‘Waliotumwa na afande’ wamaliza kujitetea, hawakuwa na vielelezo

Dodoma. Upande wa utetezi kwenye kesi ya jinai inayowakabili washtakiwa wanne wanaokabiliwa na mashtaka ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam umekamilisha kutoa ushahidi wao.

Leo Alhamisi, Septemba 26, 2024 mashahidi wawili wametoa utetezi wao hivyo kufanya idadi ya mashahidi wa utetezi kufikia wanne ambapo jana Jumatano mashahidi wengine wawili walitoa utetezi wao.

Wakati upande wa utetezi wakiwa na mashahidi wanne bila vielelezo kwenye kesi hiyo ya washtakiwa hao ‘waliotumwa na afande’, upande wa Jamhuri ulileta mashahidi 18 na vielelezo 12 kuhusu kesi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama, wakili anayewawakilisha washtakiwa hao, Meshack Ngamando amesema upande wa utetezi wameshakamilisha kutoa ushahidi ambapo kulikuwa na mashahidi wanne ambao wote ni washtakiwa kwenye kesi hiyo.

Waliotoa ushahidi jana ni Askari wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) MT 140105 Clinton Damas, maarufu Nyundo na Amin Lema (Kindamba). Mashahidi wa leo walikuwa ni Nickson Jackson (Machuche) na Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi.

Ngamando amesema upande wa utetezi awali ulisema utakuwa na mashahidi 10 na vielelezo sita lakini waliotoa ushahidi ni wanne tu bila vielelezo vyovyote.

Amesema vielelezo kwenye utetezi viliegemea kwa mshtakiwa ambaye ni askari Magereza, Praygod Mushi lakini havikufika kwa wakati mahakamani kwa sababu vipo upande wa Serikali hivyo wamekamilisha utetezi wao bila kutoa vielelezo kwa sababu hawakuvipata kwa wakati.

Amesema pande zote mbili zimeshatoa ushahidi wao na kesho Ijumaa Septemba 27, 2024 kitakachofanyika ni kutoa mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo mzima kuhusu kesi hiyo tangu walipokamatwa mpaka kufunga ushahidi kama ulifuata taratibu za kisheria.

“Tumeiomba mahakama kesho tuwasilishe mawasilisho ya kisheria kuhusu mwenendo mzima wa kesi hii kuanzia ukamataji wa washtakiwa, utambuzi, mashahidi waliotoa ushahidi dhidi yao, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kama vilizingatia matakwa ya kisheria,” amesema Ngamando.

Washtakiwa hao wa kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2024 ambapo walisomewa mashtaka ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo ambaye mahakamani anatambulika kwa jila la XY.

Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule. Baada ya kusomewa mashataka yao waliyakana.

Hata hivyo, ofisi ya Taifa ya mashtaka walizuia dhamana ya washtakiwa hao kutokana na unyeti wa kesi hiyo na waliiomba mahakama kusikiliza kesi hiyo mfululizo ambapo ilianza kusikilizwa Agosti 20, 2024.

Related Posts