Sifa ya chama cha siasa kushiriki uchaguzi

Dodoma. Sharti la kuwataka wagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa wawe wanachama wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, linawahusu pia wapigakura kujua vyama vyenye usajili wa muda ambavyo havina sifa ya kushiriki uchaguzi huo.

Ni muhimu kwa wapigakura kufahamu kanuni za uchaguzi wa Serikali za mitaa za mwaka 2024, zinaeleza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi watatakiwa kuwa wanachama na wadhaminiwa wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Hadi sasa ni vyama vya siasa 19 ndivyo vyenye usajili wa kudumu nchini ambavyo vina sifa ya kusimamisha wagombea kwenye vijiji 12,333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 kwa nafasi mbalimbali za uongozi ikiwamo mwenyekiti na wajumbe.

Vyama vya siasa ambavyo havina usajili wa kudumu, yaani vyenye usajili wa muda, havitaruhusiwa kusimamisha wagombea katika uchaguzi huu.

Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vinakidhi vigezo vya kisheria na taratibu zilizowekwa ili kuthibitisha uwepo wao na uwezo wa kuongoza na kusimamia masuala ya kisiasa kwa muda mrefu.

Kupata usajili wa kudumu kunahitaji vyama vya siasa kukidhi masharti mbalimbali yanayoonyesha kuwa vinaweza kushiriki siasa za muda mrefu kwa uwajibikaji katika maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar (Pemba na Unguja).

Vyama vya muda vinakuwa katika hatua za awali za kujaribu kujijenga na havina uthibitisho wa muda mrefu wa uwezo wao wa kushiriki siasa kwa ufanisi na kwa uadilifu, pia kama vimekubalika kwenye maeneo yote ya Jamhuri ya Muungano.

Kuwa na usajili wa kudumu kunahakikisha kwamba chama kimepata nafasi ya kujitambulisha kwa wananchi, kufuata taratibu za kisheria na kuwa na uthabiti wa kisiasa unaohitajika.

Kwa hiyo, ni muhimu kwa Watanzania kufahamu kuwa vyama hivi vimepata kibali cha kudumu na vinaaminika, hivyo vinastahili kusimamisha wagombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa.

Ushiriki wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu pekee ni muhimu kwa ajili ya kulinda mchakato wa kidemokrasia na kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa utulivu na uwazi.

Vyama vya siasa vyenye usajili wa muda vinaweza kuwa bado vinaimarisha misingi yake ya kisiasa na kiutawala, hali ambayo inaweza kuathiri uwezo wake wa kushiriki kikamilifu na kwa uwajibikaji katika uchaguzi.

Wananchi wanapaswa kufahamu, kuzuia vyama vyenye usajili wa muda kushiriki uchaguzi ni njia ya kuhakikisha wagombea wanaowekwa na vyama wanatoka katika taasisi zilizo na misingi thabiti ya kikatiba na kiuongozi.

Pia, wananchi wanapaswa kufahamu mfumo thabiti wa vyama vyenye usajili wa kudumu unatoa uhakika kwa wapigakura kujua wagombea wanatoka katika vyama vyenye uwezo wa kushiriki siasa za kitaifa na za muda mrefu.

Wapigakura, wanapaswa kujua wagombea wanaotoka kwenye vyama vilivyo na usajili wa kudumu, wanapunguza mkanganyiko na kuwasaidia kufanya maamuzi bora zaidi.

Kimsingi vyama vyenye usajili wa muda vinaweza kuwa bado havijajulikana vyema na vinaweza kuleta changamoto kwa wapigakura, kujua malengo yao na sera zao.

Wananchi wanapaswa kufahamu uchaguzi wa Serikali za mitaa ni wa ngazi ya chini ambako wanachagua viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji, ni muhimu kwamba mchakato huo uwe wazi na usio na utata kwa wapigakura.

Ni vyema ikaeleweka kuwa, vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu tayari vinajulikana kwa wapigakura, vina sera ambazo zimekuwa zikifahamika na kupimwa, hivyo vinatoa fursa bora kwa wananchi kufanya maamuzi sahihi.

Kwa kuzingatia kuwa Tanzania ina vijiji 12,333, vitongoji 64,274 na mitaa 4,269 ambavyo vitashiriki uchaguzi wa viongozi, vyama vyenye usajili wa kudumu vina uwakilishi wa kitaifa wa kufika maeneo mengi ya nchi.

Hii inasaidia kuleta uwakilishi wa kitaifa wa wagombea wanaosimamishwa na vyama vyenye usajili wa kudumu katika uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 27, mwaka huu.

Ushiriki wa vyama vyenye nguvu ya kitaifa unasaidia kuhakikisha kuna uwiano wa maendeleo katika ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji.

Pia, vyama vyenye usajili wa kudumu vina ufuatiliaji wa kisheria na kikatiba, hivyo vinaeleweka na wananchi na vinaweza kuwajibishwa katika kushiriki uchaguzi.

Kama vyama vya muda vingekuwa vinaruhusiwa kushiriki, mchakato mzima wa uchaguzi ungeweza kupoteza uaminifu kwa wapigakura kwa kuwa, vyama hivyo vinaweza kuwa na changamoto za uwajibikaji na kuwa na maamuzi ya muda mfupi bila malengo ya muda mrefu.

Vyama vya kudumu vinazingatia sera na miongozo ya kudumu, hali inayoongeza imani kwa wapigakura kwamba mchakato wa uchaguzi ni wa haki na usawa.

Ni muhimu kwa Watanzania kuelewa kuwa kushiriki kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu uchaguzi wa Serikali za mitaa wa Novemba 27, 2024, ni hatua muhimu inayolenga kuimarisha mfumo wa kidemokrasia nchini.

Vyama hivi vina uthabiti wa kisiasa, vinafuata sheria na vina uwakilishi wa kitaifa unaowapa wananchi nafasi nzuri ya kuchagua viongozi bora wa mitaa, vijiji na vitongoji.

Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 (iliyofanyiwa marekebisho kadhaa) inatambua vyama vya siasa kwa mujibu wa aina mbili za usajili; usajili wa muda na usajili wa kudumu.

Ili chama kiweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa lazima kipate usajili wa kudumu kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Pia, Sheria ya Vyama vya Siasa inaeleza kwamba chama cha siasa hakiwezi kushiriki katika uchaguzi wowote, ikiwa hakijapata usajili wa kudumu.

Hii inamaanisha kuwa chama kinachotaka kusimamisha wagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kinapaswa kuwa na usajili wa kudumu.

Msajili wa Vyama vya Siasa huhakikisha chama kilichoomba usajili wa kudumu kimekidhi vigezo vyote vya kisheria na katiba ikiwamo kuwa na idadi inayotakiwa ya wanachama kutoka mikoa kadhaa ya Zanzibar na Tanzania Bara na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi.

Vyama vinavyokuwa na usajili wa muda vinaonekana kuwa bado vipo katika hatua za awali za kutimiza masharti hayo.

Kwa jumla, vyama vya siasa visivyokuwa na usajili wa kudumu havitaweza kusimamia wagombea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa sababu ya kutokidhi matakwa ya kisheria yaliyowekwa na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Usajili wa kudumu ni ishara ya kwamba chama kimekidhi masharti yote ya kisheria ikiwamo kuwa na wanachama wa kutosha, kufuata katiba ya chama na kuendesha shughuli zake kwa uwazi.

Sheria hizi zinalenga kuhakikisha  vyama vinavyoshiriki uchaguzi vina uwezo wa kisiasa, uwajibikaji na uthabiti wa kutosha kushiriki mchakato wa uchaguzi kwa haki na uwazi.

Related Posts