WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amekanusha wagonjwa kusafirishwa kwa pikipiki wakiwa wamewekwa kwenye matenga kupelekwa hospitali, wilayani Tunduru. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Badala yake, Mchengerwa amesema mwaka jana serikali ilitoa magari 535 ya wagonjwa nchi nzima na wilaya hiyo ilipata magari manne (4), ya kubebea wagonjwa.
Ametaja Vituo vya Afya vilivyopewa magari wilayani Tunduru kuwa ni Nakapanya, Matemanga, Mtesi na Nyalasi; na kwamba yanafanya kazi saa 24. Aidha, amesema rufaa zote zinaratibiwa kwa utaratibu maalumu na sio kuchangisha wananchi.
Mchengerwa aliyasema hayo jana wakati akitoa salamu za Wizara kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi wa Tunduru uliofanyika wilayani humo.
Aidha, akikuwa akijibu hoja ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, aliyeeleza kusikitishwa na kitendo cha wagonjwa wa Kata ya Mchoteka wanaokwenda kutibiwa Hospitali ya Mbesa, kusafirishwa kwenye matenga kutokana na gharama kubwa ya gari la wagonjwa.
Kamera ya MwanaHALISI ilinasa picha ya mgonjwa akisafirishwa kwenye pikipiki huku akiwa kwenye tenga, alipohojiwa mgonjwa huyo alisema hakuna magari ya kusafirishia wagonjwa na yaliyopo huwagharimu wananchi fedha nyingi, hivyo wanashindwa kumudu.
“Utaratibu unaotumika kusafirisha wagonjwa nikutumia magari ya kubebea wagonjwa, kwa kutumia madereva ngazi ya jamii waliosajiliwa wakati wa mfumo wa M-Mama. Mfumo huu unahusika na kusafirisha wajawazito na watoto wachanga bila malipo yoyote,” amesema Mchengerwa.