Ibrahim Bacca asisitiza ile ya KenGold ni sare ya 1-1

BAADA ya kuipa pointi tatu Yanga ugenini dhidi ya Ken Gold, beki Ibrahim Hamad ‘Bacca’ amesema ubao unasoma sasa ni 1-1 dhidi ya mabeki wenzake wa timu hiyo.

Bacca ambaye anaitumikia Yanga kwa msimu wa tatu sasa amefunga bao lake la kwanza akiungana na Bakari Mwamnyeto na Dickson Job wote wanacheza eneo la ulinzi. Kwa hiyo ni kama amesawazisha walichokuwa wanamtambia Job na Mwamnyeto na sasa maisha yanaendelea baada ya kuweka kumbukumbu sawa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Bacca alisema anafurahi kuipa timu yake pointi tatu muhimu kwenye uwanja aliokiri kuwa ulikuwa mgumu kwao, lakini amewataja Mwamnyeto na Job kuwa ubao ni moja moja.

“Nina furaha kuipa Yanga pointi tatu lakini pia nina furaha nimefunga bao chini ya Miguel Gamondi kikosi ambacho kila mchezaji anafunga walianza nimemaliza nawakumbusha tu,” alisema na kuongeza;

“Ulikuwa mchezo mgumu kila mchezaji alikuwa anapambana kuhakikisha anaipambania timu iweze kupata pointi tatu muhimu kitu ambacho kwa upande wangu nilifanikiwa nikiifungia timu bao ambalo ni la kwangu tangu nimeanza kuichezea timu hii.”

Akizungumzia mchezo kwa ujumla alisema matarajio yao kama wachezaji yalikuwa ni makubwa lakini dakika 90 ziliamua kuwapa pointi tatu na bao moja wamesahau matokeo yaliyopita wanaangalia mchezo unaofuata.

Nahodha wa Yanga, Job alimpongeza Bacca kwa kupachika bao la ushindi ambalo limewapa pointi tatu muhimu.

“Bacca alitumia vizuri nafasi moja aliyoipata licha ya kutengeneza nafasi nyingi hasa kipindi cha kwanza, bao alilifunga litaongeza morali kwenye timu,” alisema na kuongeza;

“Uwanja haukuwa rafiki kwetu ndio maana tumepata matokoe hayo, kikubwa ni pointi tatu, sasa tunarudi kwenye uwanja wetu wa nyumbani tutarekebisha makosa tuliyoyafanya.”

Related Posts