Mbeya. Septemba unaweza kuwa mwezi mbaya zaidi mkoani Mbeya kutokana na ajali za barabarani, baada ya watu 12 kufariki dunia na wengine 23 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea leo Septemba 27, 2024 wilayani Mbeya.
Ajali hiyo imetokea eneo la Jojo Kata ya Ilembo, ikihusisha gari aina ya Fuso ambalo lilikuwa likielekea mnada.
Alfajiri ya Septemba 6, basi la Kampuni ya A-N Classic lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea mkoani Tabora lilipata ajali na kusababisha vifo vya watu 12, akiwamo mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo ya familia, Amduni Nassor aliyekuwa dereva. Katika ajali hiyo watu 44 walijeruhiwa.
Septemba 4, katika Kata ya Chimala, wilayani Mbarali mkoani hapa ilitokea ajali nyingine ikihusisha basi la Kampuni ya Shari Line iliyosababisha vifo vya watu tisa na kujeruhi wengine 18.
Katika ajali ya leo Septemba 27, Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Ilembo, Dk Philimon Irungi amethibitisha kupokea miili ya watu 11, akieleza majeruhi mmoja alifariki dunia baada ya kufikishwa kituoni hapo.
“Eneo la tukio walifariki dunia 11, ikatangulia miili sita kisha ikaja mitano na mmoja akafariki wakati akipatiwa matibabu, majeruhi ni 23” amesema Dk Urungi.
Mmoja wa mashuhuda katika eneo la ajali, Elias Shiwiwi amesema gari hilo la Kampuni ya Chakazi likiwa limebeba wafanyabiashara kuwapeleka mnadani lilikatika propela na kusababisha ajali hiyo.
“Palepale wamefariki watano, baadaye wengine watano wakafia njiani wakielekea Kituo cha Afya Ilembo nikiwa nawaona,” amesema Shiwiwi.
Wiliam Mwashiuya, majeruhi wa ajali hiyo amesema alisikia kelele kabla ya ajali na kwamba alipokuja kujitambua aliona gari likianguka mtoni. Amejeruhiwa mguu na kichwani.
“Tulipanda lori lakini eneo lile likawa na mteremko na kawaida yake huwa abiria wanashuka kwenye mteremko huo na tulifanya hivyo, baadaye dereva akasema tupande ndipo ikatokea hivyo,” amesema.
Josephine Kinyata, amesema hakujua ajali ilivyotokea kabla ya kujitambua amefikishwa kituo cha afya.
“Yaani hata sijui nianzie wapi, sielewi ilivyotokea ajali na baadaye kujikuta nimefikishwa hapa kituo cha afya, kimsingi Watanzania wenzetu watuombee,” amesema.
Baada ya ajali za Septemba 4 na 6, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango Septemba 7 alikemea tabia za uzembe na kutozingatia sheria za usalama barabarani ambazo zimesababisha kushamiri kwa ajali za barabarani zinazogharimu maisha ya wananchi wengi.
Akimwakilisha Raia Samia Suluhu Hassan katika kilele cha maadhimisho ya jubilei ya miaka 50 ya Kanisa la New Life Outreach iliyofanyika katika kanisa hilo Sakina, mkoani Arusha aliwataka wakaguzi wa magari wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) na Kikosi cha Polisi cha Usalama Barabarani kutimiza wajibu wao ili kudhibiti magari mabovu yasiingie barabarani, kuhakikisha vidhibiti mwendo vinafanya kazi, na kukagua sifa za madereva hasa wa mabasi ya abiria na malori.
Alisema wamiliki wa mabasi na malori wanapaswa kuhakikisha magari yao yanakuwa na madereva walau wawili kwa safari zote ndefu zinazozidi kilomita 300.
Pia aliuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha alama za tahadhari zinawekwa katika maeneo yote hatarishi ya barabara kuu.