Simiyu. Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Kenani Kihongosi ameagiza Polisi wilayani Maswa kuondoka na wananchi wawili waliotoa tuhuma za kuwepo vitendo vya utekaji, kupotezwa na kuuawa watu wazima na watoto lakini wakashindwa kuthibitisha ili kupata maelezo ya kina kutoka kwao.
Ametoa agizo hilo leo Ijumaa Septemba 27, 2024 baada ya wakazi wa vijiji vya Sangamwalugesha na Mbaragane kutoa malalamiko mbele yake wakidai hali ya ulinzi na usalama kwenye vijiji vyao si shwari kwa kuwa kuna vitendo vya watoto na watu kupotea, kutekwa na kuuawa.
Festo Mikael, mkazi wa Kijiji cha Sangamwalugesha amesema hali ya ulinzi na usalama si shwari kutokana na kuwepo kwa vitendo vya watoto kuuawa, kupotea na kutekwa.
Amesema kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanaishi kwa mashaka kwani ikifika saa 12.00 jioni ni lazima wawe ndani ya nyumba kwa kuhofia maisha yao na ya watoto wao.
“Hapa Sangamwalugesha tuna shida, roho ziko hatihati, wananchi wanaishi kwa mashaka ikifika jioni saa 12.00 unakaa ndani na mtoto kwa kuhofia vitendo vya kutekwa, kupotezwa na kuuawa wakati Jeshi letu la Polisi lipo lakini maisha yetu yana dukuduku,” amesema.
Baada ya malalamiko hayo Kihongosi alimtaka kuthibitisha kauli hiyo lakini alishindwa, ndipo alipowauliza wananchi kama matukio hayo yapo, ambao walikana.
“Niwaulize wananchi katika kijiji hiki cha Sangamwalugesha na kata hii kuna matukio ya watoto kutekwa na kuuawa?”
Wananchi walisema hakuna matukio hayo.
“Kama hakuna matukio hayo kama mlivyojibu inakuwaje mtu anakuja mbele ya mkutano na kutoa taarifa za uongo ambazo zinazua taharuki kwa jamii?” amehoji.
Kwa upande wake, Costantine Samo mkazi wa Kijiji cha Mbaragane amesema kwa sasa kumekuwa na matukio ya watu kuuawa na kutolewa nyongo, hivyo kumtaka Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Simiyu na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Maswa kutoa maelezo ya kina juu ya kuwepo kwa matukio hayo.
“Kumekuwa na matukio ya watu kuuawa na kutolewa nyongo, RPC na OCD wapo hapa nataka mtupatie maelezo juu ya kuwepo kwa matukio hayo,” amesema.
Alipotakiwa kuthibitisha uwepo wa matukio hayo alishindwa.
Kihongosi alimuagiza Mkuu wa Polisi Wilaya ya Maswa, Mrakibu Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SSP), Maganga Ngosha kuwachukua wananchi hao kwa lengo la kupata maelezo ya kina kutoka kwao juu ya malalamiko waliyotoa.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa taarifa, Kihongosi ameonya kuhusu za uongo ambazo zinaweza kusababisha taharuki katika jamii.
Ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanapata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo vya kuaminika na kuepuka kusambaza habari ambazo hazijathibitishwa.
Amesema kwa sasa imezuka tabia kwa baadhi ya wananchi kutoa taarifa za uongo za watu kutekwa, kupotea na kuuawa katika maeneo yao wakati matukio hayo hayajatokea hali inayoweza kuvuruga amani na utulivu wa wananchi.
Amewataka wananchi kuacha upotoshaji kwenye mikutano ya hadhara na kuacha kutafuta umaarufu mbele za watu kwa kutoa taarifa za uongo.
Kihongosi yuko katika ziara ya siku sita kwenye wilayaniza mkoa huo inayolenga kusikiliza na kutatua kero zinazowakabili wananchi.