New York. Katika hali isiyo ya kawaida, baadhi ya viongozi na wanadiplomasia waliohudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) jijini New York, Marekani wameonekana wakitoka nje wakati Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alipoanza kuhutubia mkutano huo.
Sintofahamu hiyo imetokea leo Septemba 27, 2024 kwenye mkutano wa 79 wa Baraza la Umoja wa Mataifa uliowakutanisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali duniani, kwa mujibu wa mtandao wa Daily Mail.
Hata hivyo, duru za kimataifa zinaeleza kwamba hatua ya viongozi na wanadiplomasia hao kukacha hotuba ya Netanyahu ni sehemu ya kupinga vita vinavyoendelea Gaza ambapo zaidi ya watu 42,252 wamepoteza maisha hasa wanawake na watoto.
Vilevile, kuongezeka kwa vita vya hivi karibuni nchini Lebanon vinavyolenga mamia ya wanachama wa Hezbollah na raia, vinatajwa kuwa sababu ya makumi ya wanadiplomasia na wajumbe kutoka nchi kadhaa kuondoka ukumbini wakati akihutubia.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamiiĀ zimewaonyesha wakiondoka ukumbini wakimuacha Netanyahu katika jukwaa akihutubia.
Hata hivyo, wakati Netanyahu, anawasili mjini New York, jana AlhamisiĀ waandamanaji wanaopinga vita huko Gaza walikusanyika karibu na makao makuu ya Umoja wa Mataifa wakionyesha kupinga vita hivyo.
Ingawa katika hotuba hiyo kwa mujibu wa tovuti ya UN, Netanyahu amesema awali alikuwa na nia ya kutokuja kwenye mkutano huo, lakini baada ya kusikia kile alichokiita uongo na kashfa zinazotolewa dhidi ya nchi yake na viongozi wengine, aliamua kwenda ili kufafanua na kuliweka sawa suala hilo.
“Niliamua kuja hapa kuwasemea watu wangu, kuongea kwa ajili ya nchi yangu na kusema ukweli, Israel inatamani amani. Tunakabiliana na maadui wakali na wakubwa wanaotaka kutuangamiza, na lazima tujilinde dhidi ya wauaji hawa wakatili ambao sio tu wanataka kutuangamiza, bali kuharibu ustaarabu wetu wa kawaida na kuturudisha sote kwenye enzi ya giza ya dhuluma na ugaidi,” amesema.
Netanyahu amenukuliwa na kituo cha utangazaji cha DW akisema Serikali yake inataka amani, huku akionya pia kuwa iko tayari kupigana kuwalinda raia wake.
Amesema maadui wa Israel wanataka kuwaangamiza. Ameikosoa vikali Iran kwa kuhusika na mzozo huo wa Mashariki ya Kati huku akisema Israel ilikuwa inajilinda dhidi ya jirani yake huyo.
Katika mkutano huo, Kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Tusimwache mtu nyuma: tushirikiane kwa ajili ya kuendeleza amani, maendeleo endelevu na utu wa binadamu kwa vizazi vya sasa na vijavyo”.