KOCHA wa zamani wa Stand United na Gwambina, Athuman Bilal ‘Bilo’ amesema matokeo inayoyapata Pamba Jiji ni kutokana na ugumu na ushindani mkali uliopo Ligi Kuu msimu huu huku akiwataka mashabiki kuacha presha na kuipa muda timu hiyo.
Bilo alisema matokeo iliyoyapata timu hiyo mpaka sasa ni sahihi na yanastahili kutokana na ugeni wake kwenye michuano hiyo huku akitaka ivumiliwe na kupewa angalau mechi kuanzia saba ili mambo mazuri yaanze kuonekana.
Pamba Jiji ambayo ni msimu wake wa kwanza Ligi Kuu Bara baada ya kukosekana kwa miaka 24, haijapata ushindi katika mechi tano ikiambulia suluhu tatu, sare moja na kupoteza mechi moja ikivuna alama nne na kukamata nafasi ya 12.
Bilal ambaye ni kocha mkongwe katika soka la Tanzania akiwa amezifundisha Stand United, Rhino Rangers, Gwambina, Singida United na Alliance FC, alisema uvumilivu ndiyo kitu kitakachoikoa timu hiyo kwa sasa, na wachezaji kujituma wakijua kiu ya mashabiki wao kupata matokeo mazuri.
“Pamba inacheza vizuri isipokuwa wananchi wana hamu ya kupata matokeo lakini ligi ni ngumu kwa matokeo anayopata Pamba si mabaya kutokana na ugeni wa timu, inatakiwa subira kuanzia mechi labda ya saba na kuendelea timu itakuwa imeshasimama imara na itapata matokeo,” alisema Bilo.
“Ni subira tu unajua wananchi wa Mwanza sasahivi wana presha ya kupata matokeo lakini muda unahitajika na timu itafanya vizuri, yaani timu iko vizuri labda tu kidogo kwenye ufundi kasi iongezeke kwasababu mechi nyingi ikiwemo dhidi ya Mashujaa tunateketea kidogo, ni muda tu mambo yatakuwa mazuri,” alisema.
Kocha huyo ameshauri wachezaji kupambana na kujituma katika mechi zijazo ugenini dhidi ya Coastal Union na Yanga zitakazopigwa jijini Dar es Salaam Septemba 28 na Oktoba 3, kuhakikisha wanavuna alama kama walivyofanya ugenini dhidi ya Azam.
“Wachezaji wanatakiwa watambue hivyo jinsi walivyocheza na Azam kwa kujituma na kupambana ndivyo wanatakiwa wacheze na Yanga na Coastal Union. Ni wachezaji kwanza kujituma na kutambua nini watu wanahitaji kama huwezi kupata pointi tatu unatakiwa upate moja,” alisema Bilo.