Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imewataka vijana kuja na bunifu zenye tija kwa jamii, ili hatimaye wapate wafadhili watakaosaidia kukuza bunifu hizo.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Septemba 27, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho ya tisa ya Sahara Sparks, yaliyolenga kutoa fursa kwa vijana wabunifu kujitangaza na kupata wafadhili katika bunifu zao.
Akizungumza katika maonyesho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Watu, Ujuzi na Malengo’, Dk Nungu amesema moja ya changamoto wanayoipitia vijana mpaka kukosa ufadhili ni kukosa mawazo yenye sifa.
“Ni kweli tuna mawazo mazuri lakini wakati mwingine ili upate ufadhili ni lazima wazo lako lijaribiwe ili kujua kama linaendana na mahitaji ya soko? Kila mwekezaji anaangalia biashara, anaweka fedha sehemu ambayo itarudisha faida na ataendelea kusaidia wengine,” amesema.
Dk Nungu amewaasa vijana kuwa tayari kujifunza, kupokea mrejesho na kubadilika ili kuendana na wakati, lakini pia kuhudhuria fursa mbalimbali za maonyesho kitaifa na kimataifa ili kuboresha mawazo yao na kuweza kutumika na kupata wa wawekezaji.
Akitoa mifano ya baadhi ya vijana walioshauriwa kuboresha mawazo yao, amesema vijana hao walipata mikopo wakarejesha na sasa wana uwezo wa kukopa tena ikiwa watahitaji.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesema Serikali imekuja na mfumo mpya utakaoingizwa kwenye mitaala na kutumika shuleni wa namna ya kuwaendeleza wale wanaoonekana kuwa na utundu kwa kufanya bunifu mbalimbali.
“Serikali inaandaa mfumo wa kuwatambua wanafunzi wenye vipaji vya kibunifu kuanzia ngazi ya shule ya msingi na baadae kuwaendeleza kufikia ndoto zao, mfumo huu umeanza rasmi mwaka huu na unaendelea kufanya kazi, na kuwa mtoto atakayepata mafunzo hayo ya kuendeleza kipaji chake, atakapo maliza darasa la saba atapata cheti sawa na yule aliesoma Veta,” ameeleza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Sahara venture, Jumanne Mtambalike amesema katika maonyesho hayo wanaangazia ni kwa namna gani teknolojia, ubunifu na ujasiriamali, vitaweza kubadilisha maisha ya vijana wa Tanzania.
“Tuna vijana zaidi ya 100 watakaoonesha bunifu zao na wageni zaidi ya 1,500 watakaotembelea bunifu hizo.
“Lengo letu ni kufungua fursa kwa vijana na kuwaonesha namna teknolojia ilivyo na nafasi kubwa kwenye maisha yao na pia itawasaidia kujiandaa na changamoto za ajira,” amesema Mtambalike
Amesema kwa nmna nmoja ama nyingine kila shughuli ya leo inaguswa na teknolojia na ndiyo sehemu pekee inatoa ajira kwa vijana wa Kitanzania.
“Vijana wajue kwamba Serikali imefanya uwekezaji mkubwa, kama mnavyofahamu mkongo wa taifa umefika kila mahali,’’ amesema.
Tangu kuanzishwa kwa maonyesho hayo Mtambalike amesema kampuni nyingi za vijana ambazo zimefanikiwa, zimepita katika mifumo yao na kuunganishwa na wawekezaji.