WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wameendelea kuonyesha ubora wao msimu huu wa mashindano 2024/25 wakiwa chini ya kocha, Fadlu Davids kwa kuibuka na ushindi wa tatu mfululizo katika ligi bila ya kuruhusu bao baada ya kuichapa Azam mabao 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Katika michezo mitano, mitatu ya ligi na miwili ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba imefunga jumla ya mabao 12, ikiwa ni wastani wa kufunga mabao 2.4 katika kila mchezo (kwa ligi tu ina wastani wa kufunga mabao matatu kwa kila mchezo) huku nyavu zao zikiguswa mara moja tu (kimataifa) na ilikuwa dhidi ya Al Ahly Tripol ambapo hata hivyo katika mchezo huo waliibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Ndani ya dakika 90 za mchezo dhidi ya Azam, uliopigwa jana usiku, Simba walicheza kwa nidhamu ya hali ya juu, wakitumia mbinu mbalimbali kuhakikisha wanatawala mchezo huo na kumzuia mpinzani wao kuwa na madhara langoni kwao.
Huku wakiweka presha ya haraka kwa wachezaji wa Azam, walihakikisha hakuna nafasi nyingi za wazi za kushambulia, huku wakiimarisha safu yao ya ulinzi kwa kufanya ‘blocks’ na kufunga njia zote mbele ya viungo na mabeki.
Simba walitumia kwa ufanisi mipira iliyokufa na matunda yake ni bao la pili ambalo lilifungwa na Fabrice Ngoma moja na kasi ya wachezaji wake hasa pale ambapo mabeki wa Azam walikuwa wakijisahau. Kila mara mpinzani alipoteza mpira, walijibu kwa haraka na kuanzisha mashambulizi ambayo yaliwaletea matokeo mazuri.
Pia, walicheza kwa akili, wakitunza nguvu zao kwa kutokukimbia sana na kuhakikisha wachezaji wanakaa karibu ili kupunguza umbali kabla ya kuvuka katika nusu ya pili ya uwanja wakati wakishambulia.
Mbele ya goli, Simba walikuwa na ufanisi, ingawa walipoteza nafasi kadhaa katika kipindi cha kwanza ambapo walipaswa kwenda mapumziko wakiwa na mabao zaidi ya moja na hapa kocha wa kikosi hicho, Fadlu anaeleza; “Tulisikitika kwamba hatukuongeza mabao mengine katika kipindi cha kwanza. Tulitakiwa kuua mchezo mapema, tulipata nafasi nyingi kutokana na mipango tuliyoipanga na tulivyochambua wapinzani wetu,” alisema Davids.
Katika kipindi cha pili, Davids alifurahishwa na jinsi timu yake ilivyoweza kudumisha kasi ya mchezo licha ya changamoto ya mechi nyingi mfululizo kabla ya kukutana na Azam, jambo ambalo lilikuwa changamoto kwa wachezaji wake kimwili.
“Ilikuwa ya kuvutia kuona jinsi tulivyoweza kudumisha kiwango cha juu katika kipindi cha pili. Kumbuka, tulitoka kwenye mechi kali, na ilibidi tuzingatie jinsi ya kusimamia nguvu za wachezaji. Hii ndiyo sababu nilifanya mabadiliko mara tatu dakika ya 60,” aliongeza Davids.
Kwa upande wake kocha wa Azam FC, Rachid Taoussi ameonyesha wazi kutofurahishwa na maamuzi ya mwamuzi, Herry Sasii kwenye mchezo huo.
“Nilikuwa na hasira sana kwa sababu hatukupaswa kupoteza,” alisema kocha huyo.
Kocha huyo pia alilalamikia jinsi mwamuzi huyo alivyoshughulikia faulo, akisema Simba waliruhusiwa kucheza kwa nguvu bila kuadhibiwa, lakini Azam walikuwa wakipigwa faulo mara kwa mara bila hatua kuchukuliwa.