Ramani kumfanya msichana atimize ndoto zake hii hapa

Dar es Salaam. Wakati mikakati ikiendelea kufanywa na wadau kuhakikisha mazingira rafiki kwa msichana kupata elimu na kufikia ndoto zake, msisitizo umetolewa wa ushirikiano wa makundi tofauti kufanikisha hilo.

Msisitizo unatolewa kipindi ambacho nchi inashuhudia kuendelea kuwapo kwa ndoa za utotoni na ukatili wa kijinsia, ambao ni chanzo cha kuwafanya mabinti wengi kushindwa kuendelea na masomo.

Katika kuliona hilo, Shirika la Plan International leo Ijumaa, Septemba 27, 2024 limezindua kampeni ya ‘Sikia Sauti Zetu’ ya miaka mitatu inayolenga kuwafikia wasichana nchini.

Kampeni hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya msichana inayoadhimishwa duniani kila Oktoba 11.

Mkurugenzi Mkazi wa Plan International Tanzania, Jane Sembuche amesema ni wakati wa kudai fursa zaidi ili kila msichana aweze kuwa kile anachotaka kuwa.

Amesema dunia inahitaji kuona nguvu kubwa inayotokana na kufungulia wasichana dunia ili waonyeshe uwezo wao.

Amesema ni muhimu kushughulikia masuala hayo muhimu kwa haraka na kufanya uamuzi sahihi.

“Kwa kufanya hivyo, tunatengeneza kesho ambayo wasichana si tu wanapewa ulinzi na elimu, bali pia wanakuwa na uwezo wa kuongoza na kufanya maamuzi. Sauti zao si tu kusikika bali zinakuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii zetu na Taifa letu,” amesema.

Amesema Serikali inapaswa kuunda sera rafiki na kuongeza: “Itunge na kuhakikisha utekelezaji wa sera zinazounga mkono malengo ya kampeni hii ili kutatua changamoto zilizopo.”

Pia itenge rasilimali fedha za kutosha kusaidia miradi na programu zinazolenga kukuza haki za wasichana na kutia chachu safari yao ya kuelekea kuwa viongozi shupavu wenye mafanikio.

“Asasi za kiraia ziendelee kuhamasisha kuhusu masuala yanayokabili ustawi hasa ustawi wa wasichana ili kuleta mabadiliko kupitia uchechemuzi na afua za msingi,” amesema.

Amesema Azaki zinaweza kutekeleza programu katika ngazi ya jamii, zikijitolea maarifa na ujuzi wao wa ndani, huku washirika wa maendeleo na misaada wakiendelea kutoa utaalamu wa kiufundi na msaada wa kubuni na kutekeleza programu zenye ufanisi.

“Kusaidia kujenga uwezo wa mashirika na taasisi za ndani. Kutoa msaada wa kifedha kwa mipango mikakati na afua mbalimbali,” amesema.

Jane amesema, “tunapojitahidi kuwawezesha wasichana na kuimarisha sauti zao, ni muhimu kushughulikia baadhi ya masuala makubwa wanayokabiliana nayo.

“Ndoa za utotoni zinawanyang’anya wasichana utoto wao, elimu, na fursa za baadaye. Inadumisha mzunguko wa umaskini na ukosefu wa usawa. Lazima tuweke sheria zinazopiga marufuku ndoa za utotoni, kuhamasisha kuhusu madhara yake, na kutoa msaada kwa familia ili kuzuia hilo.”

Kuhusu ukosefu wa usawa wa elimu amesema wasichana wengi wananyimwa haki hiyo kutokana na vikwazo vya kifedha, vizuizi vya kitamaduni, na miundombinu isiyo na uwezo.

“Tunahitaji kuhakikisha kila msichana anapata nafasi ya kupata elimu jumuishi na ya kiwango bora kwa kujenga shule zaidi, na kuunda mazingira salama ya kujifunza,” amesema.

Kuhusu unyanyasaji wa kijinsia amesema suala hilo linakwenda pamoja na unyanyasaji wa kimwili, kihisia, na kingono, unakumbusha kwa nguvu afya, ustawi, na uwezo wa wasichana kufanikiwa.

“Tunahitaji kutekeleza na kuimarisha sheria kali dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, kutoa huduma za msaada kwa waathirika, na kuwafundisha jamii kubadilisha mitazamo na tabia mbaya,” amesema.

“Haitoshi kwa wasichana kuonekana na kusikilizwa, lazima washiriki kwa kazi katika kuunda uamuzi unaoathiri maisha yao. Tunahitaji kuunda majukwaa ambapo wasichana wanaweza kushiriki katika majadiliano na michakato ya uamuzi katika ngazi zote, kuanzia baraza la mitaa hadi majukwaa ya kitaifa. Kuwatia moyo na kuwasaidia wasichana kuchukua nafasi za uongozi,” amesema.

Katika mkutano huo na waandishi, miongoni mwa wasichana wanufaika wa kampeni hiyo walieleza mapito waliyoyapitia.

Mwanafunzi wa Chuo cha Kijeshi cha Sayansi na Tiba, Lugalo, Mariam Surve amesema: “Nimekuwa kwenye mazingira ambayo naona baba na mama wanahangaika huku na huko kutafuta fedha za kunisokesha, nakumbuka kuna siku walikosa hela ikanifanya nisiende shule wiki mbili hivi.”

“Hiyo ilinivunja moyo na kuona siwezi kufika malengo yangu na hasa nikiangalia katika familia yetu hakuna msichana aliyesoma ambaye ningekuwa namwona kama mfano wa aliyefanikiwa,” amesema Mariam.

Amesema wazazi wake walipambana na alipofikia anaona anakwenda kutimiza ndoto zake kwani jamii kwa ujumla imeanza kuwa na mtazamo chanya kuhusu wanawake.

“Nilipochaguliwa katika kampeni hii ni fursa kubwa kwani nitakuwa mfano wa kuwa tumaini na kupitia kampeni hii nitapata fursa ya kufikia ndoto zangu. Hasa nikiona kwa sasa wanawake wanashika nafasi mbalimbali kama urais, mawaziri, wabunge, wakurugenzi wa taasisi,” amesema.

Zafarani Ramadhani, Mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shahada ya Kwanza ya Kemia amesema: “Nimetokea familia ambayo hawajasoma masomo ya sayansi. Walikuwa wananiambia niacha sitaweza lakini mimi niliweza na nikamaliza masomo vizuri.”

Amesema amekuwa mdau wa kuwahamamisha mabinti wenzake kusoma masomo ya sayansi. Amesema pia ni mdau wa mazingira ambayo ameeleza yanapaswa kuwa salama.

Feslister Alex, mwanafunzi wa UDSM amesema, “namshukuru Mungu nipo hapa, nimelelewa katika familia kwa kunyanyapaliwa kwa ulemavu wa ngozi (ualbino) ilikuwa changamoto kubwa.”

“Nilitaka kuwa daktari nikaambiwa siwezi. Nikataka kusoma Mass Communication wakasema siwezi kuona vizuri kuchukua picha. Nikaenda kusoma fashion,” amesema.

Related Posts