Jela maisha kwa kumbaka binti wa miaka tisa

Iringa. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Iringa imemhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela mkazi wa eneo la Migoli, Fumo Renatus (26) baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka mtoto wa miaka tisa.

Katika hukumu hiyo ambayo Mwananchi imeiona nakala yake leo Ijumaa Septemba 27, 2024, Fumo amehukumiwa kutumikia adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Mwandamizi wa mahakama hiyo, Honorious Kando, Alhamisi Septemba 26, 2024.

Hakimu Kando amemtiani hatiani kwa kosa hilo baada ya kuridhika kuwa ushahidi wa upande wa mashtaka kwa kiwango kinachotakiwa kisheria yaani bila kuacha shaka.

“Baada ya mahakama kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na kulinganisha na utetezi, Mahakama hii, imeridhika kuwa upande wa mashtaka umethibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa kuwa alitenda kosa hilo,” amesema Hakimu Kando na kuongeza:

“Hivyo mahakama hii imemtia hatiani mshtakiwa Fumo Renatus kama alivyoshtakiwa na Jamhuri”.

Kabla ya kumtia hatiani mshtakiwa, mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Muzna Mfinanga amesema kuwa hakuna kumbukumbu za nyuma za mshtakiwa za uhalifu.

Hata hivyo, Wakili aliiomba mahakama hiyo itoe adhabu kali kwa mshtakiwa huyo kwa mujibu wa sheria  ili iwe fundisho kwa wengine ambao walikuwa na dhamira ya kujaribu kufanya vitendo hivyo.

Mshtakiwa wakati alipopewa nafasi ya shufaa (huruma ya Mahakama katika kutoa adhabu) amesema kuwa aliomba mahakma impunguzie hadhabu kwa sababu ana familia  inayomtegemea.

Akitoa adhabu hiyo Hakimu Kando amesema kuwa amezingatia maombi ya upande wa mashtaka na maombi ya shufaa ya mshtakiwa pamoja na matakwa ya sheria.

“Hivyo mshtakiwa Fumo Renatus unahukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo cha maisha gerezani”, amesema Hakimu Kando.

Kwa mujibu wa hukumu hiyo ya kesi hiyo ya jinai namba 20 ya mwaka 2023, kwa siku mbili tofauti mshtakiwa, Fumo alikuwa akimlaghai binti huyo na kwenda naye kwenye kichochoro kisha kumuingizia vidole katika sehemu zake za siri.

Siku ya tukio akiwa na mtoto huyo alimuingilia kwa kumuingiza uume wake sehemu za siri na alipomaliza akampatia fedha kiasi cha Sh500, huku akimtisha asiseme popote kwani atamfanya kitu kibaya,” ilielezwa mahakamani hapo.

Shahidi wa pili katika kesi hiyo ambaye ni mama mzazi, alisema alibaini tofauti kwa binti yake namna ambavyo alikuwa anatembea alipo msogelea alikuwa ni mtu mwenye uoga huku mkononi akiwa ameshika Sh500.

Mama huyo alisema kuwa baada ya kuona hali hiyo alimuhoji kwa kumbana ndipo akaeleza kuwa fedha hiyo alipatiwa na mtu aliyemtambua kwa jina Fumo baada ya kumfanyia kitendo hicho, huku akidai kuwa alimtisha asiseme popote kwamba atamfanyia kitu kibaya.

Hivyo alifanya maamuzi ya kwenda ofisi ya kijiji, kisha kituo cha Polisi ambapo aliandikiwa Fomu ya Polisi namba 3 (PF3) kwa ajili ya kwenda hospitali.

Kwa upande wake shahidi wa tatu wa kesi hiyo ambaye ni daktari alithibitisha alimpokea binti huyo na alipo mchunguza alibaini kuwepo kwa michubuko sehemu zake za siri hali iliyodhihirisha aliingiliwa na kitu butu.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alipopewa nafasi ya kujitetea alikana kutenda kosa hilo.

Related Posts