Ligi Kuu Bara… Ngoja tuone inakuwaje

Leo jioni inapigwa mechi moja tu ya Ligi Kuu Bara kati ya wenyeji Fountain Gate dhidi ya Kagera Sugar, lakini sasa ni kwamba kesho kipute cha ligi hiyo kinaendelea kwa michezo mitatu ikikutanisha timu zilizopo nafasi tofauti tofauti zikiwania pointi tatu.

Mapema saa 8 mchana kuna mchezo utapigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kwa waburuza mkia KenGold watakaokuwa wenyeji wa Tabora United kabla ya saa 10:15 jioni Coastal Union na Pamba Jiji kuvaana jijini Dar es Salaam kila moja ikisaka ushindi wa kwanza wa msimu huu.

Baada ya vipute hivyo, saa 1:00 usiku itakuwa ni zamu ya Namungo kuikaribisha Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na kuhitimisha Jumamosi, kabla ya kesho Jumapili vigogo Simba, Yanga na Azam kuwa kibaruani katika viwanja tofauti katika mfululizo wa ligi hiyo iliyopo raundi ya sita.

Mechi hizo tatu za leo si mchezo kutokana na ukweli kwamba zinakutanisha timu zenye hali zinazofanana, lakini zikiwa zinahitaji kupata pointi tatu zitakazoziweka pazuri kabla ligi haijachagamka mbele ya safari.

LIGI 2
LIGI 2

Kila moja itakuwa ikishuka uwanjani kwa ajili ya mechi ya sita, kwani tayari zimeshacheza michezo mitano, lakini mambo sio mazuri hususan kwa wenyeji, KenGold waliopoteza michezo yote ukiwamo uliopita juzikati dhidi ya Yanga na kulala 1-0 kwa bao la beki wa kati, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’.

KenGold, inayoshiriki ligi hiyo kwa mara ya kwanza baada ya kupanda msimu huu kutoka Ligi ya Championship, ilianza kwa kipigo cha mabao 3-1 kutoka Singida Black Stars kwenye uwanja huohuo kabla ya kwenda ugenini na kupoteza michezo mitatu mfululizo, ikilala 2-1 mjini Babati, Manyara ilipovaana na Fountain Gate, kisha ikapigwa 1-0 na KMC na kufungwa tena 2-0 na Kagera Sugar mjini Bukoba.

Iliporudi nyumbani katikati ya wiki hii ikanyukwa bao 1-0 na Yanga na hivyo huenda leo isitamani kabisa kupoteza tena mbele ya mashabiki hasa kwa aina ya soka ililocheza mbele ya watetezi ambao walishindwa kulipiga lile soka lao lililozoeleka kiasi cha kutowafurahisha mashabiki licha ya kuzoa pointi hizo tatu.

Tabora inayoshiriki Ligi Kuu kwa msimu wa pili sasa baada ya msimu uliopita kunusurika kushuka kupitia ‘play-off’ dhidi ya Biashara United, imetoka kupoteza kwa 3-1 mchezo uliopita dhidi ya Singida Black Stars tena ikiwa nyumbani, kitu ambacho leo ikicheza ugenini ingependa kubadilisha upepo mbele ya KenGold.

Timu zote zimeonekana kuwa na ulaini ulioruhusu mabao mengi, kwani KenGold imefungwa mabao tisa na yenyewe kufunga mawili, wakati wageni wao wamefunga saba na kufungwa manne na zote zitashuka zikitegemea mastaa walioanza na moto katika mechi zilizopita.

Wenyeji wanatabia Ibrahim Joshua, mchezaji pekee aliyeifungia mabao hayo mawili, huku Tabora ikiwa na nyota wa zamani wa Yanga, Yacouba Songne, Heritier Makambo na wengine ambao kama mabeki wa KenGold wataendelea kufanya uzembe, basi wajue wanaweza kulizwa mapema.

Kitu kizuri ni kwamba timu hizo zitakuwa zinakutana kwa mara ya kwanza katika mechi za Ligi Kuu, lakini zinazofahamiana kwani zimecheza mara kadhaa katika Ligi ya Championshipa kabla ya kupanda daraja. Hautakuwa mchezo rahisi kwa timu zote.

LIGI 1
LIGI 1

Hizo ni timu zenye historia kubwa katika soka la Tanzania, zimeshawahi kutamba na kukubana mara kadhaa kabla ya Pamba kushuka daraja mwaka 2001. Hili ni pambano la kwanza kwa msimu huu, lakini ni la sita kwa kila timu kwani zimeshacheza mechi tano na ni kati ya timu nne ambazo hazijaonja ushindi Bara.

Coastal iliyotoka kupoteza mechi nne mfululizo ukiwamo ulopita dhidi ya JKT Tanzania, ndio wenyeji wa mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa KMC Complex, wakati Pamba ikitoka kutibuliwa na Mashujaa kwa kutoka sare ya 2-2 baada ya kuongoza kwa muda mrefu mabao 2-0 na ‘Wazee wa Mapigo na Mwendo’ kuyachomoa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Tofauti na msimu uliopita ambao Coastal ilionekana kuwa imara na moja ya timu mbili zilizozoruhusu mabao machache na kumaliza nafasi ya nne katika msimamo, msimu huu imeanza hovyo ikiruhusu wavu kuguswa mara saba na kufunga mabao mawili ikiwamo lile la sare ya 1-1 na KMC.

Pamba imetoka sare nne na kupoteza mchezo mmoja, na leo itakuwa na kazi ya kusaka ushindi wa kwanza kama ilivyo kwa wenyeji wao ambao kocha wa timu hiyo, Joseph Lazaro amekiri kwamba hajui kipi kinawasumbua kwani katika uwanja wa mazoezi wachezaji wanaonyesha umahiri, lakini wakiwa uwanjani wanafanya tofauti na vile walivyoelekezwa, japo ameshakaa nao na kuweka mambo sawa.

Coastal itaendelea kuwategemea washambuliaji wake John Makwata, Maabad Maulid, Charles Semfuko na Ernie Malonga kuichachafya ngome ya Pamba, huku wageni wakiwategemea nyota kama  John Nakibinge, George Mpole, Erick Okutu na Salehe Masoud ili kuondoa mdudu wa sare anayeiandama na kushinda ugenini.

LIGI 3
LIGI 3

Kwenye Uwanja wa Majaliwa kutakuwa na vita kubwa kati ya wenyeji Namungo dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons ambao hawajaonja ushindi wowote hadi sasa licha ya kucheza mechi nne kama walizocheza Wauaji wa Kusini walioshinda mara moja na kupoteza mechi tatu hadi sasa.

Rekodi zinaonyesha tangu Namungo ilipopanda daraja mwaka 2020 imekutana mara 10 na Prisons kwenye ligi na kupoteza mara nne, huku ikishinda mechi moja na nyingine tazo zilizosalia zikiisha kwa sare tofauti, ikiwa na maana wenyeji leo watakuwa na kazi ya kupindua meza kwa maafande hao, kwa sababu katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita uwanjani hapo iliisha kwa sare ya mabao 2-2 wakati mchezo wa ugenini ilipoteza 1-0.

Timu zote hadi sasa zimeonyesha kuwa na safu butu ya ushambuliaji, licha ya Namungo kupata ushindi wa 2-0 ilioupata ugenini mbele ya Coastal Unio na kuifanya iwe na mabao matatu katika mechi hizo nne, wakati wageni hawajafungwa wala kufunga bao lolote hadi sasa katika michezo minne iliyopita.

Katika mchezo wa leo mabeki wa timu zote watakuwa na kazi ya kuwachunga washambuliaji wasumbufu wanaoweza kuzitibulia ngome kwa kule kuwa na uchu wa mabao, Namungo ikiwa na Pius Buswita, Ritch Nkoli, Hassan Kabunda na wengineo watakaokuwa na kazi ya kuipita ngome ya Prisons chini ya Nurdin Chona, Salum Kimenya, Samson Mwituka wanaomlinda kipa Mussa Mbisa mwenye ‘clean sheet’ nne.

Kwa upande wa safu ya ushambuliaji ya Prisons kuna Haruna Chanongo, Hamis Mayombya na Meshack Abraham watakaokuwa na kazi ya kuipita ngome ya Namungo inayolindwa na kipa Beno Kakolanya na mabeki Djuma Shaban, Erasto Nyoni na wengine ili kutoka na ushindi ugenini ni japokuwa lazima wakaze buti.

Kocha wa Coastal Union, Lazaro alisema mchezo dhidi ya Pamba wamejipanga vilivyo ili kuhakikisha kwamba wapinzani wao hawachomoki.

“Tumejipanga kuzuia, kushambulia na kukaba ili kuweza kupata ushindi mkubwa, kwani tumewashawasoma wapinzani wetu na aina yao ya uchezaji,” alisema kocha huyo.

Beki wa Prisons, Kimenya alisema hawana presha yoyote japokuwa watakuwa wanacheza ugenini.

“Sio suala jepesi kucheza ugenini mashabiki, uwanja na kila kitu ni cha wapinzani ila safu yetu kama kawaida haitafunguka, hivyo Namungo ijapange tu,” alisema mchezaji huyo.

LIGI 4
LIGI 4

Baada ya mechi hizo tatu za leo, kesho Jumapili itapigwa michezo minne –  mapema saa 8:00 mchana vinara wa ligi hiyo, Singida Black Stars watakuwa wenyeji wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Liti mjini Singida, huku kila moja ikitoka kupata ushindi katika mechi zilizopita.

Singida Black Stars iliifunga Tabora United kwa mabao 3-1 ikiwa ugenini na JKT kushinda 2-1 nyumbani dhidi ya Coastal Union, kisha saa 10:15 jioni itakuwa ni zamu ya Mashujaa watakaovaana na Azam iliyotoka kupasuka nyumbani kwa mabao 2-0 mbele ya Simba.

Mashujaa yenyewe ililazimisha sare ya 2-2 ugenini kibabe mbele ya Pamba kwa kutoka nyuma ya mabao mawili na kumaliza dakika 90 ikivuna pointi moja muhimu na leo itakuwa na kazi ya kuepuka aibu iliyoikuta msimu uliopita kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma ilipolala 3-0 kwa Azam.

Saa 12:30 jioni itakuwa ni zamu ya Mnyama kumalizana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma katika pambano linalotarajiwa kuwa la kuvutia na mechi ya kwanza ya ligi msimu huu kupigwa uwanjani hapo tangu ulipofunguliwa baada ya awali kufungiwa na Bodi ya Ligi.

Haitakuwa mechi nyepesi kwa timu zote, lakini rekodi zinaibeba Simba mbele ya wenyeji wao, japo Dodoma Jiji ya Mecky Maxime inaonekana msimu huu imekuja kivingine.

Baada ya mchezo huo saa 3:00 usiku watetezi Yanga watamalizia shoo dhidi ya KMC iliyoshinda mechi moja na kutoka sare mbili na kupoteza pia katika michezo mitano iliyocheza, wakati Yanga ikicheza mechi mbili na zote ikishinda dhidi ya Kagera Sugar na KenGold kwa 2-0 na 1-0 mtawalia. Ngoja tuone.

Related Posts