaji utakaofanyika Afrika Kusini ambapo wawekezaji zaidi ya 200 kutoka sehemu mbalimbali duniani watashiriki.

Kwa upande wake Mkuu wa Masoko wa Kampuni ya Simba Money ambayo imeingia ubia na taasisi hiyo, Anna Chinyoyo, amesema wanajihusisha na huduma za kifedha zinazofanyika kwa njia ya kidigitali na kwamba wanahakikisha vijana wanaoingia kwenye programu hiyo wanapata uungwaji mkono wa kutosha ili kufanikisha ndoto zao.

Related Posts