Kocha Azam ajiweka pabaya akilia na marefa

KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi ameonja joto ya Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba kwa mabao 2-0, lakini akaonyesha wazi kutofurahishwa na uamuzi wa refa Herry Sasii na wasaidizi wake katika mechi hiyo iliyopigwa jana usiku kwenye New Amaan Complex, Zanzibar.

Taoussi aliyekumbana na kipigo cha kwanza tangu alipoajiriwa kuchukua nafasi ya Youssouf Dabo, alisema timu yake ilicheza vizuri, lakini uamuzi wa Sasii uliharibu mtiririko wa mchezo.

“Nilikuwa na hasira sana kwa sababu hatukupaswa kupoteza. Tulikuwa tunacheza vizuri, na wachezaji wangu wanaendelea kuimarika katika kila mchezo,” alisema kocha huyo, raia wa Morocco.

Alisisitiza kwamba wamepitia video ya mchezo huo na kugundua makosa yaliyofanywa ambayo yaliwagharimu.

Kocha huyo pia alilalamikia jinsi mwamuzi huyo alivyoshughulikia faulo, akisema Simba waliruhusiwa kucheza kwa nguvu bila kuadhibiwa, lakini Azam walikuwa wakipigwa faulo mara kwa mara bila hatua kuchukuliwa.

Hata hivyo, kocha huyo aliwapongeza wachezaji wa Azam kwa kuonyesha kiwango bora licha ya changamoto hizo.

“Nawashukuru wachezaji wangu kwa sababu walicheza vizuri. Simba ni timu nzuri, lakini hatukuwa na bahati,” alisema Taoussi ambaye huenda akakumbana na adhabu kutoka Bodi ya Ligi (TPLB) kupitia kanuni zinazosimamia ligi hiyo zinazokataza makocha, wachezaji na viongozi kuwajadili waamuzi.

Taoussi atabanwa na kanuni ya 40 kifungu cha (2) cha Udhibiti wa Kimashindano kinachoainisha kuwa, “Ni marufuku kwa kocha/kiongozi wa timu/klabu, mchezaji au mdau mwingine yeyote wa mpira wa miguu kushutumu au kutoa matamshi/maandiko/picha/video kwa lengo la kumkejeli au kumshutumu au kumkashifu au kumdhalilisha mwamuzi yeyote wa mchezo/kiongozi wa TFF/FA (M)/TPLB kwenye vyombo vya habari na mahali pengine popote.

“Kiongozi au mdau atakayekiuka atafungiwa idadi ya michezo isiyopungua mitatu au kutojihusisha na mpira wa miguu kwa kipindi kati ya miezi mitatu mpaka kumi na miwili na au faini kati ya Sh500,000 na 5,000,000.

Related Posts