Dar es Salaam. “Nimeshazoea, kwa sasa siwezi kufurahia kunywa pombe kali bila kuchanganya na energy drink (kinywaji cha kuongeza nguvu), pasipo kufanya hivyo ninahisi kama kinywaji changu kinapungua ladha,” anasema mmoja wa vijana akiwa katika moja ya maduka ya kuuza vinywaji jijini Dar es Salaam.
Huyo ni mmoja kati ya vijana ambao wamekuwa na utaratibu wa kuchanganya vinywaji vya kuongeza nguvu, maarufu kama ‘energy drink’ pale anapohitaji kunywa pombe kali.
Baadhi ya vijana wanaotumia mchanganyiko wa vinywaji hivyo pamoja na wauzaji wa pombe kali, wakizungumza na Mwananchi, wamebainisha sababu mbalimbali zinazochangia wao kupendelea kuchanganya ‘energy drink’ pamoja na vilevi vikali.
Ali Kalinga, ambaye ni mkazi wa Magomeni jijini Dar es Salaam, anasema anapokunywa mchanganyiko wa kinywaji hicho cha kuongeza nguvu na kilevi hufanya kinywaji chake kuwa na ladha nzuri, pia anasema anapokunywa hupata ‘stimu’ hivyo kumfanya aweze kuchangamka.
Kwa upande wake Daniel, anasema anapochanganya kilevi pamoja na ‘energy’ huhisi kulewa kwa haraka zaidi kuliko anapokunywa bila kuchanganya.
“Ukichanganya pombe kali na energy, kwa kuwa ina ladha ya sukari, inafanya kilevi kupungua ladha ya ukali,” anasema.
Hata hivyo, wengine wanapokosa fedha ya kununua kinywaji hicho au vinywaji laini hulazimika kuweka kiasi kidogo cha sukari ili waweze kupata ladha nzuri katika vinywaji vyao, kama anavyoeleza Amina Mandia, mkazi wa Kimara.
Mandia, ambaye ni muuzaji wa duka la vinywaji, ikiwemo pombe, anasema baadhi ya wateja wanaotaka kuchanganyiwa husema wakifanya hivyo huwapa motisha ya kunywa zaidi.
Hata hivyo, wataalamu pamoja na tafiti mbalimbali za afya zilizowahi kufanyika zinaonyesha kuwa uchanganyaji wa vinywaji hivyo unaweza kuleta athari katika figo, ini, moyo pamoja na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula kwa mtumiaji.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa Afya na Mazoezi kutoka Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyo ya kuambukiza, Dk Waziri Ndonde anasema tabia ya kuchanganya pombe na vinywaji vya kuongeza nguvu ‘energy drink’ na kunywa ni hatari kwa afya ya binadamu, kwani husababisha ini kushindwa kufanya kazi vizuri.
“Mtu anapokunywa pombe analipa ini kazi ya kuchakata kiasi cha pombe kilichoingia mwilini, pia hata unapokunywa vinywaji vya kuongeza nguvu unapochanganya unalipa kazi kubwa ini na hii husababisha ini kufa au kushindwa kufanya kazi vizuri,” anasema.
Dk Ndonde anafafanua kuwa ini ni kati ya viungo vya lazima katika mwili wa binadamu ili kuwezesha maisha na kazi yake kubwa ni kama chujio, ambalo huchuja damu inayozunguka mwilini.
Anasema ini linaposhindwa kufanya kazi vizuri, sumu mbalimbali zinazoingia mwilini kwa njia ya chakula au vinywaji zitashindwa kuchujwa vizuri na kubaki mwilini, jambo ambalo ni hatari kwa afya.
Kwa upande wake Mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daudi Gambo anasema ini linaposhindwa kufanya kazi na sumu kuendelea kubaki mwilini husababisha uharibifu wa viungo vingine, ikiwemo figo kushindwa kufanya kazi vizuri.
Dk Gambo anasema figo ni kiungo chenye kazi ya kuchuja takamwili na kuzitoa nje kwa njia ya mkojo na kupunguza kiasi cha maji kilichozidi mwilini.
Anasema figo linaposhindwa kufanya kazi vizuri husababisha mwili kuwa na mrundikano wa maji yaliyozidi, ambayo yangehitajika kutolewa kwa njia ya mkojo.
“Pia husababisha takasumu na mabaki mengine yasiyohitajika mwilini kurundikana, hali inayoweza kuleta changamoto mbalimbali katika mwili,” anasema.
Dk Gambo anasema baadhi ya changamoto hizo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, pamoja na mafuta yasiyohitajika mwilini.
Hata hivyo, Dk Ndonde naye anaongeza kuwa kutokana na takasumu kujaa mwilini zinazotokana na figo pamoja na ini kufa au kushindwa kufanya kazi yake vizuri, huweza kusababisha changamoto katika ubongo.
Anasema ubongo unapata virutubisho muhimu pamoja na hewa ya oksijeni kupitia mzunguko wa damu ndani ya mwili wa binadamu, hivyo kama figo na ini limeathirika kemikali zilizoko katika vinywaji au vyakula hupita moja kwa moja katika ubongo, jambo linaloweza kuleta athari katika mwili.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Dk Isaya Mhando anasema unywaji wa mchanganyiko wa vinywaji hivyo huleta athari katika mishipa inayopitisha damu, moyo pamoja na katika mfumo wa uzazi, hasa kwa wanaume.
Anasema mtu anapokunywa mchanganyiko wa vinywaji hivyo, hufanya mishipa ya fahamu kusisimka kupita kiasi na pia kufanya mapigo ya moyo kuongeza kasi.
“Mapigo ya moyo yakiongezeka damu nayo itasambaa kwa kasi katika maeneo mbalimbali ya mwili, ikiwemo sehemu za uzazi na kwa upande wa mwanamume unaweza kufanya uume kusimama na kumfanya kuwa na matamanio ya kufanya tendo la ndoa,” anasema.
Hata hivyo, Dk Mhando anafafanua kuwa changamoto inayoweza kujitokeza ni kushindwa kufanya tendo hilo kwa muda mrefu.
Pia anasema inamuweka mhusika katika hatari ya kupata uraibu pamoja na kujenga tabia ya kushindwa kufanya tendo la ndoa hadi anapokunywa vinywaji hivyo.
Anasema pombe inapoingia katika mwili wa binadamu inakwenda kuzuia kemikali ambayo inamsaidia mtu kuwa na soni, inayomsaidia kujua yuko wapi, ni maneno gani au matendo gani anapaswa kufanya kutokana na eneo alipo.
“Inasababisha mtu anaweza kufanya matendo ambayo hayakubaliki katika jamii,” anasema.
Wakati wataalamu wakieleza hatari ya kuchanganya vinywaji hivyo, inaelezwa kuwa Serikali hutumia kati ya Sh88.1 bilioni mpaka Sh110.2 bilioni kila mwaka kwa wagonjwa wasio na uwezo, wanaopata tiba ya kuchuja damu kwa utaratibu wa misamaha.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kati ya asilimia 30 mpaka 40 ya wanaolipia huduma ya kusafisha damu, wapo kwenye misamaha ya kiwango tofauti, kuanzia wanaolipia Sh20,000 mpaka Sh100,000 kwa mzunguko mmoja, huku asilimia 10 kati yao hawalipi chochote.
Hadi Januari 2024 takwimu zinaonyesha jumla ya wagonjwa 3,500 wanapata huduma ya dialysis ikilinganisha na wagonjwa 1,017 ambao walikuwa kwenye huduma hiyo Agosti 2019, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 70 ndani ya miaka mitano.