Naibu Katibu Mkuu Aagiza Maafisa Utalii Kuuza Vivutio Bila Mipaka

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayesimamia utalii, Nkoba Mabula, amewataka maafisa utalii nchini kuuza vivutio vya utalii bila kujali mipaka ya maeneo yao. 

Mabula alitoa maagizo hayo Septemba 25, 2024, katika kikao na wahifadhi wa TFS Kanda ya Kaskazini, wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

Akitoa mfano wa uwepo wa kivutio cha Kaburi la Shaban Robert na ukaribu wake na Magofu ya Tongoni, alisema, “Ni muhimu maafisa wa utalii waongeze hadithi zinazohusisha vivutio vyote, sio maeneo yao pekee! Hii itamsaidia mtalii kutumia zaidi muda na rasilimali fedha zake.”

Aliongeza kuwa nchi ina utajili mkubwa wa vivutio na aliwataka wahifadhi kwanza kujua sasa wao si wahifadhi pekee ila ni maafisa utalii na hivyo kuandaa hadithi nzuri za kutangaza vivutio hivyo.

Mabula pia alisisitiza umuhimu wa kutoa maelezo sahihi na ya kina kuhusu kila ndege, mdudu, wanyama na mimea ili kuwasaidia watalii kupata taarifa za kina. 

“Kuhakikisha mnapotoa maelezo, mtaje kwa mfano, kama ni chura, ni ndege gani na kipindi gani cha mwaka wanapatikana, na wapi. Ikiwa ni mti mrefu kama Mvule uliopo Msitu wa Rau Moshi, usiishie kwenye urefu na upana tu; unganisha na hadithi ya Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu barani Afrika. Kwa kufanya hivi, tutasaidiana kuimarisha mauzo ya vivutio vyetu,” alisisitiza.

Aidha, aliwapongeza wahifadhi wa TFS kwa kuchangamkia fursa za utalii ikolojia na uhifadhi na kuleta manufaa kwa jamii. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Utalii wa Wizara ya Maliasili na Utalii, …..akizungumza na wahifadhi wa Ziwa Duluti, aliongeza kuwa utalii ni kuhusu hadithi na matangazo, na hivyo ni lazima kuboresha miundombinu na kuandaa hadithi zinazovutia.

Kamanda wa Uhifadhi TFS,  Kanda ya Kaskazini, James Nshare, alieleza kuwa ziara hiyo itasaidia kuboresha ufanisi wa juhudi za kutangaza utalii nchini, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja katika kutekeleza majukumu hayo. 

Aliongeza kwamba hatua hii itachangia katika kuondoa mipaka na kuleta manufaa kwa masilahi mapana ya nchi, huku akitaja umuhimu wa kuhusisha jamii za eneo hilo ili kukuza utalii ikolojia na maendeleo ya kiuchumi.

Related Posts