WATETEZI wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), JKU ubingwa inautaka tena baada ya juzi kuendelea kugawa dozi katika ligi hiyo na kuzidi kujiimarisha kileleni mwa msimamo ikiifyatua Tekeleza ya Pemba kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Gombani, visiwani humo.
Mabao mawili kutoka kwa kinara wa orodha ya Wafungaji wa ligi hiyo, Mudrik Abdi Shehe na jingine la Adam Ibrahim Abdalla yalitosha kuwapa JKU ushindi wa tatu mfululizo na kufikisha pointi tisa kileleni na mabao 15 ya kufunga hadi sasa.
Mudrik aliyefikisha jumla ya mabao saba hadi sasa kupitia mechi mbili tu, akiwamo matano aliyofunga katika mechi iliyopita walipoisambaratisha Mwenge kwa mabao 9-0, juzi alianza kwa kufunga bao dakika ya saba kabla ya kuongeza jingine dakika ya 20.
Tekeleza iliyopanda daraja msimu huu sambamba na Junguni pia ya Pemba, Inter Zanzibar na Mwembe Makumbi za Unguja, ilitulia baada ya kufungwa mabao hayo mawili, lakini umakini mdogo wa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iliifanya iende mapumziko ikiwa nyuma kwa 2-0.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kuongeza kasi ya mchezo, lakini ni JKU iliyonufaika kwa kuongeza bao la tatu dakika ya 60 likiwekwa kimiani na mtokea benchi Adam Ibrahim Abdalla likiwa bao lake la kwanza msimu huu na kuwakatisha tamaa wenyeji, Telekeza ambao hicho ni kipigo cha tatu katika michezo minne iliyocheza hadi ikiwamo ule wa sare dhidi ya KVZ na kuwapa pointi moja pekee.
Kwa mujibu wa ratiba ni kwamba ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena kwa mchezo mmoja tu kati ya mabaharia wa KMKM dhidi ya maafande wenzao wa Uhamiaji ambapo kila moja ilipata ushindi katika mechi zilizopita.
KMKM iliisambaratisha Zimamoto kwa mabao 4-1, huku Uhamiaji ikiizima wageni wa ligi hiyo Inter Zanzibar kwa mabao 2-1.