Mkandarasi mzawa achechemea mradi wa HEET

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omar Kipanga ameuagiza uongozi wa Kampuni ya ukandarasi ya Comfix kufika ofisini kwake Dodoma Oktoba 2, 2024 kufuatia kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa kampuni hiyo kwenye utekelezaji wa mradi wa ujenzi katika Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT).

Kampuni hiyo imepewa kazi ya ujenzi wa majengo mawili ya chuo hicho ambayo ni jengo la maktaba na utawala kwa gharama ya zaidi ya Sh21 bilioni ujenzi ambao umefikia asilimia 30.7 huku ukitakiwa kukamilika Mei mwakani.

 Akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa miundombinu ya chuo hicho kampasi kuu ya Butiama, leo Septemba 26, 2024, Msimamizi Mwelekezi wa mradi, Dk Adonis Kamala amesema mkandarasi huyo ameshindwa kwenda na kasi inavyotakiwa licha ya kupewa maelekezo mara kwa mara.

“Huu mradi unatekelezwa na makandarasi kutoka  China lakini pia kuna mkandarasi mzawa ambaye ndiye Comfix, wachina wao wapo sawa lakini mwenzetu mzawa mambo yake hayaridhishi hasa ukizingatiwa yeye ndiye alikuwa kwa kwanza kufika eneo la kazi lakini wenzake walifika kwa kuchelewa na tayari wako mbali kiutekelezaji,” amesema.

Amesema hadi sasa hakuna mkandarasi anayedai malipo kwa maelezo kuwa katika mradi huo serikali inajitahidi kulipa kwa wakati tofauti na miradi mingine ambayo amewahi kusimamia.

“Nina miaka 36 kwenye hii kazi lakini niseme kweli huu mradi serikali inautendea haki yaani ukiandika hati ya malipo ndani ya siku saba unakuwa umelipwa ingawa utaratibu ni kwamba unatakiwa ulipwe ndani ya siku 28 huu mradi ni kama ule wa Bwawa la Mwalimu Nyerere malipo yanawahi tofauti na miradi mingine ambayo nimeismimia,” amesema

Kufuatia hali hiyo, Naibu Waziri Kipanga ameutaka uongozi wa juu wa kampuni hiyo kufika ofisini kwake kwa majadiliano na hatua zaidi kwa maelezo kuwa serikali haiko tayari kuona mradi unashindwa kukamilika kwa wakati.

Kipanga amesema ili mabadiliko ya mitaala na sera ya elimu yaweze kutekelezwa kwa ufasaha na tija ni lazima viwepo vyuo vya kati na vikuu vitakavyokuwa na uwezo wa kutoa elimu katika masuala ya umahiri na amali hivyo chuo hicho ni moja ya vyuo vinavyotegemewa katika kufanikisha jambo hilo.

“Hapa kutakuwa na kozi za kilimo, madini,nishati na nyinginezo ambazo kiuhalisia ndio mwelekeo wa mtaala na sera yetu mpya ya elimu kwahiyo hatuko tayari kuona tunakwamishwa kutimiza haya,” amesema.

Amesema ili kufanikisha sera hiyo kwa vitendo serikali ilipokea mkopo kutoka benki ya dunia kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya zaidi ya Sh970 bilioni ambapo zaidi ya asilimia 70 ya mkopo huo umeelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya vyuo ambapo mikoa 14 inatarajiwa kunufaika huku akisema katika utekelezaji wa miradi hiyo chuo cha MJNUAT ndicho kinaongoza hadi sasa.

Mwakilishi wa Kampuni ya Comfix, Justine Mwikwabe amesema wako nyuma kwenye utekelezaji wa mradi huo kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo mvua nyingi wakati walipokabidhiwa mradi.

“Tumekabidhiwa mradi mwezi Novemba,2023 na hadi sasa tuna asilimia 30.7 na tumeshapokea malipo kwa asilimia 37 tuna amini mradi utakamilika mwezi Mei, 2025 kama inavyotakiwa, changamoto ilikuwa ni mvua wakati mrafi unaanza,” amesema Mwikwabe

Akitoa taarifa ya Chuo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Lesakit Mellau amesema ujenzi wa mradi mkubwa wa miundombinu ya chuo katika kampasi kuu ya Butiama kwa ujumla umefikia asilimia 37.68 ya utekelezaji wake.

Amesema mradi huo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh102.5 bilioni unahusisha ujenzi wa mkubwa wa miundombinu ya chuo ikiwepo majengo ya utawala, hosteli zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 800, vyumba vya mihadhara, madarasa, mgahawa, maktaba,barabara pamoja na miundombinu mingine na kwamba mradi huo ukikamilika chuo hicho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi zaidi ya 6,000 kwa wakati mmoja.

 “Hadi sasa tumepokea kiasi cha Sh51.8 bilioni ambapo pamoja na changamoto za hapa na pale tumefikia asilimia 37.68 ambapo mkandarasi wanatakiwa kukabidhi kazi zao kuanzia Mei hadi Novemba mwakani hii ni kulingana na mkataba na aina ya kazi kwani kazi zinatekelezwa na makandarasi watatu tofauti,” amesema

Kuhusu udahili wa wanafunzi, Profesa Mellau amesema wanatarajia kudahili wanafunzi 150 mwaka huu wa masomo baada ya kudahili wanafunzi 28 mwaka wa masomo 2023/24 kufuatia ukarabati wa miundombinu ya iliyokuwa Shule ya Sekondari ya wavulana ya Oswald Mang’ombe ambayo hivi sasa inatumika.

 Amesema chuo hicho amabcho kilikaa zaidi ya miaka saba bila kudahili wanafunzi kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu hivi sasa kina uwezo wa kudahili idadi hiyo ya wanafunzi baada ya serikali kutoa Sh2.6 bilioni mwaka 2023 kwaajili ya kukarabati.

“Hadi sasa tumepokea maombi 156 na tayari wanafunzi 43 wamethibitisha, mchakato bado unaendelea na baada ya hapo ndipo tutajua wanafunzi wangapi wamedahiliwa ingawa tuna uwezo wa wanafunzi 150,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amesema wakazi wa wilaya hiyo wanakisbiri chuo hicho kwa hamu kwani mbali na elimu chuo hicho pia kitakuwa moja ya kichocheo cha ukuaji wa uchumi katika wilaya hiyo.

Related Posts