shule za kata,Mashirika ya kutetea wasichana yamesaidia kupunguza ndoa za utotoni Tarime

 

 

Na Humphrey Shao, Michuzi Tv

KAIMU Mkurugenzi  Wilaya ya Tarime,Peragia Barozi amesema uanzishwaji wa shule za kata na uwepo wa mashirika ya kutetea haki za wasichana katika Wilaya ya Tarime imeweza kusaidia kupunguza kasi za ndoa za utotoni kwa miaka ya sasa kuliko miaka ya nyuma.

Amesema miaka ya nyuma watoto hao wakike walikuwa wakiolewa kuanzia darasa la nne,kwa sasa watoto wanapomaliza shule wengi wanaunganisha kusoma sekondari kutokana na uwepo wa shule hizo za kata na kukimbia kuozeshwa kwa umri mdogo.

Akizungumza hayo jana Mkoani Mara wilayani humo,wakati wa Msafara(Caravan)wa Mtandao wa Kutokomeza ndoa za Utotoni kutoka Mashirika 87 ambayo yamewakilishwa na wanachama wa Mtandao huo kutoka Shirika la Msichana Initiative,Binti Makini,Medea,Plan Internationa pamoja na My Legacy.

Amesema licha ya uwepo wa shule za kata kusaidia wasichana kuendelea na shule pamoja na mashirika yanayotetea haki za wasichana kwa hali halisi ndoa za utotoni bado zipo katika wilaya hiyo lakini sio kama miaka ya nyuma.

Barozi amesema mashirika hayo yameweza kusaidia kwenda vijijini hadi katika kata na kuwafikia watu mbalimbali katika kutoa elimu ya athari za ndoa za utotoni na ukeketaji kwa wasichana.

“Mbali na hivyo uanzishwaji wa kituo vya masanga ambavyo vipo kwaajili ya kupokea watoto wanaokimbia majumbani mwao baada ya kupatwa na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ukeketaji pamoja na mimba za utotoni vimekuwa vikisaidia kuwalea watoto hao pindi wanapokumbana na changamoto hizo,”amesema.

Kwa upande wake Mratibu wa Mtandao huo,Lilian Kimati alisema lengo la Caravan hiyo ni kupita katika mikoa minne ambayo ina asilimia kubwa ya ndoa za utotoni ikiwemo mkoa wa  Mara kwa wilaya ya Tarime,Shinyanga,Tabora pamoja na Dodoma.

Amesema kwa msafara huo wameanza kuwafikia watu mbalimbali ikiwemo halmashauri na kituo cha kupokea watoto wanaokimbia ukeketaji na ndoa za utotoni cha Masanga wilayani humo.

”Lengo letu ni kutoa hamasa na elimu kuhusiana na masuala ya ndoa za utotoni jinsi gani wazazi wanatakiwa kusimama katika nafasi zao kuhakikisha  mabinti hawaozeshwi mapema bali waende shuleni kusoma na kuja kufanya mambo makubwa kwa jamii baadae,”Amesema.

Aidha Amina Mtengeti Mratibu wa Programu kutoka Shirika la MyLegacy amesema wamechangua mikoa hiyo minne kwa sababu kutokana na takwimu za demographia ya mwaka 2015/2016 ilionyesha kuwa asilimia 36 ya wasichana walio na umri kati ya miaka 20 hadi 24 walioolewa kabla hawajafikia miaka 18.

”Wasichana hao wengi walionekana kutoka katika mikoa hii minne ambapo Shinyanga ilikuwa na asilimia 59,Tabora asilimia 58,Mara ilikuwa asilimia 55 na Dodoma ikiwa na asilimia 51 hivyo Caravan imelenga kuangalia wasichana wenyewe wanaweza kutumia nafasi zao kuongea na kupaza sauti kukabiliana na vitendo vya kikatili vinavyoathiri utu wao ikiwemo ndoa za utotoni,”amesema.

Mmoja wa Mabinti aliyekumbwa na ndoa za Utotoni,Leila Lupatu Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wasichana kutoka Shirika la Msichana Initiative amesema anatamani ifike mahali wasichana wapaze sauti zao ili kuweza kusikika haraka kwa serikali na kuchukua jitihada mbalimbali kutokomeza hizi ndoa za utotoni ili waweze kufika katika nafasi kubwa.

”Tunaomba Serikali kushirikiana na wasichana katika kutokomeza ndoa za utotoni kwani zimekuwa zinaathari kubwa kwa mabinti katika kutokomeza ndoto zetu,”amesema.

Mwishoooooo

Related Posts