KICHAPO cha mabao 3-1, ilichokipata Al Ahli Tripoli dhidi ya Simba katika mchezo wa pili kusaka tiketi ya kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimemponza kocha Mtunisia, Chokri Khatoui aliyefutwa kazi, huku Milutin Sredojevic ‘Micho’ akitajwa kuchukua nafasi hiyo muda wowote kuanzia sasa.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa watu wa karibu na timu hiyo zinasema, Chokri alifanya kikao na viongozi wa Tripoli ili kutoa ripoti ya kile kilichosababisha kikosi hicho kutolewa na Simba katika mashindano hayo ya Afrika na maamuzi ni kwamba jamaa ameteshwa kibarua.
“Malengo ya viongozi wao yalikuwa ni kufika kwanza hatua ya makundi lakini kitendo cha kukosa ushindi mechi ya kwanza tu pale Libya, kilianza kuwapa wasiwazi kwa sababu hawakuwa na matumaini makubwa wakichezea ugenini, kilisema chanzo hicho.
Mwanaspoti linatambua kwamba, Chokri aliwekewa mashaka ndio maana viongozi wa klabu hiyo walimleta aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Libya Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’ ambaye ndiye anayetajwa kuchukua nafasi ya Mtunisia huyo.
Hata hivyo, Mwanaspoti lilimtafuta ‘Micho’ kuhusu mazungumzo yake na timu hiyo ambapo aliweka wazi hana uhusiano wowote huku akieleza sababu ya yeye kuja jijini Dar es Salaam katika mchezo wa kikosi hicho lilikuwa ni jambo la kawaida kwake.
Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Kibu Denis, Leonel Ateba na Edwin Balua huku lile la kufutia machozi kwa upande wa Al Ahli Tripoli ya Kocha Mkuu, Chokri likifungwa na mshambuliaji raia wa Angola, Cristovao Paciencia Mabululu.
Chokri alijiunga na kikosi hicho Julai 16, mwaka huu akitokea Abu Salem SC ya Libya pia ambapo Tripoli msimu uliopita ilikuwa kundi ‘A’ lenye timu 11, ikimaliza nafasi ya kwanza na pointi 48, ikishinda michezo 15, sare mitatu na kupoteza miwili.
Kwenye michezo hiyo safu ya ushambuliaji ya Tripoli ilifunga mabao 29 huku eneo la kujilinda likiruhusu saba huku kundi ‘B’ likiongozwa na Al-Nasr Benghazi iliyoshinda michezo 11 kati ya 18, sare minne na kupoteza mitatu ikiwa na pointi 37.
Kwa mfumo wa Ligi ya Libya, timu tatu za juu kutoka kila kundi kwa maana ya ‘A’ na ‘B’ zinakutana kucheza kwa kila mmoja wao ambazo zitatoa bingwa wa nchi hiyo na klabu zitakazoshiriki kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.
Msimu uliopita, bingwa ni Al-Nasr katika mfumo wa timu sita kufuatia kushinda michezo yote mitano ya mtoano ‘Play-Off’ na pointi 15 huku Al Ahli ikishika ya tatu baada ya kushinda miwili, sare mmoja na kupoteza miwili ikiwa na pointi saba.
Al Ahli yenye makao yake mjini Tripoli, ni klabu ya pili ya Libya yenye mafanikio makubwa katika historia baada ya Al-Ittihad ambapo imeshinda jumla ya mataji 13 ya Ligi Kuu ya Libya, makombe saba ya Libya na mawili ya Super Cup za Libya.