Dar es Salaam. Uwepo wa dhana potofu na elimu duni ya afya ya uzazi katika jamii vimetajwa kuchangia kuwakosesha vijana kupata elimu ya uzazi wa mpango.
Hayo yamebainishwa jana Septemba 26, 2024 na baadhi ya vijana waliozungumza katika mkutano wa wadau wa afya ya uzazi katika kuadhimisha Siku ya Uzazi wa Mpango Duniani uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo, Getrude Clement ambaye ni kijana na Mshauri Jopo la Vijana Washauri kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA Tanzania), amesema katika baadhi ya jamii hasa za vijijini huwachukulia vijana wanaofuatilia uzazi wa mpango kuwa ni wahuni.
Getrude amesema hata anapojitokeza mtu au taasisi kufundisha vijana kuhusu uzazi wa mpango, huonekana kama anawafundisha kuanza uhuni mapema.
“Hiyo inarudisha nyuma jitihada za vijana katika kutafuta elimu na kupata huduma za uzazi wa mpango wakihofia kuonekana wameanza tabia za kihuni,” amesema.
Amesema moja ya manufaa ya uzazi wa mpango ni pamoja na kuwasaidia vijana kufahamu namna sahihi ya kujitunza na kuwaepusha na mimba zisizotarajiwa ambazo zinaweza kuwa kikwazo cha kutimiza ndoto zao.
Amejitolea mfano yeye binafsi kuwa elimu aliyoipata kuhusu masuala ya uzazi wa mpango, imemsaidia kuweza kuhitimu masomo yake bila ya kupata mimba zisizotarajiwa.
Rahim Nasser ambaye ni Ofisa Vijana kutoka taasisi ya Management and Development for Health (MDH) anasema changamoto nyingine katika baadhi ya jamii imekuwa ikiwaweka kando vijana wa kiume katika masuala ya uzazi wa mpango kwa kuona masuala hayo yanawahusu wanawake pekee.
Nasser anasema ni vyema jamii kuondokana na imani hiyo kwani watoto wa kiume nao wana haki ya kupata elimu na kufahamu kuhusiana na masuala ya uzazi wa mpango.
Anasema mwanaume anapokuwa na uelewa kuhusiana na afya ya uzazi pamoja na kusaidia kuepukana na mimba zisizotarajiwa lakini pia inasaidia kuondoa unyanyapaa katika hali mbalimbali wanazopitia wasichana akitolea mfano suala la hedhi.
“Tuwaelimishe pia watoto wa kiume ili waweze kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko katika jamii,” amesema.
Selia Rehani ambaye ni mmoja kati ya kijana aliyeshiriki katika mkutano huo anasema changamoto nyingine ni baadhi ya wazazi kuwa na mitazamo hasi kuhusiana na masula ya uzazi wa mpango.
Rehani anasema kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha baadhi ya wazazi wamekuwa wakihofia kuzungumza na watoto wao kuhusu masuala hayo, wakidhani kuwa kwa kufanya hivyo ni kumfanya aweze kujiingiza katika uhusiano wa kingono mapema.
Rehani anasema kutokana na kukosa taarifa sahihi kuhusu masuala ya uzazi wa mpango, huchochea baadhi ya vijana kuingia katika matumizi holela ya dawa za P2 zinazotumika kuzuia mimba, jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya yao.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo Clara Maliwa ambaye ni Ofisa Miradi kutoka shirika la Young and Alive Initiative, amesema watu wenye ulemavu wamekuwa wakipitia changamoto ya kupata elimu hiyo ikiwa pamoja kunyanyapaliwa.
Kwa upande wa changamoto ya mawasiliano Maliwa anasema katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya uzazi, hakuna mazingira rafiki kwa ajili ya kuweza kupata taarifa hizo.
Maliwa ametoa mfano wa kutokuwepo kwa wakalimani wa lugha za alama, maandishi ya nukta nundu pamoja na miundombinu mingine kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Pia amebainisha uwepo wa unyanyapaa kwa watu wenye ulemavu kwa kuwaona kuwa hawana haki ya kupata elimu pamoja na huduma ya afya ya uzazi.
Maliwa anashauri kuendelea kutolewa kwa elimu kwa jamii pamoja na watu wenye ulemavu kuhusu umuhimu wa haki ya afya ya uzazi kwa watu wenye ulemavu.
Meneja Mawasiliano kutoka UNFPA Tanzania, Dk Warren Bright ametoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuachana na mila potofu kudhani kumfundisha watoto masuala ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango ni kumfanya mtoto au kijana kujiingiza katika uhusiano kabla ya wakati.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohammed Mang’una amesema elimu ya afya ya uzazi kwa vijana ni muhimu kwani itasaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa; itawezesha vijana kujitunza, vilevile kuwaepusha na magonjwa mbalimbali ya zinaa.