Mbunge wa Jimbo la Kavuu na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda ameshiriki kikao cha halmashauri ya CCM kata ya Mamba wilaya ya Mlele mkoa wa Katavi.
Katika kikao chake Mhe. Pinda aliwaeleza wajumbe wa mkutano huo, namna serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza miradi mbalimbali ndani ya jimbo la Kavuu.
Ametolea mfano wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara ambapo amesema barabara ya urefu wa Km 1 kutoka Mamba kuelekea Kasansa hadi Majimoto inakwenda kutengenezwa katika kiwango cha lami.
Mhe. Pinda ameweka wazi kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutaongeza kasi ya ukuaji maeneo mbalimbali sambamba ufikiaji eneo moja kwenda lingine ikiwa pamoja na urahisi wa kusafirisha mazao na kurahisisha utoaji wa huduma za jamii katika jimbo hilo.
“Lakini pale majimoto upande wa viwandani kwa sababu ndio uchumi wetu uko pale tupitishe barabara ikaguse upande wa pili wale wafanyabishara wetu wawe na amani na hata nyie mnapotoa mazao kule sehemu ya lunguya ukifika pale pawe na ulaini wa kupitisha mazao yetu” amesema mhe. Pinda.
Naye, Katibu wa Itikadi Uenezi na Mafunzo wa Chama hicho ndugu Renatus Kamaneja amewahimiza Madiwani wote ni jukumu nlao la kwanza kuendelea kuisemea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao.
Mhe. Geophrey Pinda yupo katika muendelezo wa ziara yake iliyoanza tarehe 25 Sept 2024 na kukamilika Oktoba 4, 2024 ambapo atatembelea kata zote ndani ya jimbo la Kavuu.