Kagera Sugar, Fountain Gate patachimbika Bara

MAKOCHA wa Fountain Gate na Kagera Sugar wametambiana kwa kila mmoja kuhitaji pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara unaopigwa leo kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, mjini Babati Manyara  kutokana na wachezaji wa pande zote mbili kuwa kwenye morali nzuri.

Wenyeji wa mchezo huo, ni Fountain na ni pambano pekee linalopigwa leo katika mfululizo wa ligi hiyo inayoingia raundi ya sita, huku kama ilivyo kwa Kagera nao wanashuka uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya matokeo mazuri ya mechi zilizopita.

Kocha mkuu wa Fountain Gate, Mohammed Muya alisema umoja uliopo kati yao na wachezaji ndio siri ya mafanikio wanayoyapata huku akitaja mchezo wa leo dhidi ya Kagera na hawatafanya makosa kwani wanahitaji pointi tatu zitakazowaweka kileleni mwa msimamo ikiing’oa Singida Black Stars inayoongoza.

Singida inaongoza msimamo ikiwa na pointi 12 kutokana na michezo minne, huku Fountain ikifuata na alama zao 10 ikicheza michezo mitano.

“Wachezaji wote wapo katika hali nzuri na kila mmoja anautamani huo mchezo, naamini wale watakaoanza hawatafanya makosa, ili kuona timu itaondoka na matokeo mazuri,” alisema Muya na kuongeza;

“Tutaingia kwa kumuheshimu mpinzani wetu ambao wametoka kupata matokeo mchezo wao wa mwisho hivyo naamini watakuwa katika morali nzuri hivyo natarajia mchezo wa ushindani.”

Kwa upande wa kocha Kagera, Paul Nkata aliyeanza kwa kusuasusa kwa kupoteza mechi tatu mfululizo kisha kutoka sare na kushinda mchezo uliopita dhidi ya KenGold, alisema wachezaji wana morali kubwa na wamejiandaa vyema kukabiliana na Fountain Gate, japo alikiri hawatarajii mteremko.

“Tunaenda kukutana na timu ambayo ipo kwenye ubora tutaingia kwa kuwaheshimu huku na sisi morali yetu ikiwa juu naamini utakuwa mchezo mzuri.” alisema Nkata raia wa Uganda aliyeajiriwa hivi karibuni kuchukua nafasi kocha Fred Felix ‘Minziro’ aliyemaliza mkataba na klabu hiyo.

Licha ya tambo hizo za makocha, lakini rekodi zinaonyesha zimeshakutana mara nne, huku hakuna mbabe, kwani kila moja imeshinda mechi mbili na kupoteza mbili na hakuna sare yoyote iliyowahi kupatikana.

Mara ya kwanza timu hizo kukutana ilikuwa Oktoba 21, 2022 Fountain enzi ikifahamika kama Singida Big Stars iliposhinda ugenini kwa mabao 2-1 kisha jkutamba tena ziliporudiana Januari 17, mjini Singida kwa ushindi wa 1-0, ndipo Kagera ikazinduka msimu uliopita kwa kushinda nje ndani kwa mabao 3-2 na 1-0 mtawalia.

Hivyo pambano hilo la leo litakaloanza saa 10:00 jioni, kila moja itakuwa na kiu ya kuzoa alama tatu na kuboresha rekodi iliyopo, lakini kujiwepa pazuri katika msimamo, huku kila moja ikitegemea nyota wanaounda vikosi hivyo.

Fountain itaendelea kumtegemea Seleman Mwalimu, Edgar William, Dickson Ambundo na Salum Kihimbwa walio na mwanzo mzuri na kikosi hicho, huku wageni Kagera watawategemea Obrey Chirwa, Nassor Kapama na Mganda, Peter Lwasa aliyefunga mabao mawili waliopoizamisha KenGold.

Related Posts