Mwalimu matatani madai ya kuua mwanafunzi

 

JESHI la Polisi mkoani Kagera, linamshikilia Adrian Tinchwa (36), ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Igurwa na Mkazi wa Kanoni, wilayani Karagwe, mkoani humo kwa tuhuma za kumshambulia na kumsababishia kifo mwanafunzi Phares Buberwa, akimtuhumu kumwibia simu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kagera … (endelea).

Mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Igurwa, anadaiwa kukutwa akitoka ndani kwa mwalimu huyo (mtuhumiwa), ambaye alikuta kufuli la nyumba limevunjwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, amesema wanamshikilia mwalimu huyo kwa tuhuma za kumshambulia mwanafunzi huyo kwa kumpiga ngumi kwenye paji la uso, kisha kutumia nondo kumpiga nayo miguuni na mikononi akimtuhumu kumwibia simu yake.

Kamanda Chatanda alisema mtuhumiwa alitenda kosa hilo tarehe 18 Septemba 2024, saa nane mchana katika Kijiji cha Kanoni, wilayani Karagwe.

“Awali tarehe hiyo hiyo majira ya saa tatu asubuhi, inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo alifika nyumbani kwake na kukuta kufuli la mlango wa nyumba yake limevunjwa na alipotaka kuingia ndani alikutana na Phares Buberwa, mlangoni akijaribu kukimbia,” alisema Chatanda.

Alisema baada ya hapo alimkamata na kuanza kumshambulia hadi kumsababishia majeraha makubwa mwilini; na baadaye kumpeleka hadi nyumbani kwa wazazi wake na kumkabidhi kisha wazazi wake walimpeleka katika Kituo cha Afya cha Rwambaizi kwa ajili ya kupata matibabu.

“Phares alifariki dunia kituoni hapo wakati akipatiwa matibabu na chanzo cha tukio hili ni mtuhumiwa kujichukulia sheria mkononi na kutoa adhabu iliyopitiliza kwa marehemu huyo,” alisema Kamanda Chatanda.

Alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani taratibu zote zitakapokamilika.

About The Author

Related Posts