Masharti watumishi wanandoa kuungana | Mwananchi

Dodoma. Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imewataka watumishi wa umma wanaotaka kuhama kwa lengo la kuwafuata wenza wao wa ndoa kuwasilisha taarifa kwa waajiri wao kabla au ifikapo Oktoba 5, 2024.

Hata hivyo, waziri mwenye dhamana na wizara hiyo, George Simbachawene amesema kuna utaratibu utafuatwa, akionya wale watakaobainika kudanganya watafukuzwa kazi.

Barua kuhusu wito huo imetolewa na Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Juma Mkomi Septemba 24, 2024 kwenda kwa viongozi wa umma kwa ajili ya utekelezaji.

Barua hiyo imetumwa kwa makatibu wakuu, makatibu tawala wa mikoa, watendaji wakuu wa wakala wa Serikali, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma, wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji na wakurugenzi wa halmashauri za wilaya Tanzania Bara.

Mkomi katika barua hiyo amesema utaratibu wa uhamisho wa watumishi wa umma kutoka kwa mwajiri mmoja kwenda kwa mwingine umefafanuliwa katika Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 kwenye aya ya 4.17, Kifungu cha 8(3)(h) cha Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 vikisomwa kwa pamoja na Kanuni ya 106(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, Kanuni D.56 ya Kanuni za Kudumu Katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009 na aya ya 13(k) ya Taratibu za Uendeshaji Utumishi wa Umma za mwaka 2003.

“Vifungu vya sheria, kanuni na taratibu vilivyotajwa hapa juu, vinampa Katibu Mkuu (Utumishi) mamlaka ya kufanya uhamisho kwa watumishi miongoni mwa waajiri kwa nia ya kuwiainisha rasilimaliwatu iliyopo na kila kunapokuwepo sababu zenye masilahi kwa umma na ili kuboresha utendaji kazi serikalini,” amesema.

Amesema mbali na sababu za uhamisho zenye masilahi kwa umma, kupitia waraka wa barua yake wenye Kumb. Na. EA. 45/257/01/49 wa Machi 31, 2006 ofisi yake ilitoa utaratibu kwa watumishi ambao wana sababu za kuruhusiwa kuhama, ikiwamo kuwafuata wenzi wao wa ndoa.

“Katika utekelezaji wa waraka huu, watumishi wameendelea kuhama kwa lengo la kuwafuata wenzi wao wa ndoa. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa kutoka kwa watumishi wanaoomba uhamisho kwa lengo la kuwafuata wenzi wao wa ndoa.

“Kutokana na hali hii na ili kuiwezesha ofisi hii kuwa na taarifa kamili ya idadi ya watumishi wanaohitaji kuhama kwa lengo la kuwafuata wenzi wao wa ndoa mnaelekezwa kuwajulisha watumishi wenu kuwasilisha taarifa zao kwenu ili mziwasilishe taarifa hizo katika ofisi hii kabla au ifikapo Oktoba 5, 2024,” amesema Mkomi katika barua hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Septemba 27, 2024, kuhusu barua ya Mkomi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema familia zimekuwa zikiumia na watoto kukosa malezi kwa wazazi kufanya kazi kwenye maeneo tofauti, hivyo kuleta changamoto katika jamii.

“Si kila kada itawezekana hili, tumejaribu kuchukua hiyo ili kuangalia ni kwa kiasi gani lakini tutaanza kwa utaratibu wa kuangalia kwa mfano walimu na wale wanaofanya kazi katika sekta ya afya level (ngazi) za chini.

“Kwa mfano hawa ma- senior (waandamizi), wakurugenzi unasemaje habari ya kumfuata mke au mume. Level hiyo ni kubwa kwa hiyo tutaanza kwa awamu,” amesema.

Amesema lengo ni kuangalia na kuwasaidia watumishi wa ngazi za chini.

Simbachawene amesema cheti cha ndoa kitakachotakiwa ni kile ambacho kimesajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) na si vinginevyo.

Waziri amesema watakaoangaliwa kwa karibu ni wale waliofunga ndoa miaka mitatu iliyopita.

Amesema hata muda uliotajwa haumwezeshi mtu kwenda kutafuta ndoa ili aweze kuingia katika orodha ya kuwafuata wenza wao.

“Tumesema tunataka wajaze halafu tuone ikoje, sasa wale watakaojaza uongo kwa kweli tutawashitaki. Katika utumishi wa umma ukidanganya kwa tangazo kama la Katibu Mkuu Utumishi, ana uwezo wa kukufukuza kazi.

“Wasithubutu kuleta utani, halafu baadaye wakasema tulifikiria hatutachukuliwa hatua, watafukuzwa kazi, amesema.

“Kumdanganya mwajiri kama wale wa vyeti feki kwamba nimemaliza form four (kidato cha nne) kumbe hakumaliza wote wamefukuzwa kazi. Hata kwenye sekta ya ndoa ukimdanganya mwajiri tu kazi huna. Wasichukulie poa wala utani wataondoka watu hapa kimasihara hivyo hivyo.”  

Kuhusu ongezeko la wanaotaka kuhama, Simbachawene amesema baada ya ujazaji wa taarifa hizo ndipo watajua ukubwa kisha maamuzi ya Serikali yatafuata.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya amesema kuna mazingira ambayo unakuta asilimia 95 ya walimu katika shule husika ni wanawake na wanaume wameenda mjini.

“Unapouliza kwa nini hali hiyo, unajibiwa baadhi yao waliwafuata waume zao mijini na wengine unakuta hadi wanadanganya (ili kuhamishwa), unatetea hadi unafika mahali unaogopa,” amesema.

Amesema changamoto ipo wakati wanataka kuhama kufuata wenza wao bado kuna wanaotaka kuajiriwa lakini ajira ziko vijijini.

Hata hivyo, amesema shida ni kuwa suala la watumishi kuwafuata wenza wao ni suala la haki na msingi.

“Tunasubiri kuona wenzetu wanasemaje, angalau wapunguze umbali kwa kuwaleta katika sehemu iliyo karibu. Sisi nia yetu ni kuwaona (watumishi), wawepo karibu na familia zao. Lakini kama kuna ugumu basi wapunguze umbali,” amesema.

Nyamhokya amesema kuna mahali pengine wakuu wa wilaya wanalazimisha watumishi kukaa katika maeneo yao ya kazi hata kama familia yake iko mbali kidogo na anaweza kwenda na kurudi nyumbani kwa kutumia usafiri wa gari.

Ameishukuru Serikali kwa kufikia uamuzi huo ambao amesema umewagusa, akiomba wafikirie pia suala la wanaume kufuata wake zao walio mbali na maeneo wanayofanyia kazi.

“Tumeridhishwa sana na uamuzi wa Serikali wa kuangalia mahusiano ya familia na maadili ya watoto yanavyopotea kwa kumpa mzigo mzazi mmoja hasa wa kike. Kukaa na watoto wameshapevuka ambao wanahitaji maagizo na amri za baba ni changamoto,” amesema.

Amesema mazingira ya mwanamume kukaa mbali na familia yanasababisha wakati mwingine kila mmoja kuwa na hasira na mwenza wake na matokeo yake ndoa inavyunjika, hivyo kuzidi kuongeza tatizo katika jamii.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk Paul Loisulie amesema hilo ni jambo jema kwa sababu litawezesha familia ambazo baba na mama wanaishi maeneo tofauti kuungana.

Amesema watu walikuwa wakipata changamoto kubwa wanapokuwa mbali na familia zao na lilikuwa ni moja ya jambo ambalo lilikuwa likiwasumbua watumishi nchini.

“Hii itasaidia kwenye uwajibikaji kwa sababu italeta utulivu katika familia na kujenga familia. Uwekwe utaratibu kuwa watu hawataitumia vibaya, unajua kuna watu wengine wanaweza kutengeneza ndoa feki,” amesema.

Hoja ya Serikali kuangalia uhamisho kwa watumishi wa umma wenye ndoa iliwahi pia kuzungumzwa bungeni na Mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM) Charles Mwijage.

Akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2021/22, Mwijage alitaka  suala la uhamisho kwa watumishi wenye ndoa za kati ya miaka miwili hadi 10 kuangaliwa ili kuepuka watoto kuwaita baba zao wajomba.

Related Posts