Russia inavyochomoza katika uwekezaji Tanzania

Tanzania imeendelea kuwa kituo cha uwekezaji Afrika, huku wadau wakieleza namna wananchi wanavyoweza kunufaika na uwekezaji huu.

Pia, wadau wametaka hatua zinazofuata baada ya usajili kutochukua muda mrefu ili wananchi waone matunda ya kile kinachoripotiwa kuongezeka kupitia uzalishaji wa ajira ili kukwamua vijana wengi waliopo mtaani.

Hayo yamebainishwa wakati ambao Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimerekodi ongezeko la uwekezaji katika miradi na mitaji katika robo ya mwaka iliyoishia Juni, 2024 ikilinganishwa na kipindi kilichotangulia.

Uwekezaji katika miradi kwa robo ya mwaka iliyoishia Juni, 2024 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kilichotangulia, umeongezeka kwa asilimia 53, huku mtaji ukikua kwa zaidi ya asilimia 60.72.

Katika upande wa ajira zilizotengenezwa, uwekezaji uliofanywa katika robo iliyoishia Juni, 2024 umeongeza fursa za ajira mara tano zaidi ya zile zilizozalishwa kipindi cha mwaka uliotangulia.

Kwa mujibu wa TIC, kati ya Aprili hadi Juni, 2024, Sh4.42 trilioni ziliwekezwa katika miradi 198, ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2.75 trilioni kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.

Pia, ongezeko hilo ni takribani asilimia 10 ikilinganishwa na mitaji iliyowekezwa katika robo ya mwaka ya Januari hadi Machi, 2024 iliyokuwa Sh4.02 trilioni.

Hii inafanya zaidi ya Sh8.44 trilioni kuwekezwa kati ya Januari hadi Juni, 2024 katika miradi tofauti ya maendeleo.

Kwa mujibu wa TIC, Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kuwa na miradi 75, ikifuatiwa na Pwani iliyokuwa na miradi 30, Arusha miradi 19 na Dodoma miradi 13.

“Kampeni ya kitaifa ya kukuza uwekezaji na maonyesho yanayofanywa katika nchi zinazolengwa yamekuwa na njia muhimu katika kuvutia mitaji ya nje na ndani,” anasema Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri.

Kwa mujibu wa Teri, ukuaji huu pia umechangiwa na uimarishaji wa huduma uliofanyika katika kituo cha huduma kwa pamoja kilicho chini ya TIC kwa kuongeza wawakilishi wapya wawili kutoka Wizara ya Kilimo na Tume ya Madini.

“Ongezeko hili linalenga kuhakikisha kuwa wawekezaji wanapata usaidizi kamilifu pindi wanapochagua kuwekeza nchini,” anasema.

Pia katika hilo, Teri anaweka bayana mkakati wao ambao ni kuweka kipaumbele katika kushughulikia changamoto za wawekezaji wa ndani, kupanua fursa za uwekezaji na kuhimiza wajasiriamali wa ndani kutumia motisha zinazopatikana.

Wakati Teri akiyasema hayo, Russia ndiyo nchi inayoongoza kwa kuleta mtaji mkubwa katika robo iliyoishia Juni, 2024 ikiweka zaidi ya Sh886.48 bilioni, ikifuatiwa na China iliyoonyesha nia ya kuwekeza Sh473.28 bilioni.

Ulaya ilishika namba tatu kwa kuonyesha nia ya kuwekeza Sh438.05 bilioni, Bermuda Sh137.34 bilioni na nchi za Jumuiya za Kiarabu zikiwekeza Sh98.8 bilioni.

Fedha hizi na nyingine zilizowekezwa kutoka nchi tofauti ziliwekezwa katika maeneo 12 ambayo ni kilimo, majengo ya biashara, miundombinu ya kiuchumi, nishati, taasisi za kifedha, rasilimali watu, viwanda, mafuta na madini, huduma, mawasiliano, utalii na usafirishaji.

Katika miradi hiyo, viwanda ndivyo viliongoza kwa kupata miradi 92, ikifuatiwa na sekta ya ujenzi wa majengo ya biashara yaliyokuwa 28, usafirishaji 22, utalii 21, kilimo miradi 11, huduma na nishati zikiwa na miradi mitano kila moja.

Hata hivyo, wakati kilimo kikiwa na miradi michache, ndicho kinachoongoza kwa kutengeneza fursa nyingi za ajira zinazotarajiwa kutolewa, 76,023 huku sekta ya viwanda inayoongoza kwa kuwa na miradi mingi ikitarajiwa kuzalisha ajira 12,667.

Hatua hii inapigwa ikiwa lengo la Serikali lililowekwa wazi Januari 11, 2024 na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ni kuhakikisha mwaka 2025 TIC iwe na uwezo wa kusajili miradi ya uwekezaji yenye thamani ya Sh37.72 trilioni.

Ongezeko la thamani ya miradi hiyo itakuwa ni mara mbili zaidi ya kiwango cha uwekezaji kilichofanywa mwaka 2023, ambayo ilikuwa Sh14.06 trilioni.

Alipokuwa akizungumza na wanahabari, Profesa Mkumbo alisema tayari wamefanya hesabu na kuangalia ukuaji wa uwekezaji unaofanyika kila mwaka na kuona lengo lililowekwa linawezekana.

Katika mwaka 2023, TIC ilifanikiwa kusajili miradi 504 ambayo ilikuwa na thamani ya Sh14.06 trilioni na itakapoanza kazi inatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 23,000.

Thamani ya miradi hiyo ilikuwa ni ongezeko kutoka zaidi ya dola za Marekani bilioni 3 (zaidi ya Sh7.53 trilioni) iliyosajiliwa mwaka uliotangulia. “Hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya, tumewapa lengo hili Kituo cha Uwekezaji (TIC) wapambane, walibisha kidogo ila tumewaambia hili ndiyo lengo. Tutakapokamilisha Dira ya Maendeleo 2050 tutaona tunataka kwenda wapi, bodi imekubali na watahakikisha wanatekeleza,” alisema Profesa Mkumbo.

Ili kufanikisha hilo, TIC iliutangaza mwaka 2024 kuwa maalumu kwa ajili ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, jambo ambalo lilifanya kuanza kwa kampeni mbalimbali, hasa katika mikoa ambayo fursa hazijaguswa ipasavyo.

Akizungumzia ukuaji huu unaoendelea kushuhudiwa, mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora anasema uwekezaji ndiyo njia ya kukuza uchumi.

Anasema kunapofanyika uwekezaji, Serikali inakuwa na uwezo wa kupata matumizi, kwani pindi mitaji inayowekwa inapozaa huweza kuongeza mapato na kodi zinazokusanywa na Serikali.

“Kuwekeza ndiyo kunafanya nchi ipate bidhaa za kuuza nje ya nchi na watu wake kutumia, hili lifanyike zaidi na inawezekana kwa sababu wapo mawaziri wenye mitazamo chanya katika vitu wanavyofanya,” anasema Profesa Kamuzora.

Hata hivyo, ili uwekezaji huu uwanufaishe watu wa chini wanapozunguka katika maeneo ambayo miradi inatekelezwa, Profesa Kamuzora anasema ni vyema wananchi wafundishwe kila mtu kufanya kazi kwa bidii katika eneo alilopo.

“Tuanzie kila mtu afanye kazi, kila mtu anavyoweza katika eneo lake, kama wewe ni muuza nyanya basi hakikisha unakwenda sokoni kuuza nyanya, walimu wafundishe vizuri tupate wataalamu, wakulima walime wapate bei nzuri na kuuza malighafi, hivi ndivyo tunaweza kushirikisha watu kunufaika na matunda ya uwekezaji,” anasema.

Anasema hilo litawezekana pia kwa kuangalia namna ya kuwawezesha Watanzania katika nafasi walizopo kupitia kuwapa mitaji kwenye vikundi walivyopo kama ilivyokuwa ikifanyika awali katika utoaji wa mikopo ya asilimia 10. Mikopo hiyo ilikuwa ikihakikisha kuwa hakuna anayeachwa nyuma katika makundi yote, ikiwemo vijana, wanawake na wenye ulemavu.

Mchambuzi wa masuala ya biashara na uchumi, Oscar Mkude anasema ili uwekezaji huu umguse mtu mmojammoja, ni vyema kuhakikisha miradi inayosajiliwa inatekelezwa kwa asilimia 100.

Hiyo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa changamoto iliyopo ni miradi mingi imekuwa ikitumia muda mrefu tangu kusajiliwa hadi kuanza kutekelezwa.

“Hiyo inafanya watu mitaani wasiamini wanapoambiwa miradi imesajiliwa ya gharama hizi waone ni uongo, kuwe na mabadiliko hasa katika upatikanaji wa ajira. Zamani mtu ilikuwa akimaliza chuo anaweza kutumia miezi sita kutafuta kazi, lakini sasa hata miaka 9 yuko mtaani, sasa miradi hii utuonyeshe matokeo,” anasema Mkude.

Pia, anashauri kuwa ni vema miradi itakayosajiliwa iwe ni ile itakayochagiza uchumi wa nchi, iwe inayogusa sekta ya uzalishaji moja kwa moja, ikiwemo kuongeza thamani ya bidhaa za ndani.

“Hii itachangia pia katika uuzaji wa bidhaa zetu nje ya nchi. Katika hili ni vyema kuangalia ulinganifu wa miradi, isijekuwa mingi imeshikwa na watu wa nje, si jambo zuri, bali tuhakikishe tuna wazawa pia.

Mtaalamu wa biashara, Dk Donath Olomi anasema hali hii ni fursa kwa Watanzania, kwani watanufaika na fursa za ajira zitakapotolewa, nchi itaweza kupata kodi na watu kuweza kujifunza kutoka kwa wawekezaji wa nje.

“Hii inamaanisha mazingira ya biashara yanaendelea kuwa mazuri, lakini ili uwekezaji huu uwe na faida, ni lazima kuhakikisha sekta zinazogusa watu wengi katika kilimo miradi mingi inavutiwa huko,” anasema Dk Olomi.

Pia, ili Watanzania wanufaike zaidi anasema ni vyema kuwekeza katika kuwajengea ujuzi ili waweze kutumika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali pindi inapoanza utekelezaji wake nchini ili kupunguza utegemezi wa wataalamu kutoka nje.

Related Posts