Zitto ashauri upinzani kuungana kwenye chaguzi kuing’oa CCM

Dar es Salaam. Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema mbinu ya kukishinda chama tawala Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji, vitongoji Novemba 27, 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025 ni vyama vya upinzani kuungana.

Kutokana na hilo, mbunge huyo wa zamani wa Kigoma Kaskazini, amevishauri vyama vya upinzani kukaa meza na kutengeneza mchoro utakaohakikisha wanaibuka kidedea kama ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, vyama Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD viliungana kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ambapo kwa mara kwanza uliacha historia ya nchi, kwa Bunge kupata wabunge wengi wa vyama vya upinzani.

Kwenye uchaguzi huo, Ukawa kupitia Chadema ilimsimamisha Hayati Edward Lowassa aliyepata kura milioni 6.07 sawa asilimia 39.97 ambazo hazikutosha awe Rais mbele ya mgombea wa CCM  Hayati John Magufuli aliyepata kura milioni 8.8 sawa asilimia 58.47.

Ni uchaguzi huo uliosababisha Ukawa kuongoza halmashauri zaidi ya 20 yakiwemo majiji ya Dar es Salaam, Arusha na Tanga.

Zitto ameeleza hayo jana Jumatano Septemba 25, 2024 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mbozi mkoani Songwe, katika mwendelezo wa ziara ya chama hicho,  yenye lengo maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji na kupata wanachama wapya.

“Mkoa wenu wa Songwe mwaka 2015 uligawana nusu kwa nusu kati ya upinzani na CCM, sasa hivi vyama vya upinzani hapa Songwe tukaeni pamoja, tuchore mchoro tugawane majimbo ili tuinyime CCM kura katika mkoa huu.

“Haya mambo ya kila mtu kujiingilia kivyake katika chaguzi au kujiona bora kuliko mwingine, kujiona mkubwa kuliko mwingine, hayatusaidii lolote badala yake CCM inafaidika,” amesema Zitto.

Zitto aliyewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini, amehitimisha ziara yake mkoani humo, amewaagiza viongozi wa ACT-Wazalendo mkoa wa Songwe kukaa na vyama vya upinzani kuangalia vijiji, mitaa na vitongoji ambavyo Chadema ina nguvu watoe ushirikiano katika uchaguzi utakaofanyika mwisho mwa mwaka huu.

Mwanasiasa huyo, amesema sehemu ambayo ACT-Wazalendo ina nguvu basi vyama vya upinzani viwaunge mkono ili kuwaondoa CCM katika madaraka kuanzia ngazi ya chini.

“Hii ndiyo kazi tunayoweza kuifanya, sisi hatuwezi kuwa watu wa kurudia mambo yaleyale, kila uchaguzi tunafanya vilevile wa vyama kuingia kivyake vyake, tukidhulumiwa ndiyo tunaitisha mkutano na wanahabari tunalalamika, uchaguzi ukiitishwa tunaenda kupambana walewale.

“Tuacheni ujinga, tukaeni chini tuisafishe CCM na inawezekana, ila bado hatujifunzi badala yake tunaongoza kwa kupigana vita wenyewe kwa wenyewe mambo ya kijinga kabisa,” amesema Zitto.

Wakati Zitto akinguruma mkoani Songwe, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu akiwa wilayani Kongwa, mkoani Dodoma amesema bado kuna changamoto katika huduma za kijamii hasa za afya akisema wananchi wamekuwa wakizilalamikia.

Semu amesema ili kuondokana na kadhia hiyo amewataka wananchi wa Kongwa na Watanzania kukichagua ACT-Wazalendo katika chaguzi zijazo, akisema kipo tayari kuwahudumia na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“ACT- Wazalendo ipo tayari kuwahudumia, tutahakikisha huduma za afya zinakuwa, tumedhamiria kubadilisha historia ya namna bora ya kuwahudumia Watanzania katika maeneo mbalimbali,” amesema Semu.

Related Posts