Mila potofu zinavyoongeza mimba za utotoni Shinyanga

Shinyanga. Inasikitisha! Ndivyo unavyoweza kueleza katika simulizi za maumivu za wasichana walioozeshwa na wengine kuzalishwa wakiwa na umri wa miaka 13 hadi 15 mkoani hapa.

Kwa umri huo, wanapaswa kuwa shuleni, lakini wamejikuta wakitishwa mzigo wa kulea familia na wengine kuhudumia ndoa kutokana na baadhi ya mila zisizofaa mkoani humo kuwakandamiza na kupitia changamoto za ndoa na mimba za utotoni.

Wakizungumza leo Septemba 26, 2024 katika ziara ya Mtandao wa Kupinga Ndoa za Utotoni (TECMN) mkoani hapa, mabinti hao wameeleza changamoto walizopitia.

TECMN yenye mashirika 87 inafanya kampeni za kupinga ndoa hizo kwa kutembelea mikoa minne iliyoathirika zaidi.

Miongoni mwa simulizi hizo za kusikitisha ni ya Dotto Kashinje binti wa miaka 13 mwenye mtoto wa miezi minne aliyempa jina la Loveness.

Dotto alibakwa na kaka yake mtoto wa mama yake mkubwa walipokuwa wakichunga ng’ombe huko kijijini kwao Kishapu na kupata ujauzito.

Kutokana na umri wake, hata maziwa ya mtoto wake kunyonya hayatoki, hivyo analazimika kumnywesha maziwa ya ng’ombe.

Mazingira ya malezi ya binti huyo kwa mwanaye pia ni magumu, kutokana na ukweli kwamba naye anahitaji kulelewa kama mtoto, lakini analazimika kumlea mtoto wake ambaye nyakati zingine anaona aibu kumbeba mbele za watu akisema hapendi kwa kuwa wengi wanamshangaa na wengine kumcheka.

Akieleza alivyopata ujauzito huo anasema akiwa analelewa na mama yake mkubwa huko Kishapu, alikuwa na jukumu la kwenda kuchunga ng’ombe kila alipotoka shuleni.

Siku moja akiwa katika jukumu hilo, ndipo kaka yake huyo alimbaka

“Alinipa mimba akakimbia, tulienda polisi wakasema kama amekimbia basi aende asirudi tena Kishapu, ndio pale Polisi wakanileta huku (kituo cha kulea mabinti wanaopitia mazingira magumu cha Agape),” anasema.

Dotto anasema alihitimu darasa la saba mwaka huu na anasubiri matokeo ajiunge na sekondari kama atapata nafasi hiyo.

Binti mwingine, Kulwa Msengi yeye anasema alichukuliwa Mbeya na kudanganywa kwamba anakwenda Shinyanga kwa ndugu yake kumbe alipelekwa kwa mume.

“Wakati huo nilikuwa na miaka 11, tulitoka kwa basi kule na mtu ambaye mjomba na babu walinikabidhi kwake kumbe walinileta kuolewa,” anasema kwa uchungu huku akilengwa na machozi.

Kulwa ambaye hawajui wazazi wake, anasema alilelewa na bibi yake ambaye alifariki na kumuacha na babu na mjomba wake.

Anasema majirani ndiyo walimtoa kwenye hiyo ndoa kutokana na mateso aliyopitia, ambapo walikwenda kwenye nyumba aliyoolewa wakiwa na polisi na kumkamata na baadaye walimpeleka kuishi kwenye kituo cha Agape.

“Hivi sasa najifunza kusoma na kuandika, sikuwahi kwenda shule kabla, pia nimeambiwa nitajifunza ufundi,” anasema.

Kwa upande wake, Vumilia Mwangulumi anasema baba yao aliwakata yeye na kaka yake baada ya kuhitimu darasa la saba mwaka 2023.

“Baba alioa mke mwingine, waliachana na mama nikiwa darasa la tatu, nilipomaliza darasa la saba alitaka niolewe, tulifaulu na kaka yangu kwenda sekondari baba akasema hawezi kutusomesha, mimi nilisaidiwa na watu nikaletwa hapa, kaka yangu sijui yuko wapi,” amesema.

Anasema alipaswa kuanza kidato cha kwanza Januari mwaka huu, lakini kutokana na changamoto alizopitia alijiunga sekondari Machi 2024.

Mila, tamaa ya mali chanzo

Wakati takwimu za kimataifa kutoka utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) za mwaka 2015/16, zinaonyesha Mkoa wa Shinyanga ndiyo unaongoza kwa asilimia 59 ya ndoa za utotoni nchini, inaelezwa mila potofu na tamaa ya mali ndiyo chanzo.

John Myola, Mkurugenzi wa kituo cha Agape kinachojihusisha na malezi ya watoto waliookolewa kwenye mazingira magumu. Anasema mila za Kisukuma alozozitaja kama uswezi, ukango, mabasa na bukwilima ndiyo chanzo cha ndoa hizo.

“Tamaa ya mali ni kidogo, kwani kuna baba aliwaozesha binti zake wawili wa miaka 13 kwa ng’ombe 34, tulipokwenda kwake tumekuta ana ng’ombe kama 200, huyu baba sio kama hana ng’ombe bali ni tamaa tu,” anasema.

Anasema katika kabila la Wasukuma baada ya mavuno kuna mambo ya mila wanafanya akiitolea mfano ile ya Bukwilima anayosema inafanyika kijana anapokwenda kuoa.

“Wale vijana wa rika lake watakaomsindikiza kuoa nao wanaandaliwa mabinti vigoli kulingana na idadi yao kama vijana 100, 200 au zaidi na idadi hiyo hiyo ya mabinti.

“Baada ya harusi kiongozi wao anasema vijana wao wafunguliwe, ndipo mabinti wanatolewa kila mmoja anaondoka na wake iwe kwa kuridhia au kupigwa ngwala na lazima wafanye tendo la ndoa, hii inasababisha kwa kiasi kikubwa mimba na ndoa za utotoni,” anasema.

Kuhusu mila ya Uswezi anasema inahusisha ngoma ya mila isiyo na maadili.

“Hizi mila zingeangaliwa ingesaidia, fikiria hapa kituoni kwa mwaka napokea mabinti si chini ya 50 wanaookolewa na ndoa na mimba za utotoni,” anasema.

Myola anamtaja Dotto kama binti mdogo zaidi aliyempokea akiwa na miaka 12 na miezi kadhaa akiwa amepewa mimba huku wengine waliopokelewa pale na ujauzito wakiwa na miaka 14 na 15.

“Dotto sasa ana miaka 13, amejifungua miezi minne iliyopita lakini hata maziwa hayatoki, mtoto wake anakunywa maziwa ya ng’ombe tangu amezaliwa.

Daktari wa binadamu, Kuduishe Kisowile anasema mimba za utotoni ni hatari kwa kuwa via vya uzazi huwa havijakomaa na afya ya mama huwa hatarini.

“Zina madhara mengi ikiwamo kupata mtoto njiti au mwenye uzito chini ya unaotakiwa, vilevile watoto wanaozaa huwa hawana uelewa kuhusu ujauzito na kulea,” amesema.

Anasema wapo wanaopata shida kunyonyesha kama ilivyo kwa Dotto kwa kuwa mwili wake unakuwa haujakomaa kutengeneza maziwa ya kutosha kwa mtoto na anapompa maziwa ng’ombe si sahihi.

Kampeni kupinga mimba za utotoni

TECMN imetembelea mikoa ya Mara na Shinyanga ikifanya kampeni ya kutoa elimu ya madhara ya mimba za utotoni.

Mratibu wa Mtandao huo, Lilian Kimati anasema mashirika yaliyopo kwenye msafara huo (Caravan trip) ni pamoja na Msichana Initiative, Medea, Plan İnternational, My legacy, Binti Makini Foundation na Theatre Arts Feminist Group, yametoa elimu na misaada mbalimbali ya kijamii kwa kundi hilo katika mikoa hiyo.

Amesema Septemba 27, 2024 msafara huo utakwenda Tabora na Septemba 29 hadi 30 utakuwa Dodoma kuendelea na kampeni yao.

Itakumbukwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Msichana Initiative, Rebecca Gyumi ambaye ni, alishinda kesi aliyofungua ya madai namba tano ya mwaka 2016 dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akipinga uhalali wa kikatiba wa ndoa za utotoni.

Rebecca alishinda shauri hilo baada ya Mahakama hiyo kutamka kwamba vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ni vya kibaguzi na vinakwenda kinyume cha Katiba na kwamba vimepitwa na wakati.

Hata hivyo, Serikali kupitia kwa Mwanasheria Mkuu, ilikata rufaa kupitia shauri namba 204 la mwaka 2017, lakini mwaka 2019 baada ya Mahakama ya Rufani ilimpatia tena ushindi Rebeca na kutoa mwaka mmoja sheria hiyo iwe imefanyiwa marekebisho.

Pamoja na amri hiyo ya Mahakama, bado sheria hiyo haijafanyiwa mabadiliko.

Related Posts