KAYA 2,700 KATIKA VITONGOJI 90 VYA MKOA WA NJOMBE KUSAMBAZIWA UMEME

Wakala wa Nishati Vijijini (REA); tarehe 25 Septemba, 2024 imemtambulisha rasmi mkandarasi ambaye ataanza rasmi Mradi wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 90 vya mkoa wa Njombe ambapo imeelezwa kuwa kaya 2,700 zitanufaika na huduma ya umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji (HAMLET ELECTRIFICATION PROJECT); Mradi umetengewa shilingi bilioni TZS 10.07.

Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Njombe; Katibu Tawala wa mkoa huo, Bi. Judica Omary ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Nishati katika mkoa wa Njombe na kuongeza kuwa nishati ya umeme, imewezesha Sekta nyingine za kiuchumi kuchangia uchumi wa Mtu mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.

“Umeme kwa Watu wa Njombe umechangia kutoa ajira rsmi na zisizo rasmi, tunaendelea kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwa wigo wa miundombinu ya umeme unaendelea kuongezeka, awali tulipata kilomita tatu (3) za umeme kwenye vijiji na sasa tumepata kilomita mbili (2) zaidi kwenye vitongoji, niwaombe Wananchi wa Njombe, wachangamkie (Wajiunganishe) na nishati ya umeme mara Miradi ya umeme inapokamilika, nguzo zinaendelea kusogezwa karibu zaidi kwa watu”.

“Sisi kama mkoa, tutaendela kuwapa ushirikiano Wakandarasi wa China Railways Construction Electrification Bureau Group na ninatoa wito kwa Wataalam wetu wa mkoa kuwapa ushirikiano.” Amekaririwa Katibu Tawala wa mkoa, Bi. Judica Omary.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Njombe Mjini, Mhe. Deo Mwanyika ameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza kwa vitendo Miradi ya nishati vijijini.

“Tunaishukuru Serikali kupitia REA kwa Miradi kama hii, natoa wito kwa Mkandarasi, kuanza mara moja ujenzi wa miundombinu ya kusambaza umeme kwenye vitongoji, kulingana na jiographia ya eneo letu na hali ya hewa, kwetu hapa Njombe umeme ni kila kitu”. Amekaririwa, Mhe. Deo Mwanyika.

Awali, Msimamizi Miradi ya REA, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi, Dunstan Kalugira alisema Mikataba kwa ajili ya miradi ya kupeleka umeme kwenye vitongoji ilitiwa saini tarehe 20 Agosti, 2024 ambapo lengo la mradi ni kupeleka miundombinu ya umeme katika vitongoji 15 ambavyo vimepitiwa na umeme wa msongo wa kati kwa kila Jimbo.

Mhandisi, Kalugira ameongeza kuwa, Mradi wa Kusambaza Umeme kwenye Vitongoji kwa mkoa wa Njombe, unatekelezwa na Mkandarasi kutoka China, kampuni ya China Railways Construction Electrification Bureau Group (CRCEBG) kwa gharama ya shilingi bilioni 10.07 na unakadiriwa kukamilika, ndani ya siku 730.

Ameongeza kuwa, Mradi utahusisha ujenzi wa umeme wa msongo mdogo wa kilomita 180; ujenzi wa mashine umba tisini (90); kuunganisha Wateja wa njia moja 2,700 na kuunganisha Wateja wa njia tatu 270.

“Katibu Tawala pamoja na Viongozi, baada ya REA kumtambulisha Mkandarasi kwa Uongozi wa mkoa, Mkandarasi ataanza kufanya mapitio ya njia za mradi (Details survey) na kuendelea na utekelezaji wa mkataba wake kulingana na wigo wa Mradi.” Amekaririwa, Mhandisi, Kalugira.




Related Posts