Mashambulizi yaua watu takriban 700 Lebanon – DW – 27.09.2024

Katika kipindi hiki kukiripotiwa mapigano kati ya Israel na Hezbollah, maafisa waandamizi wa Israel wametishia kurudia mashambulizi kama ilivyotokea kwa Gaza katika ardhi ya Lebanon ikiwa Hezbollah wataendelea na mashambulizi yao, jambo linalozua hofu zaidi.

Alhamisi Shirika la Kimataifa la Uhamiaji lilikadiria kuwa zaidi ya watu 200,000 wameyakimbia makazi yao nchini Lebanon tangu Hezbollah kuanza kufyatua roketi kuelekea upande wa kaskazini wa Israel kwa lengo la kuunga mkono Hamas baada ya kuvamiwa na vikosi vya Israel, na kusababisha vita kati ya Israel na Hamas.

Idadi ya waliouawa Lebanon yadaiwa kupindukia watu 1,500

Lebanon inasema jumla ya watu 1,540 wameuawa ndani ya ardhi yake katika kipindi hicho chote cha mapigano.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa | Annalena Baerbock
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani,Annalena Baerbock akizungumza katika mjadala mkuu wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Mataifa kama Ujerumani, Marekani, Ufaransa na washirika wengine kwa pamoja yametoa wito wa kusitishwa mapigano kwa siku 21. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Israel na wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon wanapaswa kukubaliana na pendekezo hilo mara moja.

Akitoa kauli hiyo katika Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, amesema kuongezeka kwa machafuko katika kanda hiyo hakuwezi kumnufaisha yoyeto panapo husika suala la amani ya kudumu. Baerbock amesema kukosekana kwa kupigwa hatua katika mzozo huo kunakatisha tamaa, ingawa hawatopoteza matumani katika kutafuta dira ya kisiasa kwa Waisraeli na Wapalestina kuweza kuishi kwa amani kwa pamoja kwa dhana ya mataifa mawili.

Lebanon inaunga mkono hatua ya kuweka chini mtutu wa bunduki

Amenukuliwa akisema “Lazima tuhakishe hatuingii kwenye vita vingine, lakini lazima tufanye kila tuwezalo kupunguza hali hiyo, haswa kwa kuzingatia hali ya Lebanon.” Huku waziri wa mambo ya nje wa Lebanon amesema taifa lake linakaribisha juhudi za kusitisha mapigano na kushutumu kile alichokiita juhudi za kimfumo za Israel katika kuangamiza vijiji vya mpakani vya Lebanon.

Soma zaidi: Israel yakataa kusitisha mapigano na Hezbollah

Magari ya kijeshi ya Israel yameonekana yakisafirisha vifaru kuelekea mpaka wa kaskazini wa nchi hiyo na Lebanon, na makamanda wa jeshi wametoa wito wa askari wa akiba. Netanyahu anasema Israel inaipiga Hezbollah “kwa nguvu kamili” na haitasimama hadi itakapofika malengo.

Vyanzo: DPA/AFP

Related Posts