‘Serikali iangalie sera zisizo rafiki kwa wazalishaji’

Dar es Salaam. Serikali imetakiwa kuangalia sera zisizo rafiki kwa wazalishaji hapa nchini na iweke miundombinu rafiki ya barabara ili kurahisisha usafirishaji.

Wito huo umetolewa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Kampuni ya  Alaf Limited Tanzania,  Hawa Bayumi, baada ya  Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kutembelea banda la kampuni hiyo katika Maonyesho ya Kimataifa ya Viwanda (TIMEEXPO 2024) aliyoyafungua Septemba 26 2024 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, meneja huyo ameipongeza Serikali kwa kuhakikisha mazingira ya uzalishaji na biashara kwa jumla hapa nchini ni mazuri.

“Tunatoa wito kwa Serikali iendelee kuboresha mazingira haya zaidi ikiwamo kuangalia sera ambazo sio rafiki kwa wazalishaji na pia kuweka miundombinu sawa ikiwamo barabara ili usafirishaji uwe rahisi,” amesema Hawa.

Amesema Alaf itaendelea kutoa suluhisho sahihi la ujenzi kwa jumla ikiwamo kuja na teknolojia mpya inayotumika kujenga maghala ya nafaka mkoani Ruvuma ambayo imezingatia ubora wa hali ya juu.

Alaf ni miongoni mwa kampuni zinazoshiriki maonyesho ya TIMEXPO 2024 yaliyoanza Septemba 26 na yatamalizika Oktoba 2, 2024.

Awali, Dk Biteko alieleza kuridhishwa na huduma na bidhaa za Alaf Limited Tanzania na kuitaka kampuni hiyo iendelee kuzingatia ubora.

“Nawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayofanya, na pia kwa kushiriki katika maonyesho haya makubwa,” amesema Dk Biteko.

Hata hivyo, Biteko alihitaji kufahamu kama  suala la umeme kiwandani hapo (Alaf) lilishashugulikiwa baada ya kuwepo na malalamiko ya kukatikakatika kwa umeme mara kwa mara, jambo ambalo lilikuwa linaathiri uzalishaji.

Akijibu suala hilo, Meneja wa Alaf amesema: “Mheshimiwa tunakushukuru mno maana suala hili limeshashugulikiwa na sasa uzalishaji unaendelea vizuri.”

Related Posts