Dodoma. Hukumu ya kesi ya jinai ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti, mkazi wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam itatolewa Septemba 30, 2024.
Kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024, inawakabili washtakiwa wanne wakiwamo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Septemba 27, wakili wa washtakiwa hao, Meshack Ngamando amesema kila kitu kilichotakiwa kwenye kesi hiyo kimekamilika, hivyo kinachosubiriwa ni uamuzi wa Mahakama.
Amesema leo wamefanya mawasilisho ya mwisho ya kisheria kuhusu mwenendo mzima wa kesi hiyo na kwamba wamewasilisha hoja kuhusu kasoro zilizojitokeza wakati wa usikilizwaji.
“Leo tumepata nafasi ya kuwasilisha mawasilisho ya mwisho, kuhusu mwenendo wote wa kesi kuanzia hati ya mashtaka, ukamataji, utambuzi, mashahidi, vielelezo vilivyotolewa mahakamani kwa muda wa saa tatu kuanzia saa nane mchana hadi saa 11.00 jioni.
“Upande wa Jamhuri pia umewasilisha yao kuanzia saa 11.00 jioni hadi saa moja usiku kwa hiyo kinachosubiriwa kwa sasa ni uamuzi wa mahakama,” amesema Ngamando.
Amesema mwenendo mzima wa kesi ulikuwa mzuri na kumbukumbu zilichukuliwa vizuri.
Wakili Godfrey Wasonga amesema wapo tayari kwa uamuzi utakaotolewa na Mahakama.
Upande wa utetezi jana Septemba 26, 2024 ulifunga ushahidi wake ambao umetolewa na washtakiwa pekee. Hawakuwa na kielelezo chochote. Awali upande wa utetezi ulisema ungekuwa na mashahidi 10 na vielelezo sita.
Katika kesi hiyo inayosikilizwa faragha katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 18 na vielelezo 12 kuthibitisha mashitaka dhidi ya washtakiwa.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti huyo ambaye mahakamani anatambulika kwa jila la XY.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule washtakiwa baada ya kusomewa mashataka walikana na kutokana na unyeti wa kesi hiyo hawakupatiwa dhamana.