Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa jinsi aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Ukonga, Josephat Mkama na wenzake wawili walivyoghushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa na kujipatia Sh45 milioni.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala, ameeleza hayo leo Septemba 27, 2024 alipowasomea washtakiwa maelezo ya awali ya kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili.
Washtakiwa wengine ni aliyekuwa Ofisa Tehama wa gereza hilo, Sibuti Nyabuya na mfanyabiashara, Joseph Mpangala, mkazi wa Mbezi, Dar es Salaam.
Washtakiwa katika kesi hiyo namba 25517/2024 wanakabiliwa na mashtaka manne ya kuongoza genge la uhalifu, kughushi barua ya msamaha wa Rais kwa wafungwa, kuwasilisha nyaraka ya kughushi na kujipatia Sh45 milioni kwa njia ya udanganyifu.
Kasala amedai Machi 18, 2016 wafungwa watatu wenye asili ya China ambao ni namba 585/2019 Song Lei, namba 205/2019 Xiu Fu Jie, na namba 206/2016 Haung Quin, walihukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo katika Gereza la Ukonga.
Amedai walihukumiwa vifungo tofauti kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kukutwa na nyara za Serikali na hawakuwa wakijuana.
Inadaiwa Desemba 21, 2022, Mkama akiwa mkuu wa gereza hilo na Nyabuya akiwa ofisa Tehama walitengeneza nyaraka ya kughushi yenye kichwa cha habari ‘Nyongeza ya msamaha kwa wafungwa katika kuadhimisha miaka 61 ya Uhuru.”
Inadaiwa nyaraka hiyo ambayo ni barua ya Desemba 21, 2022 ilionyesha imesainiwa na aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani Kaspar Mmuya, kuwa wafungwa hao watatu wameongezwa katika idadi ya wafungwa waliopewa msamaha na Rais.
Desemba 27 na 28, 2022 inadaiwa Mkama aliwaita wafungwa hao watatu ofisi kwake, akiwa na mwenzake Mpangala na kuwaonyesha barua hiyo na hati ya kuwatoa gerezani, akiwataka watoe Sh45 milioni kama sharti la wao kuondolewe gerezani.
Upande wa mashitaka unadai Mkama aliwaelekeza wafungwa hao fedha wampe Mpangala na kwamba, wafungwa hao walitekeleza maelekezo hayo.
Inadaiwa licha ya malipo kufanyika wafungwa hao watatu hawakuwahi kutolewa gerezani.
Imeelezwa siku chache baadaye wakili Aloyscious Mandago anayemwakilisha Song Lei alienda gerezani kumtembelea mteja wake aliyemweleza aondoe kesi waliyofungua Mahakama ya Rufaa kupinga adhabu waliyopewa kwa sababu wamepata msamaha wa Rais.
Inadaiwa alimuonyesha barua aliyopewa na Mkama na kwamba wanasubiri barua ya kutolewa gerezani.
Kasala amedai wakili huyo alimweleza mteja wake kuwa taarifa hizo ni za uongo, hivyo alimpigia Mkama ambaye hakupatikana kwa wakati huo.
Kesho yake inadaiwa wakili huyo alikwenda ofisi kwa Mkama akamuonyesha barua ya msamaha, ikielezwa alimtaka waongeze Sh18 milioni ili ashughulikie hati ya kuwatoa gerezani.
Kasala anadai Mandago alikwenda kuonana na Ofisa Tawala wa Gereza la Ukonga, Lusekelo Mwanjati ili kujiridhisha kuhusu msamaha huo, ambaye naye alimweleza alipokea barua yenye kichwa cha habari cha msahama kwa wafungwa watatu kutoka kwa Sajenti Asha Mohamed, ambaye ni katibu muhtasari ofisi ya Mkuu wa Gereza.
Mwanjati inadaiwa alimweleza Mandago kuwa barua hiyo ilikuwa ikimtaka atekeleze maelezo aliyopewa na Mkama lakini akamwambia barua hiyo si ya kweli, imeghushiwa.
Inadaiwa barua hiyo ilipelekwa kwenye vyombo vya ulinzi ambavyo vilifanya uchunguzi kuhusu tuhuma hizo na ikagundulika Mkama na wenzake waliongoza genge la uhalifu na walijipatia Sh45 milioni kwa kudanganya wafungwa hao kuwa wameongezwa katika msamaha wa Rais, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Amedai washitakiwa walikamatwa na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi kwa kuhojiwa na baadaye walifikishwa mahakamani.
Baada ya maelezo hayo kusomwa, washtakiwa walikubali majina yao, nyadhifa walizokuwa nazo na siku walipofikishwa mahakamani, huku wakikana maelezo mengine yote kuhusu mashitaka yanayowakabili.
Upande wa mashtaka umesema utakuwa na mashahidi 15 ili kuthibitisha mashitaka.
Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi Oktoba 24, 2024 katika mahakama hiyo.
Wakili Henry Munisi anayewawakilisha washitakiwa amesema watakuwa na mashahidi sita.
Mkama na Mpangala wametimiza masharti ya dhamana na kuachiwa huru kwa dhamana, huku Nyabuya akishindwa kutimiza masharti na amepelekwa rumande.
Masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama hiyo, Septemba 19, 2024 ni kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya Taifa ambao watawasilisha mahakamani fedha taslimu ama hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh7.5 milioni.
Hakimu Mkazi Mkuu Geofrey Mhini anayesikiliza kesi hiyo ameiahirisha hadi Oktoba 10, 2024 kwa ajili ya kutajwa kuona kama Nyabuya atakuwa ametimiza masharti ya dhamana. Usikilizaji utaanza Oktoba 24, 2024.