Unguja. Wananchi wanaofanya shughuli za ujasiriamali na kusafirisha watalii katika Kisiwa cha Kwale, wameingiwa hofu ya kupoteza shughuli zao, baada ya kuwapo mpango wa kisiwa hicho kukodishwa.
Wameiomba Serikali kuangalia upya mpango wa kukodisha kisiwa hicho, wakisema kinategemewa na wananchi wengi, hususani wenye hali duni kuendesha maisha yao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa), Saleh Saad akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Septemba 26, 2024, amesema lengo la kukodisha visiwa ni kuleta tija katika maendeleo.
Amesema mpaka sasa kuna visiwa 16 vimekodishwa vyenye thamani Dola milioni 385 za Marekani.
Saleh amesema Kisiwa cha Kwale ni miongoni mwa vilivyokodishwa katika utaratibu wa anayekuja na mtaji unaokidhi mahitaji ya Serikali na wazo linaloridhisha ndiye hupewa.
“Kisiwa cha Kwale kimepata mwekezaji na anatarajia kuwekeza kiasi kisichopungua Dola milioni 68, takribani mara mbili ya Kisiwa cha Bawe ambacho kimewekezwa Dola milioni 37.
“Kitu ambacho niwaombe wananchi wenzangu, uamuzi wa Serikali ni kuhakikisha kuna maendeleo endelevu yenye tija kwa Serikali na wananchi, hivyo katika utaratibu wa ukodishwaji na ujenzi katika visiwa hivi, kwanza ni kuhakikisha mazingira yanatunzwa,” amesema.
Amesema matumizi ya kisiwa hayazidi asilimia 10 ya eneo la kisiwa, zaidi shughuli za kijamii ambazo zinaendelea zimezingatiwa kwa utaratibu maalumu.
“Kwa hiyo niwatoe hofu wananchi, uamuzi wa kumpatia mwekezaji kukiendeleza na kuweka mtaji mkubwa umezingatia uwapo wa wananchi na matumizi ya wananchi kwenye kisiwa husika,” amesema.
Miongoni mwa vivutio katika kisiwa hicho ni mchanga uliokusanyika katikakati ya bahari na mbuyu ulioanguka ukaota tena, ila ukatengeneza chemichemi na hutuamisha maji ambayo hayana chumvi na matumbawe maalumu kwa ajili ya makazi ya samaki.
Kutokana na vivutio, hivyo wageni wanapofika Zanzibar hupenda kutembelea kisiwa hicho, kwa siku inakadiriwa hutembelewa na wageni zaidi ya 500 na kila mmoja hulipa Dola tatu za Marekani (Sh8,200).
Kuna boti zaidi ya 60 zinazosafirisha wageni zilizosajiliwa na Serikali kwa Sh100,000 kwa mwaka, huku kila boti ikiajiri watu wanne.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, baadhi ya wajasirimali na waendesha boti katika kisiwa hicho wamemuomba Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kuwaachia kisiwa hicho kwa kuwa wengi wamejiajiri hapo.
Mjasiriamali kisiwani humo, mkazi wa Shehia ya Kikungwi, Bahati Issa Suleiman amesema wana hofu ya kuondolewa akifika mwekezaji.
“Haya maeneo ya visiwa yameajiri watu wengi ambao wapo katika kipato cha hali ya chini hususani wanawake na vijana, watu wa kila rika wapo ndani ya visiwa hivi vinatupatia riziki mkono uende kinywani, leo tukisikia visiwa vinawekezwa tunafikiria tutakwenda wapi na hiki ni kilio cha wengi,” amesema.
Bahati ambaye ni Katibu wa Kamati ya vijiji sita vya Ng’ambwa, Uzi, Kikungwi, Unguja, Ukuu na Bungi, amesema kazi ya kamati hiyo ni kulinda na kuhifadhi mazingira ndani ya eneo la ghuba ya Minai.
Amesema, “tunasomesha watoto kupitia kisiwa hiki, hata baba aondoke wiki nzima nyumbani hatasikia anaambiwa hakuna chumvi nyumbani, lakini leo tukiondoshwa itakuwaje?” amehoji.
Bahati, ambaye ni nahodha mwanamke wa boti amesema: “Naamini Rais atatusikia kilio chetu kwa sababu kisiwa hiki ndiyo kinachotuweka hata katika usalama wa ndoa na kupunguza udhalilishaji.
“Unadhani kijana aliyetoka Fumba, Bweleo, Unguja Ukuu kafika hapa saa 4.00 asubuhi anaondoka saa 10.00 jioni unafikiri atakuwa na muda wa kwenda kufanya vitendo vya udhalilishaji au kuiba? Hawezi, kwa hiyo kinapunguza matatizo ya vijana wengi,” amesema.
Mussa Muhamed Mkadamu, mzaliwa wa Fumba amesema maisha yao yote yapo kwenye kisiwa hicho, wamejiajiri kwenye utalii baada ya sekta ya uvuvi kuwa na changamoto nyingi.
“Lakini masikitiko yetu ni kuona kile kisiwa tayari kinatafutiwa mwekezaji kuwekezwa, lakini mwanzoni walisema visiwa visivyotumika ndiyo vitakavyowekezwa,” amesema.
Amesema zamani walikuwa wakitumia kwa shughuli za uvuvi, lakini baada ya kuona kuna fursa kwenye utalii wakaamua kujiwekeza huko.
“Hapa tumejiajiri tuna vyombo (boti) zaidi ya 60 na kila chombo kimoja kinaajiri vijana wanne, kwa hiyo kuna wengine wanapika na kuuza bidhaa zao sasa iwapo akija mwekezaji hizi ajira zote zitaondoka,” amesema.
“Hatupingi maendeleo, ila katika maendeleo endelevu na sisi tunufaike, hofu yetu ni kuwa akipewa mwekezaji kitakuwa chake kwa hiyo atakuwa na uhuru kwamba wewe njoo na wewe usije, upo uwezekano wengi hapa tukaondoshwa,” amesema.
Amesema ni jukumu la Serikali kuhakikisha matakwa ya wananchi na mahitaji yao yanazingatiwa katika kufanya uamuzi.