Ligi ya Championship kuendelea tena kesho

BAADA ya Ligi ya Championship kuanza kwa kishindo na kushuhudiwa timu tano tu kati ya 16 zikiibuka na ushindi katika mechi za raundi ya kwanza, wikiendi hii kazi inaendelea tena baada ya jana kupigwa michezo mitatu, kesho kazi itakuwa kwenye michezo mingine mitatu kwenye viwanja vitatu tofauti.

Katika mechi za wiki zilizopigwa, ni Mtibwa Sugar, Songea United, Biashara United, Stand United na Mbuni ndizo zilizotoka uwanjani na ushindi, huku nyingine sita zikiambulia sare tofauti, huku nyota aliyewahi kuwika katika Ligi Kuu, Raizin Hafidh wa Mtibwa akiwa mchezaji pekee aliyefunga mabao mawili.

Raizin aliyewahi kukipiga Coastal Union na Dodoma Jiji, alifunga mabao hayo wakati wakiizamisha Green Warriors na kuiwezesha mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu wa mwaka 1999 na 2000 kukaa kileleni, ikiizidi Songea United iliyoanza kwa kuifumua Mbeya Kwanza kwa mabao 2-1.

Timu nyingine zilizoshinda mechi za raundi za kwanza ni Mbuni iliyoinyoosha maafande wa Polisi Tanzania kwa bao 1-0 kama ilivyofanya Biashara United dhidi ya Transit Camp na Chama la Wana, Stand iliyoichapa Kiluvya United, huku Malack Joseph wa Mbeya City akiwa mchezaji aliyefunga bao la kwanza la msimu huu katika mechi ya sare ya 2-2 dhidi ya Bigman (zamani Mwadui).

Baada ya shoo ya wiki iliyopita, kesho Jumamosi kuna mechi tatu za maana zinazopigwa ikiwa ni muendelezo wa ligi hiyo inayotoa timu za kupanda Ligi Kuu msimu wa 2025-2026.

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi hiyo, maafande wa Green Warriors watakuwa nyumbani dhidi ya African Sports iliyoanza kwa sare ya 1-1 na Cosmopolitan, mechi itakayopigwa mapema saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani.

Sio mechi nyepesi hata kidogo kutokana na ukweli Warriors haitataka kupoteza tena mchezo, ikizingatiwa itakuwa nyumbani, lakini wageni wao ambao ni mabingwa wa zamani wa Ligi Kuu ya Muungano 1988, Wana Kimanumanu watataka wazoe pointi tatu za kwanza katika ligi hiyo baada ya sare na Cosmo.

Baada ya mechi hiyo ya Mlandizi, saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi, Polisi iliyonyukwa na maafande wenzao wa Mbuni, itakuwa wenyeji wa TMA iliyoanza kwa suluhu ugenini mbele ya Geita Gold, muda huo huo Biashara itakuwa Uwanja wa Karume, mjini Musoma kuvaana na Kiluvya.

Mechi hizo za jioni sio za kitoto kutokana na kila timu kupenda kupata pointi tatu ili kujitengenezea mazingira mazuri wakati ligi ikizidi kushika kazi.

Lakini uhondo wa ligi hiyo ya pili kwa ukubwa kwa ngazui za klabu nchini utaendelea keshokutwa Jumapili kwa michezo miwili wakati itakapoikaribisha Geita Gold kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha huku ikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu mechi ya kwanza mbele ya TMA.

Songea United ambayo zamani ilifahamika kama FGA Talents iliyoanza msimu kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya Kwanza, itasalia kwenye Uwanja wa Majimaji, Songea kucheza na Bigman FC ambayo mechi yake ya kwanza ilitoka sare ya 2-2 na Mbeya City.

Kocha Mkuu wa Bigman, Salhina Mjengwa alisema msimu huu ni mgumu na tayari ushindani umeanza mapema kwa sababu kila timu imejiwekea malengo yake, hivyo jambo kubwa kwao wanalopambana nalo ni kuhakikisha hawadondoshi pointi zao kizembe.

Kocha wa Songea, Ivo Mapunda alisema alisema kiu yake ni kuendelea moto kwa kuzoa alama nyingine tatu, licha ya kukiri anatarajia ushindani mkali kutoka kwa Bigman na kuwaomba mashabiki wa klabu hiyo na Songea kwa jumla wajitokeze kwa wingi uwanjani kuisapoti timu hiyo.

Related Posts