USHINDI wa bao 1-0, ilioupata Yanga juzi dhidi ya KenGold katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, umeifanya timu hiyo kuendeleza rekodi bora ya kutopoteza mashindano mbalimbali tangu mara ya mwisho Aprili 5, mwaka huu.
Mchezo wa mwisho kwa Yanga kupoteza wa mashindano ulikuwa ni wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini ilipochapwa kwa penalti 3-2, baada ya suluhu michezo yote miwili Aprili 5, mwaka huu.
Baada ya kuondolewa katika Ligi ya Mabinwga Afrika, Yanga chini ya Kocha Mkuu Muargentina, Miguel Gamondi imecheza jumla ya michezo 22 mfululizo ya mashindano mbalimbali bila kupoteza ambapo imeshinda 21 kati ya hiyo na kutoka sare mmoja tu.
Katika michezo hiyo 22 ni mmoja tu ambao ulikuwa wa mtoano kwa maana wa fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ambao Yanga ilishinda kwa penalti 6-5, dhidi ya Azam FC, mchezo uliopigwa New Amaan Complex Zanzibar Juni 2, mwaka huu.
Kuonyesha ubora wa kikosi hicho cha Gamondi, katika michezo hiyo 22 iliyocheza bila ya kupoteza, imefunga jumla ya mabao 54 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara nne tu, jambo linaloonyesha wazi inajua kufunga na wakati huohuo ikizuia pia.
Pia, ushindi wa Yanga dhidi ya KenGold, unaifanya timu hiyo kufikisha jumla ya michezo saba mfululizo ya Ligi Kuu Bara iliyocheza ugenini kuanzia msimu uliopita hadi sasa bila kupoteza, tangu ilipofungwa 2-1 na Azam FC Machi 17, mwaka huu.
Katika michezo hiyo saba kiujumla ambayo Yanga imecheza ugenini, imeshinda sita na kutoka sare mmoja tu ambao ulikuwa wa suluhu (0-0) dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania, mechi iliyopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Aprili 24, mwaka huu.
Kwenye michezo hiyo saba, Yanga imefunga jumla ya mabao 14 ikiwa na wastani wa kufunga mabao mawili katika kila mchezo huku ikiruhusu bao moja tu lililopatikana mechi ya Mtibwa Sugar iliyoisha kwa timu hiyo kushinda 3-1, Mei 13, mwaka huu.
Akizungumza juzi baada ya mchezo na KenGold, Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi alisema, katika michezo yao miwili ya Ligi waliyocheza hadi sasa walipata nafasi nyingi ila walishindwa kuzitumia, ingawa jambo kubwa ni kupata pointi tatu.
“Mchezo na Kagera Sugar tulishinda 2-0, ila tulipata nafasi nyingi ambazo tungeweza kuzitumia, kama ilivyokuwa pia kwa KenGold japo hatujapata maandalizi ya kutosha, muhimu ni kupata matokeo mazuri hivyo nawapongeza wachezaji kwa hilo.”